Cerca

Vatican News
Kumbu kumbu ya Miaka 1150 tangu Mtakatifu Cyril alipofariki dunia! Kumbu kumbu ya Miaka 1150 tangu Mtakatifu Cyril alipofariki dunia!  (Vatican Media)

Jubilei ya Miaka 1150 tangu Mtakatifu Cyril alipofariki dunia

Kanisa linaadhimisha kumbu kumbu ya Miaka 1150 tangu alipofariki dunia Mtakatifu Cyril na kwamba, mchango wake bado ni endelevu katika mchakato mzima wa uinjilishaji na utamadunisho; unaoisaidia familia ya Mungu katika nchi hizi, kujikita katika kutafuta mafao ya wengi, ukweli na uzuri.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Watakatifu Cyril na Method, wasimamizi wa Bara la Ulaya, wanaheshimiwa sana na familia ya Mungu huko Czech na Slovakia, kutokana na mchango wao katika mchakato mzima wa uinjilishaji na utamadunisho, amana na utajiri mkubwa ulioachwa na ndugu hawa pacha katika maisha na utume wa Kanisa! Ni ndugu ambao wameacha urithi mkubwa wa tunu msingi za maadili, kiasi kwamba, Ukristo umekuwa ni chemchemi ya matumaini hasa wakati wa giza na mahangaiko ya watu! Walichangia kutafsiri Biblia ambayo ni msingi wa maisha ya kiroho na maendeleo ya kitamaduni; rejea ya sheria katika nchi mbali mbali.

Ukristo umeendelea kutangazwa na kushuhudiwa katika maisha na maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa na kwamba, uinjilishaji ni utume uliotekelezwa na Mtakatifu Cyril na ndugu yake Method kwa ari na moyo mkuu. Wakati huu, Kanisa linaadhimisha kumbu kumbu ya Miaka 1150 tangu alipofariki dunia Mtakatifu Cyril na kwamba, mchango wake bado ni endelevu katika mchakato mzima wa uinjilishaji na utamadunisho; unaoisaidia familia ya Mungu katika nchi hizi, kujikita katika kutafuta mafao ya wengi, ukweli na uzuri.

Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa, tarehe 22 Machi 2019 alipokutana na kuzungumza na wawakilishi wa Wabunge kutoka Czech na Slovakia kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 1150 tangu alipofariki dunia Mtakatifu Cyril. Huu ni mwaliko kwa wanasiasa hawa kutambua uhusiano wa ndani uliopo kati ya Injili na tamaduni zao,  kwa kuthamini mizizi ya Ukristo inayojenga jamii zao, ili kukuza ukarimu na mshikamano. Mtakatifu Cyril katika maisha na utume wake, alifanikiwa kuwa kweli ni kiungo thabiti kati ya tamaduni na Mapokeo mbali mbali ya Kikanisa.

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, amana na urithi huu wa maisha ya kiroho na kitamaduni, utasaidia mchakato wa ujenzi wa utamaduni wa watu wa nchi hizi mbili kukutana na hatimaye kuishi kwa pamoja hata katika tofauti zao msingi. Wawe na ujasiri wa kujenga madaraka yanayowakutanisha watu, kwa kubomolea mbali kuta za utengano, maamuzi mbele na hali ya kutoaminiana. Kwa njia hii, wataweza kuwa kweli ni mashuhuda wa mshikamano na wajenzi wa amani. Baba Mtakatifu anawataka wanasiasa katika utekelezaji wa dhamana na majukumu yao ya kila siku, kuwa kweli ni wadau wa ujenzi wa udugu, wasimamizi na wawajibikaji wa mafao ya wengi, ili kuwapatia watu waliowachagua matumaini katika maisha, wanapotekeleza majukumu yao ya uongozi wa ngazi ya juu katika jamii!

Mt. Cyril Miaka 1150
22 March 2019, 16:42