Tafuta

Vatican News
Papa Francisko anakazia kuhusu malezi bora kwa watoto pamoja na ushuhuda makini kwa Kristo na Kanisa lake! Papa Francisko anakazia kuhusu malezi bora kwa watoto pamoja na ushuhuda makini kwa Kristo na Kanisa lake!  (Vatican Media)

Papa Francisko: Imarisheni malezi na ushuhuda wenu kwa Kristo!

Watoto wanapokuwa wanazungukwa na wazazi wao, yaani: baba na mama wanajisikia kuwa salama zaidi. Wazazi wasiwamiliki sana watoto wao kiasi hata cha kuharibu malezi na makuzi yao! Wawaachie uhuru kidogo wa kuamua na kutenda. Wazazi waendelee kuwakumbuka na kuwaombea watoto wao, kwa kuwaaminisha chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili jioni tarehe 3 Machi 2019 akiwa kwenye Parokia ya Mtakatifu Crispin wa Viterbo alipata nafasi ya kukutana na familia, watoto na vijana kutoka Parokiani hapo. Hawa ni wazazi wanaofanya katekesi kama sehemu ya maandalizi ya ubatizo wa watoto wao wachanga. Baba Mtakatifu amewakumbusha wazazi na walezi wa watoto hawa kwamba, Sakramenti ya Ubatizo ni msingi wa maisha yote ya Kikristo, lango la kuingilia uzima katika roho na hivyo kumwezesha mwamini kupata Sakramenti nyingine za Kanisa.

Kwa njia ya Ubatizo, watoto wanafanywa huru toka katika utumwa wa dhambi na kuzaliwa upya kwa maji na Roho Mtakatifu, hivyo wanakuwa kweli ni watoto wa Mungu, na viungo vya Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa. Ubatizo ni Sakramenti ya kuzaliwa upya kwa maji na katika Neno! Kumbe, wazazi wanapaswa kutekeleza vyema wajibu wao wa malezi na makuzi katika hatua za mwanzo kabisa za maisha yao hapa duniani. Watoto wanapokuwa wanazungukwa na wazazi wao, yaani: baba na mama wanajisikia kuwa salama zaidi. Wazazi wasiwamiliki sana watoto wao kiasi hata cha kuharibu malezi na makuzi yao! Wawaachie uhuru kidogo wa kuamua na kutenda. Wazazi waendelee kuwakumbuka na kuwaombea watoto wao, kwa kuwaaminisha chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria. Watoto wanapokuwa watu wazima, wakumbuke pia kuwaombea na kuwatunza wazazi wao.

Baba Mtakatifu pia amepata nafasi ya kukutana na kuzungumza na watoto pamoja na vijana wa Parokia ya Mtakatifu Crispin wa Viterbo. Hawa ni wale watoto na vijana ambao wameimarishwa kwa Sakramenti ya Kipaimara, sasa wako tayari kulinda, kutetea na kushuhudia imani yao kwa Kristo na Kanisa lake! Kundi la pili ni watoto ambao wamepokea Sakramenti ya Ekaristi Takatifu sasa wako tayari kujimega na kujisadaka kwa ajili ya watoto wenzao wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi.

Makundi haya ya watoto na vijana, yamemshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa upendo na unyoofu katika maisha na utume wake, hasa kwa kutoa kipaumbele kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Kwa wengi wao, hii ni siku ambayo kamwe hawataisahau katika maisha! Vijana walioimarishwa kwa Sakramenti ya Kipaimara, wanawashukuru viongozi wao wa Parokia kwa kuwapatia tena nafasi ya kuendelea na katekesi, ili kuwaimarisha katika imani, matumaini na mapendo!

Baba Mtakatifu amewapongeza vijana kwa kumshirikisha uzoefu na mang’amuzi katika maisha yao! Amewataka kuongozwa na dhamiri nyofu na wasikubali kumezwa na malimwengu kwani hii ni kazi ya Shetani ambaye kimsingi yupo na wala si jambo la kufikirika tu! Shetani ndiye anayewajengea tamaa mbaya na mawazo machafu, kiasi hata cha kutumbukia katika vita! Shetani kamwe hapendi amani na utulivu. Shetani ni adui wa kwanza ambaye wanapaswa kumwogopa katika maisha. Wajenge utamaduni wa kusali, kwa kujiaminisha chini ya ulinzi na tunza ya Kristo Yesu kwani anayo nguvu na mamlaka dhidi ya Shetani ambaye ni mjanja kupita kiasi!

Shetani ni mwongo na daima anataka kupindisha Amri za Mungu, ili kuwaangusha waamini dhambini. Baba Mtakatifu anawataka watoto na vijana kujiaminisha pia kwa Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa. Watoto hawa wajenge uhusiano mwema na: Mapadre, Makatekista pamoja na familia zao. Kila mtu anaweza kutekeleza na kuanguka katika dhambi na ubaya wa moyo! Vijana waongozwe na dhamiri nyoofu katika kufanya maamuzi yao. Waamini wawe makini katika safari ya maisha yao ya kiroho kwa kushiriki katika maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa; kwa Kusoma na kutafakari Neno la Mungu pamoja na kuendelea kuishi maisha ya Kikristo, ili hatimaye, waweze kuwa ni mashuhuda wa furaha ya Injili kwa kukutana na Kristo Yesu katika safari ya maisha yao! Shetani ana uwezo wa kuwapatia furaha ya mpito, lakini matokeo yake nai majonzi makubwa! Roho Mtakatifu anawakirimia waamini Mapaji yake Saba, chemchemi ya furaha ya Injili!

Papa: Mt. Crispin: Sakramenti
04 March 2019, 10:20