Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko tarehe 29 Machi 2019 ataongoza Ibada ya Upatanisho wa jumla na baadaye kitubio kwa mwamini mmoja mmoja. Baba Mtakatifu Francisko tarehe 29 Machi 2019 ataongoza Ibada ya Upatanisho wa jumla na baadaye kitubio kwa mwamini mmoja mmoja. 

Mpango Mkakati wa Saa 24 kwa ajili ya Bwana: Upatanisho, Kuabudu

“Mpango Mkakati wa Saa 24 kwa ajili ya Bwana” unaadhimishwa kati ya Ijumaa ya tarehe 29 Machi na Jumamosi ya tarehe 30 Machi 2019. Kauli mbiu “Wala mimi sikuhukumu”, enenda zako wala usitende dhambi tena” (Yoh. 8:11). Papa anataka walau kwa kila Jimbo kuwepo na Kanisa ambalo litaweza kuwa wazi kwa muda wa saa 24 ili kutoa nafasi kwa waamini kusali na kuabudu Ekaristi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., - Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kujizatiti kikamilifu katika hija ya Kipindi cha Kwaresima: kwa toba, kufunga, kusali, kusoma na kulitafakari Neno la Mungu pamoja na kulimwilisha Neno hili, katika matendo ya huruma:kiroho na kimwili. Mama Kanisa anaendelea kutoa kipaumbele cha pekee katika Sakramenti ya Upatanisho kama mahali muafaka pa kuonja huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka, tayari kusimama tena na kuendelea na safari ya: imani, matumaini na mapendo kwa Mungu na jirani!

Baba Mtakatifu Francisko kwa mara nyingine tena anapenda kuwakumbusha Mapadre waungamishaji kwamba, wao ni vyombo vya upatanisho, huruma na upendo wa Mungu na kamwe si wamiliki wa dhamiri za waamini. Wajenge utamaduni na sanaa ya kusikiliza kwa makini, ili wawasaidie waamini wao kufanya mang’amuzi ya kina, kuhusu maisha na wito wao ndani ya Kanisa na jamii katika ujumla wake! Tarehe 29 Machi 2019, majira ya saa 11:00 za Jioni kwa saa za Ulaya, Baba Mtakatifu anatarajiwa kuongoza Ibada ya Upatanisho wa pamoja na baadaye kufuatia maungamo ya mwamini mmoja mmoja kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Huu ni mwendelezo wa maadhimisho  ya Mpango Mkakati wa “Saa 24 kwa ajili ya Bwana” matunda ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya Huruma ya Mungu. “Saa 24 kwa ajili ya Bwana” unaadhimishwa Ijumaa na Jumamosi zinazotangulia Jumapili ya Nne ya Kipindi cha Kwaresima. Ni kipindi cha toba na wongofu wa ndani, tayari kumrudia Mwenyezi Mungu kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho. Hii ni Sakramenti inayomfanya mtu aguse kwa mkono wake ukubwa wa huruma ya Mungu, ili kupata amani na utulivu wa ndani!

Baba Mtakatifu anakazia tena “Mpango Mkakati wa Saa 24 kwa ajili ya Bwana” utakaoadhimishwa kati ya Ijumaa ya tarehe 29 Machi na Jumamosi ya tarehe 30 Machi 2019, kwa kuongozwa na kauli mbiu “Wala mimi sikuhukumu”, enenda zako wala usitende dhambi tena” (Yoh. 8:11). Baba Mtakatifu anataka walau kwa kila Jimbo kuwepo na Kanisa ambalo litaweza kuwa wazi kwa muda wa saa 24 ili kutoa nafasi kwa waamini kusali, kuabudu Ekaristi Takatifu na kujipatanisha na Mungu katika Sakramenti ya Kitubio! Anawaalika Mapadre kuwa mstari wa mbele kujipatanisha na Mungu katika maisha na utume wao!

Katika Kesha la Pasaka, Mama Kanisa atawasha Mshumaa wa Pasaka kwa moto mpya ambao pole pole utalifukuza giza na kuwaangaza waamini watakaokuwa kwenye maadhimisho ya Liturujia. Mwanga wa Kristo Mfufuka katika utukufu unaofukuzia mbali giza la moyo na roho, ili wote waweze kuishi katika mang’amuzi ya wanafunzi wa Emmau: kwa kusikiliza Neno la Mungu na kulishwa kwa Ekaristi Takatifu itakayoiwezesha mioyo yao kuweza kuwaka tena moto wa imani, matumaini na mapendo!

Toba : Saa 24 Kwa Bwana
27 March 2019, 10:28