Cerca

Vatican News
Papa Francisko akutana na kuzungumza na Shirikisho la Madaktari wa Watoto Italia: Huduma ya afya iwe shirikishi, maskini wapewe kipaumbele cha kwanza! Papa Francisko akutana na kuzungumza na Shirikisho la Madaktari wa Watoto Italia: Huduma ya afya iwe shirikishi, maskini wapewe kipaumbele cha kwanza!  (ANSA)

Papa akutana na Shirikisho la Madaktari wa Watoto Italia

Baba Mtakatifu Francisko analitaka Shirikisho la Madaktari wa Watoto Italia kuendelea kujipambanua kwa kujenga na kudumisha utamaduni wa afya ya mshikamano na jumuishi; kwa kuzuia na kutibu magonjwa, daima maskini na wale wote wanaosukumiziwa pembezoni mwa jamii, wakipewa kipaumbele cha kwanza.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Shirikisho la Madaktari wa Watoto Italia, katika kipindi cha miaka 40 ya uwepo na utume wake, limeweza kutoa tiba na kinga kwa watoto kutoka katika familia 5, 500. Hii ni huduma ambayo inafumbatwa katika taaluma, weledi, nidhamu na maadili, kwa kuzingatia mambo msingi ya huduma na kinga mintarafu, sheria za nchi na uwezo wa familia. Ni wito unaopaswa kutekelezwa katika hali ya utulivu na majitoleo ya kitaalamu, kwa kukazia mambo msingi katika maisha ya watoto wagonjwa.

Shirikisho hili limekuwa ni chimbuko la Sera ya Huduma ya Afya Kitaifa nchini Italia ambayo imechangia kwa kiasi kikubwa katika maboresho ya afya ya wananchi kutokana na huduma bora zinazotolewa. Shirikisho limekuwa pia ni jukwaa la majadiliano ya sera za kisiasa na kijamii, kwa kudhibiti mambo msingi yanayopaswa kuzingatiwa katika kulinda na kudumisha afya ya watoto na vijana nchini Italia.  Ni Shirikisho ambalo linahudumia umri ambao uko kwenye mchakato wa ukuaji, changamoto inayohitaji uelewa mpana kuhusu mwili wa mwanadamu na magonjwa yake!

Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko Alhamisi, tarehe 21 Machi 2019, wakati alipokutana na kuzungumza na wajumbe wa Shirikisho la Madaktari wa Watoto Italia. Katika hotuba yake, Baba Mtakatifu amekazia umuhimu wa madaktari kuwa na mafunzo endelevu kazini; tafiti makini, mijadala, makongamano na warsha mbali mbali ili kujenga na kudumisha utamaduni wa kulinda afya ya binadamu na kwa namna ya pekee kabisa, watoto wadogo! Katika ulimwengu mamboleo unaojikita katika maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia sanjari na masuala ya kijamii, waathirika wakuu ni watoto wadogo. Katika muktadha huu, Shirikisho hili linapaswa kujipambanua kwa kujenga na kudumisha utamaduni wa afya ya mshikamano na jumuishi; kwa kuzuia na kutibu magonjwa, daima maskini na wale wote wanaosukumiziwa pembezoni mwa jamii, wakipewa kipaumbele cha kwanza.

Ujuzi, weledi na maarifa yao, yawe ni msaada mkubwa katika kukuza utamaduni wa kuwasikiliza wagonjwa, ili kufahamu shida na magumu yanayowasumbua na hatimaye, kujenga imani na matumaini kwa wagonjwa wanaowahudumia! Baba Mtakatifu anawataka Madaktari pia kuboresha maisha yao ya kiroho, kwa kumpatia Kristo Yesu, kipaumbele cha kwanza kama mfano bora wa kuigwa, kwa sadaka, upendo na ukaribu kwa wagonjwa, ili hata wao, wanapokutana na wagonjwa, waweze kuwapatia tiba muafaka. Madaktari wajenge uhusiano mwema na familia za watoto wagonjwa. Wao wanahitaji huduma ya utaalam, weledi na uhakika wa usalama kutoka kwa madaktari, kwa kuwadhaminisha watoto wao wapendwa!

Madaktari wadumishe pia uhusiano mwema na watoto wadogo, watende kwa upole na ukarimu; wawaonjeshe huruma, upendo na ucheshi, ili kuwapatia watoto hawa ujasiri na hatimaye, kujiweka wazi mbele yao, ili hata dawa wanazotoa ziweze kuwa ni msaada mkubwa! Madaktari wanapowahudumia watoto wadogo waoneshe unyenyekevu, ili kugundua siri zinazofumbatwa katika maisha ya watoto wagonjwa! Madaktari wawe na mvuto kwa watoto pamoja na kuwa tayari kuwapokea na kuwahudumia kwa upendo kama alivyofanya Kristo Yesu katika maisha na utume wake! Madaktari waendelee kujisadaka bila ya kujibakiza kadiri ya utaalam na nafasi yao kwa ajili ya huduma kwa watoto wagonjwa. Wawe na ujasiri wa kuangalia shida za watoto wagonjwa kwa wakati huu na kujipanga vizuri zaidi kwa siku za mbeleni!

Madaktari wakifanikiwa kuishi na kutenda yote haya, kwa hakika anasema Baba Mtakatifu watakuwa wametekeleza utume wao unaobubujika kutoka katika akili na nyoyo zao, tayari kuhudumia wakati na mahali popote pale! Mtindo huu wa maisha ni ushuhuda wa tunu msingi za Kikristo zinazopaswa kumwilishwa katika huduma, ili kukuza haki na usawa katika mfumo wa huduma ya afya kwa jamii. Huduma hii itekelezwe kwa unyenyekevu, ujuzi na welezi mkubwa, kwa wagonjwa wote watakaokutana nao!

Papa: Madaktari

 

 

21 March 2019, 15:15