Cerca

Vatican News
Papa Francisko: Kutabarukiwa kwa Kanisa la UNIFIL, nchini Lebanon, kusaidie mchakato wa kulinda amani na ujenzi wa umoja na udugu kati ya watu wa Mataifa! Papa Francisko: Kutabarukiwa kwa Kanisa la UNIFIL, nchini Lebanon, kusaidie mchakato wa kulinda amani na ujenzi wa umoja na udugu kati ya watu wa Mataifa!  (AFP or licensors)

Papa Francisko: Kutabarukiwa kwa Kanisa Lebanon: Amani na udugu!

Hivi karibuni, Askofu mkuu Santo Marcianò, wa Jimbo la Kijeshi nchini Italia ametabaruku Kanisa la Shama, huko nchini Lebanon na kuliweka chini ya ulinzi na tunza ya Mtakatifu Yohane XXIII na Mtakatifu Decor Carmel. Katika Ibada hii, Baba Mtakatifu Francisko amewashukuru wale wote waliojitoa na kujisadaka bila ya kujibakiza ili kukamilisha ujenzi wa Kanisa hili, mahali pa Ibada na Sala.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mama Kanisa anapotabaruku Kanisa, analitenga na kulifanya kuwa ni nyumba ya: Sala na Ibada, changamoto kwa waamini kusali kwa bidii, imani na uchaji wa Mungu, huku wakichuchumilia utakatifu wa maisha, mwaliko wa kwanza kabisa kwa waamini wote! Hiki ni kielelezo cha upendo na umoja wa Kanisa Katoliki. Ni mwaliko wa kujenga Kanisa hai, yaani Jumuiya ya Kikristo katika msingi ambao ni Kristo mwenyewe. Kanisa ni mahali ambapo waamini wanakusanyika kusikiliza Neno la Mungu na kushiriki Fumbo la Ekaristi Takatifu, ili waweze kuwa ni mashuhuda wa ukweli na upendo kati ya jirani zao kwa kudumisha umoja na udugu unaotengeneza sadaka safi inayompendeza Mungu.

Waamini wanahamasishwa kuyalinda na kuyatunza Makanisa yao, kwani huu ni urithi na utajiri mkubwa wa maisha ya kiroho na kihistoria. Hivi karibuni, Askofu mkuu Santo Marcianò, wa Jimbo la Kijeshi nchini Italia ametabaruku Kanisa la Shama, huko nchini Lebanon na kuliweka chini ya ulinzi na tunza ya Mtakatifu Yohane XXIII na Mtakatifu Decor Carmel. Katika Ibada hii, Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, amewashukuru wale wote waliojitoa na kujisadaka bila ya kujibakiza ili kukamilisha ujenzi wa Kanisa hili, mahali pa Ibada na Sala panapowawezesha waamini kukutana na Mwenyezi Mungu katika undani wa maisha yao.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, ni kwa njia ya ushuhuda wa maisha yenye mvuto na mashiko, wanaweza pia kuwa kweli ni mashuhuda wa amani na udugu. Baba Mtakatifu amewahakikishia uwepo wake wa karibu kwa njia ya sala na sadaka yake pamoja na kuwapatia baraka zake za kitume! Kwa upande wake, Askofu mkuu Santo Marcianò, anasema, hili ni Kanisa litakalotumiwa na wanajeshi Wakatoliki kwa ajili ya sala na ibada wanapotekeleza utume wao wa kulinda na kudumisha amani huko Lebanon, lakini pia litaweza kutumiwa na watu wote wenye mapenzi mema.

Hapa ni mahali pa kukuza na kudumisha umoja na udugu unaofumbatwa katika majadiliano ya kidini na kiekumene; kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Lebanon. Wanajeshi wa vikosi vya ulinzi na usalama kutoka sehemu mbali mbali za dunia, watapata nafasi ya kusali, ili kuendelea na utume wao wa kulinda: usalama, amani na maridhiano kati ya watu. Mtakatifu Yohane XXIII katika Waraka wake wa kitume, “Pacem in terris” yaani “Amani Duniani” ulioachapishwa kunako tarehe 11 Aprili 1963 anakazaia: ukweli, haki, upendo na uhuru wa watu wa Mungu. Huu ndio wajibu unaopaswa kutekelezwa na vikosi vya ulinzi na usalama huko Mashariki ya Kati.

Changamoto zinazoendelea kujitokeza katika ulimwengu mamboleo kiasi cha kutishia: haki, amani na maridhiano kati ya watu ni pamoja na: vitendo vya kigaidi, ukosefu wa haki msingi za binadamu; uhuru wa kuabudu, uhalifu pamoja na misimamo mikali ya kidini inayopandikiza hofu na utamaduni wa kifo! Mtakatifu Yohane XXIII, katika maisha na utume wake, aliwahi kuwa Padre wa maisha ya kiroho kwa wanajeshi pamoja na kuwa ni Balozi wa Vatican huko Mashariki ya Kati. Hii ni changamoto ya kujenga na kudumisha msingi ya haki, amani na upatanisho kati ya watu wa Mataifa!

Kutabaruku Kanisa Lebanon
20 March 2019, 14:53