Papa Francisko anaitaka familia ya Mtakatifu Camillo wa Lellis kudumisha: Huduma kwa wagonjwa, karama, utakatifu wa maisha na kumwilisha dhana ya Sinodi katika maisha na utume wao! Papa Francisko anaitaka familia ya Mtakatifu Camillo wa Lellis kudumisha: Huduma kwa wagonjwa, karama, utakatifu wa maisha na kumwilisha dhana ya Sinodi katika maisha na utume wao! 

Papa Francisko: Huduma kwa wagonjwa, karama na utakatifu!

Baba Mtakatifu anawaalika wanafamilia hawa kuiga mifano bora ya ndugu zao, ambao wamejipambanua kwa huduma ya kinabii na utakatifu wa maisha; kwa kuendelea kusoma alama za nyakati, kwa kutambua aina mpya ya utume, ili kujibu mahitaji ya Kanisa kwa wakati huu kwa kutambua kwamba, upendo haupungui neno wakati wowote! Wanatumwa kutangaza Injili ya upendo kwa watu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Hivi karibuni, Familia ya Mtakatifu Camillo wa Lellis, iliadhimisha Jubilee ya miaka 400 tangu muasisi wa Shirika hili alipofariki dunia, changamoto na mwaliko kwa wanashirika hawa kuwa kweli ni alama ya Yesu Kristo, Msamaria mwema anayejinyenyekesha kwa ajili ya kuwaganga watu majeraha ya mwili na roho: kwa kuwapaka mafuta ya faraja na divai ya matumaini. Hili ni Shirika ambalo limejisadaka sana kwa ajili ya wagonjwa, utume muhimu sana katika Kanisa na Jamii katika ujumla wake.

Wanashirika hawa, wamekuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma na upendo wa Mungu kwa wagonjwa, wanaposikia hitaji la kupata tiba na faraja; ili hatimaye, kupata tena afya njema au kwa kuwapata wasindikizaji watakaowasaidia kukutana na Kristo Yesu! Kanisa linaitwa na kutumwa kujenga Ufalme wa Mungu, kwa kuwaganga wagonjwa, kwa kumuiga Kristo Yesu, Msamaria mwema, aliyejitaabisha kuwaganga na kuwaponya wagonjwa. Hivi ndivyo alivyofanya pia Mtakatifu Camillo wa Lellis, kwa kuwa ni shuhuda wa upendo wa Kristo wenye huruma kwa wagonjwa na kuufanya utume huu, kuwa ni sehemu ya karama ya Shirika lake. Hii ni huduma inayotolewa moja kwa moja kwa wagonjwa na maskini, lakini zaidi kwa wenye mahitaji ya: kiroho na kimwili pamoja na kuendelea kuwa ni mfano bora wa huduma inayotolewa na Mama Kanisa kwa ajili ya binadamu wote!

Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu, tarehe 18 Machi 2019 alipokutana na kuzungumza na Familia ya Mtakatifu Camillo wa Lellis. Amewakumbusha kwamba, karama ni zawadi ya Roho Mtakatifu, inayopaswa kutumiwa kikamilifu kwa kuwashirikisha jirani zao na hasa zaidi kwa ajili ya mafao ya watu wa Mungu katika ujumla wao. Karama ya kweli ni kwa ajili ya huduma kwa jirani, inayotekelezwa kwa uaminifu kama sehemu ya utekelezaji wa utume na huduma kwa wagonjwa sehemu mbali mbali duniani! Baba Mtakatifu anawaalika wanafamilia hawa kuiga mifano bora ya ndugu zao, ambao wamejipambanua kwa huduma ya kinabii na utakatifu wa maisha; kwa kuendelea kusoma alama za nyakati, kwa kutambua aina mpya ya utume, ili kujibu mahitaji ya Kanisa kwa wakati huu kwa kutambua kwamba, upendo haupungui neno wakati wowote!

Watambue kwamba, wanaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Injili ya upendo, ili watu waweze kuwa na uzima tele, kwa kuhudumia maisha pamoja na kudumisha afya ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Karama ya huduma kwa wagonjwa, imewawezesha kuunda familia moja inayojikita katika karama, kwa kuwaunganisha: wakleri, watawa na waaamini walei, kila kundi likijitahidi kuimwilisha kadiri ya wito, historia na mazingira husika. Hii ni sadaka inayotolewa Altareni kwa ajili ya kutajirishana, mafao ya wengi sanjari na utekelezaji wa utume kama ushuhuda wa upendo wa Kristo wenye huruma kwa wagonjwa. Mtakatifu Camillo wa Lellis katika maisha na utume wake, akaona hitaji la huduma kwa wagonjwa linalotolewa kwa jicho pendelevu la kimama. Ni katika muktadha huu, kukazaliwa Mashirika mawili ya kitawa kwa ajili ya huduma ya wagonjwa. Bikira Maria afya ya wagonjwa na Mama wa watawa, akawa ni msimamizi wao!

Baba Mtakatifu amewataka wanafamilia ya Mtakatifu Camillo wa Lellis kumwilisha katika maisha na utume wao, “dhana ya Sinodi”, mchakato ambao kwa sasa unavaliwa njuga na Kanisa zima, ili kukuza na kuimarisha karama na umoja wa Shirika, daima wakiendelea kuwa waaminifu kwa waasisi wa Mashirika yao, ili kusikiliza na kujibu kilio cha maskini wa nyakati hizi kama mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka!

Papa: Huduma kwa wagonjwa
18 March 2019, 15:07