Cerca

Vatican News
Papa Francisko anawataka wanafunzi wa Taasisi ya Kipapa ya "Scholas Occurrentes" kuwa ni wajenzi wa amani na majadiliano! Papa Francisko anawataka wanafunzi wa Taasisi ya Kipapa ya "Scholas Occurrentes" kuwa ni wajenzi wa amani na majadiliano! 

Papa: "Scholas Occurrentes": Dumisheni amani na majadialiano!

Baba Mtakatifu amewataka vijana hawa kujisadaka bila ya kujibakiza ili kutengeneza mtandao utakaowawezesha kushirikishana: ujuzi, elimu, maarifa, weledi pamoja na kipaji cha ugunduzi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Vijana wawe ni mashuhuda na vyombo vya haki, amani, udugu na majadiliano, tayari kupandikiza mbegu hizi, ili ziweze kukua na kukomaa, kwa wakati!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Taasisi ya Kipapa ya "Scholas Occurrentes" iliyoanzishwa rasmi na Baba Mtakatifu Francisko kunako mwaka 2013 baada ya uzoefu na mang'amuzi yake huko nchini Argentina, kwa sasa inapania kuendelea kuwa ni mahali pa utambulisho wa vijana katika mchakato wa kutangaza na kushuhudia: Injili ya maisha, kukuza elimu na kudumisha malezi bora kwa kujenga utamaduni wa watu tofauti kukutana na kusherekea zawadi ya uhai, kila mtu akiwa na utambulisho wake makini unaojionesha wazi, kwani maisha ni jambo zito.

Hii ni taasisi inayopania kukuza na kudumisha amani na majadiliano katika ukweli na uwazi, kwa kutambua kwamba, vijana wanapaswa kutekeleza kwa dhati leo ya Mungu katika uhalisia wa maisha yao. Ni changamoto inayofumbatwa katika kipaji cha ubunifu, nguvu na utashi wa ndani wa kupambana na hali pamoja na mazingira, bila kukata wala kukatishwa tamaa! Utamaduni na sanaaa ya watu kukutana pamoja na kuwasikiliza vijana ni amana na urithi mkubwa wa Kanisa kutoka kwa Mababa wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana iliyohitimishwa hivi karibuni.

Utamaduni wa watu kukutana hauna budi kuwa makini kwani unapaswa kupata chimbuko lake kutoka katika undani wa moyo wa mtu na hivyo kuwa ni chemchemi ya furaha ya kweli! Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi, tarehe 21 Machi 2019 ametembelea Makao ya Taasisi ya Kipapa ya "Scholas Occurrentes" yaliyoko mjini Roma, ili kuzindua mradi wa kimataifa kuhusu amani. Lengo la mradi huu ni kuwajengea vijana uwezo wa kujifunza kanuni, sheria, taratibu na maadili yatakayowawezesha vijana hawa katika kipindi cha mwaka mmoja kuwa mashuhuda na vyombo vya amani duniani.

Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuhojiana na vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia, waliokuwa wameunganishwa kwa njia ya luninga na baadaye, akakutana na kuzungumza na vijana ambao wameshiriki katika programu za: sanaa, michezo na shughuli za kiufundi. Taasisi ya Kipapa ya "Scholas Occurrentes" ina shule 450 katika nchi 190. Hizi ni shule za Serikali na binafsi zinazomilikiwa na kuendeshwa na dini mbali mbali duniani! Ndoto kubwa ya Baba Mtakatifu ni kujenga umoja na mshikamano miongoni mwa vijana wa vijana, hasa maskini zaidi duniani, kwa kuwajengea uwezo wa kusimama kidete kujenga, kulinda na kutetea amani, ustawi na mafao ya wengi!

Baba Mtakatifu amewataka vijana hawa kujisadaka bila ya kujibakiza ili kutengeneza mtandao utakaowawezesha kushirikishana: ujuzi, elimu, maarifa, weledi pamoja na kipaji cha ugunduzi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Vijana wawe ni mashuhuda na vyombo vya haki, amani, udugu na majadiliano, tayari kupandikiza mbegu hizi, ili ziweze kukua na kukomaa, kwa njia ya uongozi makini miongoni mwa vijana wa kizazi kipya! Vijana wanakumbushwa kwamba wao ni leo ya Mungu, wanayopaswa kuimwilisha katika uhalisia wa maisha yao; kwa kushirikiana na wengine ili kujenga leo na kesho iliyo bora zaidi.

Baba Mtakatifu Francisko anawataka wazazi na walezi kukuza na kujenga utamaduni wa majadiliano katika ukweli na uwazi pamoja na watoto wao, ili kurithisha imani, mchakato unaoanza ndani ya familia, katika hali ya urafiki na ujirani mwema, kiasi kwamba, katekesi inakuwa ni sehemu ya ushuhuda wa uhalisia wa maisha. Katika shida, mahangaiko na madhulumu ya Kanisa, wazazi na walezi ndio waliojitwika dhamana ya kuwarithisha watoto wao imani na tunu msingi za maisha ya Kikristo.

Wazazi na walezi wahakikishe kwamba, wanatekeleza vyema dhamana na wajibu wao wa malezi na makuzi! Vijana wanawajibika katika maamuzi yao, kumbe, wanapaswa kutenda kwa kuzingatia dhamiri nyofu. Hakuna sababu ya wongofu wa shuruti, imani inarithishwa kwa njia ya ushuhuda unaomwilishwa katika matendo, kielelezo makini cha imani tendaji. Mbegu ya imani, maadili na utu wema, iliyopandwa katika uhalisia wa maisha, iko siku, itazaa matunda ya toba na wongofu wa ndani. Baba Mtakatifu anasema, wazee wa ndoto lakini vijana wana unabii; wote wanapaswa kusaidiana ili kukamilishana!

Scholas Occurrentes 2019
22 March 2019, 16:27