Tafuta

Vatican News
Papa Francisko ameamua kwamba, tarehe 2 Machi 2020, Nyaraka za Siri za Papa Pio XII kufunguliwa kwa watafiti! Papa Francisko ameamua kwamba, tarehe 2 Machi 2020, Nyaraka za Siri za Papa Pio XII kufunguliwa kwa watafiti!  (Vatican Media)

Nyaraka za Papa Pio XII Kufunguliwa 2 Machi 2020! Vatican!

tarehe 2 Machi 2020, takribani miaka 80 tangu Mtumishi wa Mungu Pietro di Eugenio aliyekuja kujulikana kama Papa Pio XII, alipochaguliwa kuliongoza Kanisa kunako mwaka 1936, kufungua rasmi Pango Hifadhi la Kihistoria la Nyaraka za Siri za Vatican. Hizi ni Nyaraka zote za utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, hadi kifo chake tarehe 9 Oktoba 1958, huko Castel Gandolfo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 4 Desemba 2018 alitembelea Maktaba ya Kitume ili kuangalia shughuli zinazotekelezwa mahali hapa! Tarehe 2 Machi 1939, Mtumishi wa Mungu Pio XII alichaguliwa kuliongoza Kanisa kati ya nyakati ambazo Kanisa lilikuwa linakumbwa na mawimbi mazito katika maisha na utume wake. Imegota miaka 80 tangu tukio hili lilipotokea. Itakumbukwa kwamba, Karne ya XX ilikuwa imejeruhiwa sana na Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia. Ni katika muktadha huu, wasomi na wanazuoni wengi wakajitaabisha kutafiti kwa kina na mapana ili kubainisha mchango wa Mtumishi wa Mungu Papa Pio XII. Matokeo yake ni kwamba, mambo makuu manne yameibuliwa kuhusu ubora wa: shughuli zake za kichungaji mintarafu taalimungu, maisha yake ya kiroho pamoja na shughuli zake za kidiplomasia. Wasomi wengi walitamani sana kuingia kwenye Pango Hifadhi la Kihistoria la Nyaraka za Siri za Vatican ili kujionea wenyewe ukweli wa mambo.

Ili kukata kiu ya wasomi hawa, Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI kunako mwaka 2006 akatoa ruhusa kwa wafanyakazi katika Pango Hifadhi la Kihistoria la Nyaraka za Siri za Vatican kuanza kuandaa vyema nyaraka za maisha na utume wa Mtumishi wa Mungu Papa Pio XII, ambaye amekuwa rejea kwa watakatifu Paulo VI na Yohane Paulo II. Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu, tarehe 4 Machi 2019, alipokutana na kuzungumza na viongozi, watunzi wa vitabu pamoja na wafanyakazi wa Pango Hifadhi la Kihistoria la Nyaraka za Siri za Vatican. Baba Mtakatifu amekaza kusema, hii ni kazi ambayo inatekelezwa katika hali ya ukimya mbali kabisa na vurugu, ili kujenga na kuliimarisha Kanisa, liweze kutekeleza dhamana na wajibu wake wa kuwapeleka watu mbinguni, kwa kuendelea kuzamisha mizizi yake katika Fumbo la Umwilisho, katika historia na nyakati!

Wafanyakazi katika Pango hifadhi ni watu wanaochangia katika mchakato wa kupyaisha maisha na utume wa Kanisa, ili liendelee kuwa kijana zaidi, kwa sasa na kwa siku za usoni! Baba Mtakatifu ameamua kwamba, tarehe 2 Machi 2020, mwaka mmoja kuanzia sasa, takribani miaka 80 tangu Mtumishi wa Mungu Pietro di Eugenio aliyekuja kujulikana kama Papa Pio XII, alipochaguliwa kuliongoza Kanisa kunako mwaka 1936, kufungua rasmi Pango Hifadhi la Kihistoria la Nyaraka za Siri za Vatican. Hizi ni Nyaraka zote za utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, hadi kifo chake tarehe 9 Oktoba 1958, huko Castel Gandolfo!

Baba Mtakatifu anasema, anachukua dhamana hii kwa moyo mtulivu kabisa, akiwa na imani na matumaini, ili kutoa nafasi kwa wasomi kufanya utafiti wa dhati kabisa, kwa mwanga wa haki ili kutambua mchango wake, changamoto alizokumbana nazo na maamuzi machungu aliyoyafanya kama binadamu katika hekima ya kikristo ili kuendeleza diplomasia, akiwa na hamu ya kuona mwanga mpya miongoni mwa watu! Kanisa linapenda na kuthamini mchango wa historia kama linavyompenda Mwenyezi Mungu! Kumbe, kwa imani na matumaini ya watangulizi wake, Baba Mtakatifu anatangaza kufunguliwa rasmi kwa nyaraka za Mtumishi wa Mungu Papa Pio XII kwa watafiti. Baba Mtakatifu anawashukuru wale wote waliojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kufanikisha mchakato huu, anawataka kuendelea kuwasindikiza watafiti wa kisayansi kwa kuwapatia rejea ambazo zitaonekana kuwa ni muhimu kama walivyofanya tangu sasa!

Papa Pio XII.2020

 

04 March 2019, 13:50