Papa Francisko anawataka vijana kujenga na kukuza dhamiri nyofu, majadiliano, umoja na mshikamano, daima wakipania ustawi, maendeleo na mafao ya jirani zao. Papa Francisko anawataka vijana kujenga na kukuza dhamiri nyofu, majadiliano, umoja na mshikamano, daima wakipania ustawi, maendeleo na mafao ya jirani zao. 

Vijana fuateni dhamiri nyofu, kuzeni majadiliano & kujisadaka!

Baba Mtakatifu Francisko anawashauri vijana kuhakikisha kwamba, wanajenga na kukuza dhamiri nyofu; wanajikita katika majadiliano yanayofumbatwa katika ukweli na uwazi, ili kuweza kufanya maamuzi mazito katika maisha yao! Wajenge na kudumisha moyo wa sala na tafakari inayomwilishwa katika ustawi, maendeleo na mafao ya jirani zao! Fedha iwe ni matokeo na wala si lengo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, tarehe 23 Machi 2019 amekutana na kuzungumza na wanafunzi 1, 150, kutoka katika Chuo cha Barbarigo, Padua, Kaskazini mwa Italia. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kujibu maswali manne kutoka kwa wanafunzi hawa, yaliyogusia kuhusu maisha yao ya ndani: Je, wamwendee nani wakati wa mahangaiko yao ya ndani, ili kupata majibu muafaka. Licha ya wanafunzi hawa kukita maisha yao kutafuta ukweli, haki na uzuri hata wakati mwingine kwa kumwilisha Injili ya upendo katika maisha yao, lakini bado wanakabiliwa na maswali tete kuhusu maisha, kiasi hata cha kushindwa kujiaminisha kwa Kristo Yesu, Bwana na Mwalimu, Mungu kati ya watu wake!

Je, hata Baba Mtakatifu katika maisha yake ya ujana, alipatwa na maswali mazito katika safari yake ya imani? Baada ya malezi na majiundo makini, sasa wanafunzi hawa wanahisi kwamba, wanaweza kujisadaka kwa ajili ya jirani zao, lakini bado wanakabiliwa na changamoto ya kufanya maamuzi magumu katika maisha yao kwa leo na kesho iliyo bora zaidi, sanjari na kutambua ndoto ya Mwenyezi Mungu katika maisha yao! Baba Mtakatifu anawataka vijana kwanza kabisa kuongozwa jna dhamiri nyofu; kuthubutu katika kufanya maamuzi mazito katika maisha; kujenga na kudumisha umoja, upendo na mshikamano hasa na maskini pamoja na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Watambue kwamba, Mama Kanisa anawategemea sana vijana katika ushuhuda na majitoleo yao ya kila siku. Kumbe, waalimu, walezi wao mapadre wanaweza kuwasaidia kutekeleza vyema dhamana na wajibu wao katika maisha! Jambo la msingi ni kukuza na kudumisha majadiliano katika ukweli na uwazi.

Wazazi wanayo dhamana nyeti katika malezi na maamuzi yao kwa leo na kesho iliyo bora zaidi, hususan masuala ya imani. Familia ni neema na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayoimarishwa na kudumishwa kwa njia ya Sakramenti ya Ndoa Takatifu. Wazazi na walezi wanapewa dhamana na wajibu wa kuwapatia watoto wao elimu na malezi bora, ili hatimaye, watoto hawa waweze kufanya maamuzi mazito katika maisha yao! Vijana wajifunze kushirikishana mawazo na wengine, ili kufikia uamuzi wenye ukomavu katika maisha!

Baba Mtakatifu anawahamasisha vijana kujizatiti katika masomo, ili kung’amua maana halisi ya maisha na changamoto zake; wajikite katika kutafuta ukweli na kuudumisha, daima wakichuchumilia: haki, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Shule iwe ni mahali pa wanafunzi kupata majibu muaafaka yanayosadifu kiu na hamu yao ya ndani, ili kuunganisha nadharia, vitendo na uzoefu wa maisha, daima wakijitahidi kusoma alama za nyakati! Baba Mtakatifu anasema, hata yeye katika maisha, aliambiwa na wazazi wake kufanya kazi ili kujipatia mahitaji msingi na kwa hakika alifanya. Mang’amuzi haya yamemwezesha kuwa mchapakazi na kwamba, kazi ni kipimo cha ut una heshima ya binadamu!

Vijana wajenge utamaduni wa kusoma Maandiko Matakatifu sanjari na kutafuta kweli za maisha ya Kikristo katika maisha yao, zawadi kubwa itakayozaa matunda kwa wakati wake, kwa vijana wenye akili na nyoyo wazi kwa ajili ya utajiri huu unaobubujika kutoka katika Maandiko Matakatifu. Vijana watambue kwamba, mbele yao kuna changamoto zinazopaswa kufanyiwa kazi, kwa kuwa na mwono sahihi wa binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Watambue kwamba, kuna changamoto ya ukosefu wa fursa za ajira, kuchechemea kwa uchumi kitaifa na kimataifa; kutoweka kwa dhana ya maisha ya kweli. Matokeo yake ni kukua na kushamiri kwa uchoyo na ubinafsi; upweke hasi unaowatumbukiza vijana katika mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo, chuki na uhasama. Kuna utandawazi unaojikita katika ubinafsi na uchoyo, hatari sana katika maisha!

Vijana wajitahidi kujenga na kudumisha: haki, udugu, ukarimu na amani, ili kweli dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Vijana waendelee kujikita katika sala na tafakari ya Neno la Mungu, ili kweli waweze kuwa ni manabii na mashuhuda wa matumaini katika ulimwengu mamboleo. Vijana wawe tayari kuwa ni wajenzi wa leo na kesho iliyo bora zaidi, kwa kukazia utu na heshima ya binadamu; umoja na udugu, amani na ukweli katika maisha, tunu na utambulisho wa kijana makini! Kipaumbele cha kwanza katika kuchagua kazi kiwe ni huduma makini kwa jirani na wala si kupata mshahara mkubwa! Kila uamuzi anaoufanya kijana, anapaswa kuhakikisha kwamba, anautekeleza kwa ari na moyo mkuu! Ili kuweza kufanya maamuzi magumu na mazito katika maisha, vijana wajifunze kutafuta upweke chanya na faragha, ili kusali na kutafakari kwa kina, wakitambua kwamba, mbele yao kuna mapambano mazito ya maisha!

Papa Francisko: Wanafunzi wa Padua
23 March 2019, 17:10