Tafuta

Hospilitali mpya ya Watoto Bangui, Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati ni matunda ya Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya Huruma ya Mungu! Hospilitali mpya ya Watoto Bangui, Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati ni matunda ya Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya Huruma ya Mungu! 

Mchango wa Papa Francisko: Hospitali mpya Bangui!

Hospitali hii ambayo sasa imezunduliwa na Kardinali Konrad Krajewski, mtunza sadaka mkuu wa Papa kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko ni matunda ya Mwaka wa huruma ya Mungu! Baba Mtakatifu Francisko akiwa nchini Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati aliguswa sana na mateso na mahangaiko ya watoto wale, leo hii, wamejengewa hospitali mpya kabisa! Bangui kumenoga!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu ni tukio endelevu linalopaswa kutangazwa, kushuhudiwa na kuwazamisha watu katika huruma ya Mungu. Kanisa linahamasishwa kuwa ni shuhuda mwaminifu wa huruma ya Mungu, kiini cha ufunuo wa Kristo Yesu unaopata chimbuko lake kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Huruma ya Mungu iguse na kuwaonjesha waamini umuhimu wa kusamehe, kutegemezana, kusaidia na kudumisha upendo hasa kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii!

Ziara ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko Barani Afrika kunako mwaka 2016 na kwa namna ya pekee, nchini Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati inaendelea kuzaa matunda ya huduma makini, licha ya kwamba, ilikuwa ni nchi ya kwanza kuadhimisha Jubilei ya Mwaka Mtakatifu wa huruma ya Mungu. Baba Mtakatifu Francisko kwa kuguswa na mahangaiko ya watoto wadogo nchini Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati, aliamua kusaidia mchakato wa ujenzi wa Hospitali Mpya ya Watoto nchini humo.

Hospitali hii ambayo sasa imezunduliwa na Kardinali Konrad Krajewski, mtunza sadaka mkuu wa Papa kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko ni matunda ya Mwaka wa huruma ya Mungu. Katika ziara hii ya mshikamano wa upendo, Kardinali Konrad anaambatana na Dr. Mariella Enoc, Rais wa Hospitali ya Bambino Gesù inayomilikiwa na kuendeshwa na Vatican, Kamanda Domenico Giani, Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama mjini Vatican waliosaidia sana hupatikanaji wa fedha za ujenzi wa Hospitali hii.

Hospitali hii ina kitengo cha watoto wagonjwa wa utapiamlo, licha ya kupewa tiba na lishe bora, lakini pia wanawake wataanza kufundwa namna ya kuwahudumia watoto wao wanaokabiliwa na utapiamlo wa kutisha. Vatican pia imeanza kulipa mishahara kwa madaktari na wafanyakazi wa hospitali ya watoto wadogo sanjari na ukarabati mkubwa wa miundo mbinu ili kuweza kutoa huduma bora zaidi kwa watoto wagonjwa kama alivyokazia Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya kitume Barani Afrika.

Dalili za mafanikio zinaanza kuonekana kwa vifo vya watoto wadogo wenye umri chini ya miaka 5 kuanza kupungua kutokana na maboresho ya huduma kwa watoto hawa. Mwezi Septemba 2017, baadhi ya wafanyakazi walianza kupata mafunzo ya tiba kwa ajili ya watoto wadogo yanayotolewa na Hospitali ya Bambino Gesù ili kwamba, watakapohitimu masomo yao, waweze kurejea nchini Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati, ili kutoa huduma bora zaidi kwa watoto wagonjwa. Yote haya yanawezekana kutokana na moyo wa ukarimu na upendo unaoshuhudiwa na Baba Mtakatifu Francisko pamoja na wafadhili mbali mbali ndani na nje ya Vatican.

Papa: Bangui
01 March 2019, 13:58