Papa Francisko asema, Siasa ni wito kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi! Papa Francisko asema, Siasa ni wito kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi! 

Papa Francisko: Siasa ni wito wa huduma kwa mafao ya wengi!

Siasa ni wito na si kila mwamini ana wito wa kuwa ni mwana siasa! Ikumbukwe kwamba, siasa si njia pekee inayoweza kuwahakikishia watu haki, kumbe, medani mbali mbali za maisha, ziwe ni mahali ambapo patawasaidia waamini kuyatakatifuza malimwengu, kwa kujikita katika mchakato wa kutafuta na kudumisha haki, ustawi, mafao na maendeleo ya wengi. Jengeni Ufalme wa Mungu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kuna haja ya kuwekeza katika majiundo makini kwa vijana wa kizazi kipya ili kuwa na wakatoliki watakaosimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha: ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, mintarafu Mafundisho Jamii ya Kanisa. Lengo ni kuhakikisha kwamba, waamini walei wanatambua kwamba, wao ni mitume wamisionari, wanaotumwa ulimwenguni ili waweze kuwa kweli ni nuru ya ulimwengu na chumvi ya dunia.

Wanasiasa wanahimizwa kujenga na kudumisha umoja na urafiki na Kristo Yesu pamoja na kutambua nguvu na udhaifu wao kama binadamu. Mchakato wa kuingia katika masuala ya kisiasa unapania pamoja na mambo mengine kujenga urafiki wa kijamii, ili kuleta mageuzi yanayokusudiwa kwa kujikita katika tunu msingi za maisha ya Kiinjili. Mtakatifu Oscar Arnulfo Romero katika maisha na utume wake, alipenda kuwahimiza waamini walei kuhakikisha kwamba, wanakuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya uinjilishaji katika mazingira yao, kama kielelezo cha imani tendaji. Siasa ni wito na si kila mwamini ana wito wa kuwa ni mwana siasa!

Ikumbukwe kwamba, siasa si njia pekee inayoweza kuwahakikishia watu haki, kumbe, medani mbali mbali za maisha, ziwe ni mahali ambapo patawasaidia waamini kuweza kuyatakatifuza malimwengu, kwa kujikita katika mchakato wa kutafuta na kudumisha haki, ustawi, mafao na maendeleo ya wengi. Waamini wanahimizwa kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu hapa duniani! Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu, tarehe 4 Machi 2019, kwa Kikundi cha Viongozi Vijana kutoka Amerika ya Kusini! Baba Mtakatifu anasema, inalipa kwa vijana kujisadaka katika masuala ya kisiasa, huku wakiwa wamebeba amana na utajiri unaobubujika kutoka katika Injili ya Kristo na kwamba, siasa si sanaa inayomwezesha mtu kuratibu mamlaka, rasilimali na changamoto za maisha. Siasa ni wito wa huduma miongoni mwa waamini walei ili kudumisha urafiki wa kijamii, ustawi na maendeleo ya wengi.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, ni kwa njia hii, siasa inawawezesha watu kuwa ni wadau katika mchakato wa maendeleo yao wenyewe, bila kuwahusisha watu, hapo hakuna siasa ya kweli! Siasa inafumbata mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi ili kukabiliana na changamoto zinazoendelea kuibuka katika ulimwengu mamboleo! Fumbo la Umwilisho lililomwezesha Mungu kuwa karibu zaidi na watu wake, liwe ni kigezo kwa wanasiasa kuwa karibu na wananchi wao. Amerika ya Kusini, haina budi kuwekeza zaidi kwa wanawake, vijana na maskini, ili kuwajengea nguvu ya kiuchumi. Wanawake ni nguzo muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa na jamii katika ujumla wake na kwamba, sura ya Amerika ya Kusini inajionesha kwa namna ya pekee, miongoni mwa wanawake!

Vijana ni chachu ya mabadiliko na mageuzi ya kijamii na kwamba, maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; wanapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza katika sera na mikakati ya ustawi na maendeleo ya kijamii. Kumbe, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi ni mambo msingi kwa wanasiasa wakatoliki sehemu mbali mbali za dunia! Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, ulimwengu mamboleo unawahitaji wanasiasa wenye uwezo na uelewa mpana zaidi; watu wanaoweza kupembua kwa kina na mapana; kwa kuonesha dira na njia ya kufuata ili kufikia malengo yanayokusudiwa. Wanasiasa makini wanapaswa kuwa ni chachu ya kuganga na kuponya mapungufu makubwa yanayojitokeza katika medani za kisiasa, ili kujenga umoja na mshikamano wa kidugu; uhuru wa kweli unaofumbatwa katika misingi ya imani inayofafanuliwa katika Mafundisho Jamii ya Kanisa!

Hakuna sababu ya kuwa na Chama cha Kisiasa cha Kikatoliki, bali kuwa na wanasiasa wakatoliki, wenye kuongozwa na Mafundisho Jamii ya Kanisa, wakiwa wameshikamana na viongozi wao wa Kanisa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu! Baba Mtakatifu anasema, kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 400, yaani hapo mwaka 2030 tangu sanamu ya Bikira Maria wa Aparecida ilipookotwa mtoni kunako mwaka 1717, kuna haja kwa wanasiasa kujikita zaidi na zaidi katika Mafundisho Jamii ya Kanisa. Lengo ni kuwawezesha waamini walei kuadhimisha matukio haya huku wakiwa na uelewa mpana zaidi kwamba, wao ni mitume wamisionari, wanaopaswa kusimama kidete kupambana na ukoloni wa kiitikadi na kiuchumi, ili kulinda utu na heshima ya binadamu!

Papa: Amerika ya Kusini
05 March 2019, 09:35