Tafuta

Vatican News
Papa Francisko, Jumapili ya II ya Kwaresima amefafanua maana ya Fumbo la Mateso katika maisha ya Wakristo mintarafu mwanga wa Fumbo la Pasaka! Papa Francisko, Jumapili ya II ya Kwaresima amefafanua maana ya Fumbo la Mateso katika maisha ya Wakristo mintarafu mwanga wa Fumbo la Pasaka! 

Papa Francisko: Maana ya Fumbo la mateso kwa Wakristo!

Mateso ni hatua muhimu sana katika maisha na utume wa Kristo Yesu, lakini hiki ni kipindi cha mpito! Kung’ara kwa Yes uni tukio linaloonesha dhana ya mateso katika maisha ya Kikristo. Ni mwaliko kwa Wakristo kugeuka sura zao na kung’ara kama alivyokuwa Kristo Yesu. Yeye ni wokovu, chemchemi ya maisha yenye heri, mwanga na kiini cha upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya II ya Kipindi cha Kwaresima, Mwaka C wa Kanisa, inatoa fursa kwa waamini kulitafakari Fumbo la Kristo Yesu kugeuka sura mbele ya Mitume wake: Petro, Yakobo na Yohane, ili kuonja utukufu wa Fumbo na Ufufuko, wakiwa bado hapa duniani. Tukio hili linafanyika kwenye mlima mrefu faraghani, kielelezo cha mwanga na mang’amuzi ambayo Kristo Yesu alipenda kuwashirikisha Mitume wake watatu, wakati akiwa amezama katika sala!

Wanafunzi hawa wakafunikwa na wingu jeupe na kutokewa na Eliya pamoja na Musa aliyekuwa anazungumza na Kristo Yesu kuhusu “Fumbo la Mateso yake” yaani: Fumbo la Pasaka: mateso, kifo na ufufuko uletao wokovu, kiasi cha Mtakatifu Petro kupigwa na butwaa akitaka kipindi hiki cha neema kuendelea zaidi pasi na ukomo. Tukio hili linakuja baada ya Kristo Yesu, kuwashirikisha Mitume wake kuhusu utume ambao ungepelekea kuteswa, kufa na kufufuka siku ya tatu kama ilivyoandikwa. Yesu alitambua fika kwamba, Mitume wake, hawakuwa tayari kupokea “Kashfa ya Fumbo la Msalaba”.

Kristo Yesu, aliwaandaa Mitume, ili watambue kwamba, ni kwa njia ya mateso, Mwenyezi Mungu anamwezesha Mwanaye wa pekee kufikia utukufu, kwa kufufuka kutoka kwa wafu. Hii ndiyo njia watakayoifuata hata Mitume kwa kufuata nyayo za Yesu, ili hatimaye, waweze kufikia maisha ya uzima wa milele. Huu ni mwaliko wa kila mtu kuuchukua vyema Msalaba wa maisha yake hapa duniani. Mwenyezi Mungu tangu awali anawajalia waamini kuona hatima ya maisha yao ambayo ni Fumbo la Ufufuko kwa kutambua uzuri pamoja na kubeba vyema Misalaba yao!

Hii ni sehemu ya tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili tarehe 17 Machi 2019 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Baba Mtakatifu anasema, hii ni hatua muhimu sana katika maisha na utume wa Kristo Yesu, lakini hiki ni kipindi cha mpito! Kung’ara kwa Yesu ni tukio linaloonesha dhana ya mateso katika maisha ya Kikristo. Ni mwaliko kwa Wakristo kugeuka sura zao na kung’ara kama alivyokuwa Kristo Yesu. Yeye ni wokovu, chemchemi ya maisha yenye heri, mwanga na kiini cha upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka.

Kristo Yesu kwa kuwafunulia Mitume wake utukufu, anapenda kuwahakikishia kwamba, misalaba ya maisha, majaribu na matatizo mbali mbali wanayokumbana nayo yana suluhu, hatima na kikomo chake katika Fumbo la Pasaka. Baba Mtakatifu katika Kipindi hiki cha Kwaresima, anawaalika waamini kupanda na Kristo Yesu, kwenda mlimani kwa faragha kwa njia ya: Sala na ukimya wa roho ili kutafuta na kuonja uwepo endelevu wa Mungu katika maisha yao. Waamini wajitahidi kubaki peke yao kwa faragha mbele ya Kristo, kwa kumwangalia, ili mwanga angavu wa maisha yake, uweze kupenyeza hata katika maisha yao.

Mwinjili Luka anakazia kwa kusema, Kristo Yesu aligeuka sura alipokuwa akisali; akizungumza na Baba yake wa milele; kilele cha utimilifu wa Sheria na Unabii kwa uwepo wa Nabii Eliya na Musa, waliofafanua wokovu ulioletwa na Mwenyezi Mungu kwa njia ya Fumbo la Msalaba, kiasi kwamba, utukufu wa Mungu ukawafunika hata wale waliokuwa nje. Kumbe, Sala katika Fumbo la Utatu Mtakatifu linamgeuza mtu kutoka katika undani wa maisha yake, kiasi cha kuweza kuwa ni shuhuda wa mwanga angavu wa maisha kwa jirani zake! Sala ina uwezo wa kumgeuza mtu kutoka katika undani wake.

Mwishoni mwa tafakari yake, Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuwaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kuendelea na safari ya Kipindi cha Kwaresima kwa furaha, kwa kutoa nafasi kwa Sala na Tafakari ya Neno la Mungu. Bikira Maria awafundishe waamini kubaki na Kristo Yesu, hata pale inapoonekana kana kwamba hawamfahamu wala kumwelewa. Ni kwa njia ya waamini kubaki wakiwa wameungana na Kristo Yesu watafanikiwa kuona utukufu wake!

Papa: Kung'ara Bwana
17 March 2019, 12:34