Tafuta

Papa Francisko akutana na kuzungumza na Rais Faustin Archange Touadèra wa Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati! Papa Francisko akutana na kuzungumza na Rais Faustin Archange Touadèra wa Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati! 

Papa Francisko akutana na Rais Faustin Touadèra

Rais Faustin Archange Touadèra amempongeza na kumshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kufanikisha ujenzi wa Hospitali kwa ajili ya Watoto Wadogo mjini Bangui, iliyozinduliwa hivi karibuni. Huu ni mwendelezo wa maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka wa Huruma ya Mungu kwa watu wa Mungu, huko kwenye Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumanne jioni, tarehe 5 Machi 2019 amekutana na kuzungumza na Rais Faustin Archange Touadèra wa Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati pamoja na ujumbe wake. Baadaye, Rais Touadèra amepata nafasi ya kuzungumza na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican aliyekuwa ameambatana na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican.

Mazungumzo kati ya Baba Mtakatifu na mgeni wake, yamefanyika katika hali ya amani na utulivu mkubwa, kielelezo cha uhusiano mwema uliopo kati ya Serikali ya Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati pamoja na Vatican. Viongozi hawa wameridhishwa na Mkataba wa Makubaliano kati ya nchi hizi mbili. Wamepongeza mchango mkubwa unaotolewa na Kanisa Katoliki katika mchakato wa ujenzi na ustawi wa familia ya Mungu, Jamhuri ya Watu wa Afrika ya kati, hususan katika sekta ya elimu na afya.

Kwa namna ya pekee, Rais Faustin Archange Touadèra amempongeza na kumshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kufanikisha ujenzi wa Hospitali kwa ajili ya Watoto Wadogo mjini Bangui, iliyozinduliwa hivi karibuni. Huu ni mwendelezo wa maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka wa Huruma ya Mungu kwa watu wa Mungu, huko kwenye Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati. Wamejadiliana kuhusu hali halisi ilivyo nchini humo, mkataba wa amani kati ya viongozi mbali mbali wa kisiasa kama njia ya kumaliza kabisa vita ya wenyewe kwa wenyewe ambayo imekuwa ni kikwazo kikubwa cha maendeleo fungamani nchini humo!

Baba Mtakatifu pamoja na mgeni wake, wamekazia umuhimu wa kujenga na kudumisha mchakato wa haki, amani, utulivu na maridhiano kati ya watu pamoja na kuhakikisha kwamba, vita inakomeshwa, ili wakimbizi na wahamiaji waweze kupata nafasi ya kurejea tena nchini mwao na katika makazi yao, tayari kufungua ukurasa mpya wa maisha na maendeleo yao!

Papa: Afrika ya Kati
06 March 2019, 14:53