Tafuta

Vatican News
Papa Francisko anawataka wafanyakazi wa Mahakama ya Ukaguzi wa Mahesabu ya Umma: Kuzingatia: Utaalam, ujuzi, maarifa na dhamiri nyofu katika misingi ya ukweli na uwazi! Papa Francisko anawataka wafanyakazi wa Mahakama ya Ukaguzi wa Mahesabu ya Umma: Kuzingatia: Utaalam, ujuzi, maarifa na dhamiri nyofu katika misingi ya ukweli na uwazi!  (Vatican Media)

Papa: Ukaguzi wa mahesabu ya umma ni muhimu sana!

Baba Mtakatifu anasema, ukaguzi makini wa mapato na matumizi ya Serikali unasaidia kudhibiti kishawishi cha ufisadi wa mali ya umma pamoja na kutumia fedha ya umma kujijenga kisiasa. Siasa safi inahitajika, ili kurekebisha na kuratibu taasisi; kujenga na kudumisha utendaji ulio bora kwa kuondoa mashinikizo na urasimu usiotakiwa, ili kudumisha msingi wa jamii iliyo bora na adilifu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mahakama ya Ukaguzi wa Mahesabu ya Umma ni taasisi ya Serikali ya Italia inayoratibu na kudumisha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; kwa kujikita katika haki kwa ajili ya mafao ya jamii. Lengo ni kuendeleza mchakato wa maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu, utu na heshima ya binadamu, vikipewa msukumo wa pekee. Ni katika muktadha huu, Serikali inapaswa kusimama kidete kulinda haki asilia za binadamu kama sehemu muhimu inayoipambanua serikali inayojikita katika haki. Mafao ya binadamu hayana budi kusaidia mafungamano ya kijamii na kama kanuni inayounganisha programu mbali mbali kwa ajili ya taifa!

Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko alipokutana na kuzungumza na Wafanyakazi wa Mahakama ya Ukaguzi wa Mahesabu ya Umma, Jumatatu, tarehe 18 Machi 2019. Baba Mtakatifu amewataka kukuza na kudumisha hekima inayofumbatwa katika utaalam wa hali ya juu, ujuzi na maarifa ya mahesabu, mambo yanayoongozwa na dhamiri nyofu iliyofundwa ikafundika, ili kuzingatia haki na ukarimu kwa taasisi na jumuiya katika ujumla wake. Dhamiri nyofu na kanuni maadili ni mambo msingi katika kutekeleza wajibu huu nyeti katika jamii.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, ukaguzi makini wa mapato na matumizi ya Serikali unasaidia kudhibiti kishawishi cha ufisadi wa mali ya umma pamoja na kutumia fedha ya umma kujijenga kisiasa. Siasa safi inahitajika, ili kurekebisha na kuratibu taasisi; kujenga na kudumisha utendaji ulio bora zaidi, kwa kuondoa mashinikizo na urasimu usiotakiwa, ili kudumisha msingi wa jamii iliyo bora na adilifu. Mahakimu wanapaswa kusimama kidete kupambana na rushwa inayoendelea kusigina mafungamano ya kijamii, kwa kuwatumbukiza watu katika umaskini, kiasi cha kuwaondolea matumaini na imani kwa serikali yao.

Rushwa ina dhalilisha utu, heshima na haki msingi za binadamu, changamoto na mwaliko kwa jamii, kusimama kidete kupambana na saratani ya rushwa katika mifumo yake mbali mbali hadi kieleweke. Mahakama ya Ukaguzi wa Mahesabu ya Umma kiwe ni chombo cha kukuza na kudumisha utawala wa sheria ili kuondokana na matumizi mabaya ya madaraka, sanjari na kuonesha mbinu mkakati wa kupambana na ukosefu wa ufanisi pamoja na uharibifu unaoweza kujitokeza. Ukweli, uwazi na uwajibikaji ni mambo msingi katika kukuza na kudumisha demokrasia sanjari na kulinda fedha ya umma ambayo inapaswa kuwahudumia maskini. Kumbe, kuna haja ya kuwa makini ili kung’amua vitendo vinavyoweza kusababisha hujuma kwa Serikali!

Baba Mtakatifu anawataka wafanyakazi wa Mahakama ya Ukaguzi wa Mahesabu ya Umma kutekeleza dhamana na wajibu wao kwa amani na utulivu; kwa umakini mkubwa mambo msingi katika kazi yao, kwa kutambua kwamba, huduma hii ni makini katika kukuza jamii na utawala wa sheria. Anawataka katika kipindi hiki cha Kwaresima kuwa mashuhuda wa haki na ukweli; kwa kuendelea kujikita katika kusoma na kulitafakari Neno la Mungu, ili liwasaidie kujisadaka kikamilifu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kwaresima ni kipindi cha kupambana na ubinafsi na uchoyo; kwa kutafuta vyanzo vya matatizo na kupataia ufumbuzi wa kudumu, katika hali ya unyenyekevu na ukimya. Mwishoni, mwa hotuba yake, Baba Mtakatifu amewaweka wafanyakazi hawa chini ya ulinzi na tunza ya Mtakatifu Yosefu, mtu mwenye haki, ambaye Kanisa linafanya kumbu kumbu yake, tarehe 19 Machi, kila Mwaka!

Mahakama ya Ukaguzi

 

 

18 March 2019, 14:45