Tafuta

Mtakatifu Paulo VI: Waraka wa Kitume, "Humanae vitae" yaani "Maisha ya binadamu" unajadiliwa huko Kigali, Rwanda. Mtakatifu Paulo VI: Waraka wa Kitume, "Humanae vitae" yaani "Maisha ya binadamu" unajadiliwa huko Kigali, Rwanda. 

Waraka wa Mt. Paulo VI: Maisha ya Binadamu wajadiliwa Rwanda!

Lengo la Waraka huu wa kitume ni uhai wa binadamu dhidi ya utamaduni wa kifo unaokumbatiwa na sera pamoja na mikakati ya utoaji mimba. Huu ni urithi mkubwa wa Mtakatifu Paulo VI katika maisha, utume wa Kanisa na mafao ya binadamu wote! Hii ni sehemu ya ujumbe ulioandikwa na Kardinali Kevin Joseph Farrell, kwa washiriki wa Mkutano wa Kimataifa huko Kigali, Rwanda.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mtakatifu Paulo VI hapo tarehe 25 Julai 1968, takribani miaka 50 iliyopita, alichapisha Waraka wa Kitume: “Humanae vitae” yaani “Maisha ya binadamu”. Ni waraka wa kinabii unaobainisha dhamana na wajibu wa wanandoa wanaoushiriki katika kazi ya uumbaji, ili kuendeleza zawadi ya maisha kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Ni dhamana ambayo inapaswa kumwilishwa katika furaha ya maisha na utume wao ndani ya familia. Lengo la Waraka huu wa kitume ni uhai wa binadamu dhidi ya utamaduni wa kifo unaokumbatiwa na sera pamoja na mikakati ya utoaji mimba. Huu ni urithi mkubwa wa Mtakatifu Paulo VI katika maisha, utume wa Kanisa na mafao ya binadamu wote!

Hii ni sehemu ya ujumbe ulioandikwa na Kardinali Kevin Joseph Farrell, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha kwa washiriki wa Mkutano wa Kitaifa kuhusu Waraka wa Kitume: “Humanae vitae” yaani “Maisha ya binadamu” huko Kigali, Rwanda, kuanzia tarehe 9-10 Februari 2019. Ni mkutano ambao umeandaliwa kwa ushiriki kati ya Baraza la Maaskofu Katoliki Rwanda, Jimbo kuu la Kigali pamoja na Mfuko wa Familia ya Wapallotini Kimataifa.

Vatican inatambua fika changamoto za kisiasa na kijamii katika masuala ya elimu ya jinsia inayotolewa nchini humo, hali inayoweza kuwaundia vijana mawazo tenge kuhusu: maana, uzuri na utakatifu wa tendo la ndoa katika maisha kifamilia. Mkutano huu, pamoja na mambo mengine, umejielekeza zaidi kuhusu tunu msingi za maisha ya ndoa na famili zinazofumbatwa katika upendo wa kweli na usiogawanyika. Waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema wanahimizwa kuwajibika katika kukuza na kudumisha tunu msingi za ndoa na familia pamoja na kukazia Mpango wa Uzazi kwa Njia ya Asili. Mkutano huu unahudhuriwa na wajumbe 300 kutoka katika medani mbali mbali za maisha!

Papa Paulo VI alikuwa na upeo mpana na uwezo wa kuona mbali sana, akagundua changamoto na vikwazo vinavyowakabili wanandoa; akabainisha wajibu wa Kanisa kama Mama na Mwalimu na kuwataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kusimama kidete kulinda, kutangaza na kushuhudia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo! Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo ni kati ya mafundisho mazito ya Mtakatifu Paulo VI, anayekita mawazo yake katika dhamana na wajibu wa uumbaji, malezi, makuzi na elimu ya watoto. Wanandoa wanapaswa kufikiri, kujiandaa kikamilifu, kusindikizana na hatimaye, kupokea mtoto kama zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, dhamana inayowawajibisha!

Hizi ni changamoto zilizoibuliwa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, zinazotaka waamini kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya furaha ya Injili kwa kujikita katika kanuni maadili na utu wema, sadaka na majitoleo binafsi. Nchi zilizoendelea ziliona kwamba, ongezeko la watu duniani, lilikuwa ni tishio kwa ustawi na maendeleo yao. Kutokana na mantiki hii, wachumi wakawatangazia watu raha, starehe na anasa kwa kufumbata utamaduni wa kifo na matokeo yake, leo hii kuna nchi ambazo zinalia na kuomboleza kutokana na kuwa na idadi ndogo sana ya watoto wanaozaliwa kila mwaka pamoja na kuendelea na kuwa na idadi kubwa ya watu wenye umri mkubwa.

Mkutano wa Familia Rwanda
09 February 2019, 14:02