Tafuta

Papa Francisko anawataka waamini kulinda na kutunza ndimi zao kwani ni hatari sana kwa umoja, ustawi na mafungamano ya kijamii. Papa Francisko anawataka waamini kulinda na kutunza ndimi zao kwani ni hatari sana kwa umoja, ustawi na mafungamano ya kijamii. 

Papa Francisko: Umbeya si mtaji! Hatari sana! Tunzeni ndimi zenu

Baba Mtakatifu anasema, umbeya na majungu ni hatari sana kwa umoja, mshikamano na mafungamano ya kijamii, kwa sababu unapandikiza chuki, uhasama na adui kati ya watu na huo ndio mwanzo wa vita na misigano ya kijamii. Matokeo yake ni uharibifu mkubwa wa maisha ya watu na mali zao. Umbeya si mtaji bali ni sawa na “bomu la atomiki” linaloweza kusababisha maafa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anaendelea na utume wake wa kukutanana na kuzungumza na watu wa familia ya Mungu walioko pembezoni mwa vipaumbele vya jamii ili kuwaonjesha furaha ya Injili. Jumapili jioni tarehe 3 Machi 2019, Baba Mtakatifu ametembelea Parokia ya Mtakatifu Crispin wa Viterbo iliyoko Jimbo kuu la Roma, ili kusali pamoja na watu wa familia ya Mungu. Katika mahubiri yake, Baba Mtakatifu amekazia umuhimu wa waamini kufuata hekima ya Kikristo inayofumbatwa katika Heri za Mlimani, ili waweze kutambulikana na hatimaye, kuzaa matunda mema na matakatifu!

Baba Mtakatifu anawataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuondokana na unafiki katika maisha, bali wawe na ujasiri wa kuchunguza dhamiri zao, ili kuona udhaifu na mapungufu yao, tayari kutubu na kumwongokea Mungu. Ni kutokana na ubinafsi kwamba, watu wengi wanashindwa kuona vilema na mapungufu katika maisha yao, bali wanakuwa wataalam na watu waliobobea kusema na kutangaza mapungufu ya jirani zao. Haya ni matokeo ya dhambi ya asili yanayopelekea watu kuwalaani wenzao pamoja na kutangaza mapungufu yao hadharani. Kristo Yesu, katika Injili anawaalika wafuasi wake kuondoa kwanza boriti katika macho yao, ili kuweza kuona kibanzi kilichoko kwenye jicho la ndugu yao!

Katika maisha na utume wake, Kristo Yesu, daima alipambana na watu wanafiki; wenye maisha ya “undumila kuwili” kama alivyofanya kwa Mafarisayo na Waandishi, waliokuwa wepesi kuwanyooshea wengine vidole na kusahau mapungufu yao. Baba Mtakatifu anasema, umbeya na majungu ni hatari sana kwa umoja, mshikamano na mafungamano ya kijamii, kwa sababu unapandikiza chuki, uhasama na adui kati ya watu na huo ndio mwanzo wa vita na misigano ya kijamii. Matokeo yake ni uharibifu mkubwa wa maisha ya watu na mali zao.

Umbeya si mtaji bali ni sawa na “bomu la atomiki” linaloweza kusababisha maafa makubwa! Baba Mtakatifu anakaza kusema haya ni maonyo ambayo yamo kwenye Waraka wa Mtume Yakobo kwa Watu wote Sura ya 3:1-12! Anasema ulimi ni kiungo kidogo, lakini kinaweza kusababisha madhara makubwa, kumbe, huu ni mwaliko wa kudhibiti ulimi. Waamini wawe na ujasiri wa kukosoana na kurekebishana katika upendo. Kipindi cha Kwaresima, iwe ni fursa kwa waamini kuchukua fursa kidogo na kuanza kutafakari kuhusu unafiki, ili baada ya Kipindi cha Kwaresima, waamini waweze kupima tena maisha yao, ikiwa kama kweli wamefanikiwa, ili waweze kufufuka na Kristo Yesu katika upya wa maisha!

Hii ni changamoto kubwa na endelevu katika maisha anasema Baba Mtakatifu Francisko. Unafiki ni kazi ya Shetani. Ili kupambana na tabia ya kinafiki, Baba Mtakatifu anawaalika waamini kujenga tabia na mazoea ya kusali na kuwaombea wale wote wanaotopea katika dhambi na ubaya wa moyo. Waamini wamwelekezee Mungu tatizo na changamoto zinazowakabili, ili wao wenyewe waweze “kufunga mdogo”. Bila sala ni vigumu kuweza kusonga mbele! Dawa ya pili kwa wale wanaojisikia kutoka katika undani wao kwamba, wanataka kuwashutumu wengine, wawe na ujasiri wa “kung’ata ulimi”! Kwa njia hii, watashindwa kusema mabaya ya wengine kutokana na maumivu. Umefika wakati kwa waamini kuondoa maboriti machoni pao ili hatimaye, kuweza kuona vibanzi vya jirani zao. Mwishoni, Baba Mtakatifu anawaalika waamini kumwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kuwapatia neema na baraka ya kuondokana na maisha ya kinafiki!

Papa: Mt. Crispin: Mahubiri
04 March 2019, 10:37