Papa Francisko anawataka waamini kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma na huduma ya upendo kwa watu wa Mungu! Papa Francisko anawataka waamini kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma na huduma ya upendo kwa watu wa Mungu! 

Hija ya Papa Francisko Morocco: Ibada ya Misa Takatifu

Baba mwenye huruma anataka kuwashirikisha watoto wake wote amana na utajiri wa maisha ya kiroho: huruma na upendo wake! Nimwelekeo unaovuka mipaka ya kimaadili, kijamii, kikabila au kidini na kwamba, ni hali inayowashirikisha wote huruma na upendo wa Mungu anayetaka kuwafanyia watoto wake sherehe, ili hatimaye, wawe ni wajenzi wa Ufalme wa Mungu hapa duniani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Injili ya Baba mwenye huruma aliyejitaabisha kumsubiri Mwana mpotevu alipomwona kwa mbali akirejea nyumbani, aliondoka mbio na kwenda kumlaki, ili kumshirikisha furaha iliyokuwa inabubujika kutoka katika sakafu ya moyo wake na kumwalika kushiriki katika karamu ya upendo! Lakini bahati mbaya, kaka mkubwa alikuwa na kinyongo moyoni mwake aliyetaka kumwona mdogo wake akiendelea kutokomea na hatimaye, kumezwa na malimwengu, kiasi hata cha kumfutilia mbali kutoka katika sakafu ya moyo wake!

Kijana mkubwa alishindwa kumtambua Baba yake pamoja na mdogo wake, akaamua kuendelea kuwa yatima dhidi ya udugu, kwa kukataa kushiriki katika karamu na kuendelea kuhifadhi chuki na hasira moyoni mwake. Hakutaka hata kumsamehe mdogo wake, kiasi hata cha kushindwa kutambua kwamba, alikuwa na Baba mwenye huruma aliyethubutu kusamehe na kusahau; kwa subira na upendo mkuu, ili kumshirikisha Mwana mpotevu huruma na upendo wake wa milele! Huu ni muhtasari wa mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili tarehe 31 Machi 2019 kwenye Uwanja wa Michezo wa Mfalme Moulay Abdellah, wakati wa hija yake ya kitume nchini Morocco.

Baba Mtakatifu anasema, simulizi hili ni kielelezo cha hali ya binadamu: Siku kuu kwa Mwana mpotevu na hasira kwa vile Mwana mpotevu amefanyiwa siku kuu! Huyu ni Mwana ambaye alionja machungu na adha ya maisha, kiasi cha kutamani kujishibisha kwa chakula cha nguruwe. Hii ndiyo misigano na mipasuko inayojionesha kati ya watu, jumuiya na hata miongoni mwa mtu binafsi. Baba Mtakatifu anasema kwamba, hizi ni kinzani ambazo zinapata chimbuko lake kutoka kwa Kaini na Abeli, changamoto na mwaliko kwa waamini kujenga na kudumisha umoja na udugu wa kibinadamu, kwa kutambua na kuheshimu, haki msingi, utu na heshima ya binadamu.

Ni utashi na mapenzi ya Baba wa mbinguni kwamba, watoto wake wote washiriki katika furaha ya maisha ya uzima wa milele! Kamwe kusiwepo na mtoto wake anayeishi katika ile hali ya Mwana mpotevu kama mtoto yatima au katika uchungu na hasira kama ilivyokuwa kwa kijana mkubwa, bali wote waokoke na kupata kujua yaliyo ya kweli! Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, kuna mambo mengi yanayoweza kuchochea kinzani, mipasuko na kishawishi cha kutaka kulipiza kisasi kwa kushika sheria mkononi, lakini uzoefu unaonesha kwamba yote haya yanapoteza matumaini na kuharibu yale mambo mazuri yanayopendwa na watu.

Hii ni changamoto ya kumtafakari Baba mwenye huruma, kwa kusali “Sala ya Baba Yetu” ili kumwona kila mtu kama ndugu na wala si kama adui anayepaswa kufyekelewa mbali na kutoweka katika uso wa dunia! Baba mwenye huruma anataka kuwashirikisha watoto wake wote amana na utajiri wa maisha ya kiroho yaani: huruma na upendo wake usiokuwa na kifani! Nimwelekeo unaovuka mipaka ya kimaadili, kijamii, kikabila au kidini, bali ni hali inayowashirikisha wote huruma na upendo wa Baba wa milele anayetaka kuwafanyia watoto wake siku kuu, ili hatimaye, waweze kuwa ni wajenzi wa Ufalme wa Mungu hapa duniani.

Mwishoni wa simulizi la Injili ya Baba mwenye huruma kuna mwaliko kwa Mwanaye mkubwa kuingia na kushiriki katika siku kuu ya Mwana mpotevu! Lakini Mwinjili Luka anawaachia waamini kila mmoja kwa nafasi yake kuandika hitimisho la sehemu hii ya Injili kwa njia ya maisha na mahusiano na jirani zake. Wakristo wanatambua kwamba, nyumbani kwa Baba kuna makao mengi, wataendelea kubaki nje, wale wasiopenda kushiriki furaha ya Baba mwenye huruma! Hii ni changamoto ya kutoa ushuhuda unaofumbatwa katika Injili ya huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu, ili kweli Jumuiya za Kikristo ziweze kuwa ni chemchemi za huruma ya Mungu, kwa kukuza na kudumisha utamaduni wa huruma, ili kukuza na kudumisha upendo, mshikamano na udugu wa kibinadamu.

Injili ya huruma ya Mungu inapaswa kumwilishwa katika huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii! Huruma na upole ni maneno yanayotumiwa hata na waamini wa dini ya Kiislam, yawaimarishe watu wote wa Mungu katika kudumisha Injili ya upendo!

Papa: Misa Morocco
31 March 2019, 17:08