Tafuta

Siku ya Wagonjwa Duniani 2019: Kauli mbiu "Mmepata bure, toeni bure" Siku ya Wagonjwa Duniani 2019: Kauli mbiu "Mmepata bure, toeni bure" 

UJUMBE WA PAPA KWA SIKU YA WAGONJWA DUNIANI 2019

Kila mwanadamu ni maskini, mhitaji na fukara na daima ataendelea kubaki kuwa tegemezi katika hali mbali mbali za maisha, hivyo unyenyekevu uwasaidie watu kukubali udhaifu na hivyo kuwa tayari kushirikiana na wengine kama tendo la fadhila katika maisha. Hali hii itasaidia kukuza mema kwa mtu binafsi na jamii katika ujumla wake pamoja na kuguswa na mahangaiko ya wengine.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya 27 ya Wagonjwa Duniani huko Calcutta, nchini India kuanzia tarehe 9-11 Februari 2019 kinaongozwa na kauli mbiu “Mmepata bure, toeni bure”. Mt. 10:8. Huu ni mwaliko kwa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kuhakikisha kwamba, wanajisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma makini kwa wagonjwa sehemu mbali mbali za dunia, kama alivyofanya Msamaria mwema. Wagange kwa mafuta ya faraja na divai ya matumaini.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa maadhimisho haya anasema, Kanisa kama Mama anawakumbusha watoto wake kuwa wakarimu na watu wenye upendo kwa wagonjwa. Wawe mstari wa mbele katika kuwajali na kuwatunza wagonjwa wanaohitaji kuonjeshwa utaalam na weledi; upole, unyoofu na unyenyekevu kwa kujisadaka bila ya kujibakiza, ili wagonjwa waweze kutambua kwamba, wanapendwa na kuthaminiwa! Baba Mtakatifu anaonya kwamba, maisha ya binadamu kamwe hayawezi kubinafsishwa hasa kutokana na maendeleo makubwa ya sayansi ya tiba ya mwanadamu na teknolojia yanayotoa kishawishi cha watu kutaka kuchezea maisha.

Katika ulimwengu wa utandawazi usiojali wala kuguswa na maendeleo ya wengine, ukarimu ni zawadi ambayo inapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza, kwani hii ni asili ya Mungu na kilele cha ukarimu wa Mungu ni katika Fumbo la Umwilisho pamoja na Roho Mtakatifu kuwashukia Mitume. Kila mwanadamu ni maskini, mhitaji na fukara na daima ataendelea kubaki kuwa tegemezi katika hali mbali mbali za maisha, hivyo unyenyekevu uwasaidie watu kukubali udhaifu na hivyo kuwa tayari kushirikiana na kufungamana na wengine kama tendo la fadhila katika maisha. Hali hii itasaidia kukuza mema kwa mtu binafsi na jamii katika ujumla wake pamoja na kuungana ili kukuza umoja unaojali na kuguswa na mahangaiko ya wengine.

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, maadhimisho ya Mwaka 2019 yanafanyika Calcutta, nchini India kama njia ya kumuenzi Mama Theresa wa Calcutta, mfano wa ukarimu, upendo na huruma ya Mungu kwa maskini na wagonjwa. Maisha yake yote, yalikuwa ni kutangaza na kushuhudia huruma na upendo wa Mungu! Akasimama kidete na kuwa kweli mtetezi wa Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo! Daima ndani ya maskini na wale wote walioachwa pweke kandoni mwa barabara, aliiona ile sura na mfano wa Mungu!

Mama Theresa wa Calcutta akawa ni sauti ya wanyonge, ili kuamsha dhamiri kwa viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa ili waweze kujifunga kibwebwe, kupambana na umaskini. Katika ushuhuda huu, Mama Theresa akawa ni nuru ya ulimwengu na  chumvi ya dunia, mwaliko wa kujisadaka bila ya kujibakiza ili kuzima kiu ya uelewa wa upendo na huruma ya Mungu kwa waja wake, hasa wale wanaoteseka. Ukarimu uwe ni sehemu ya vinasaba na utambulisho wa wahudumu katika sekta ya afya, kama ilivyokuwa kwa Msamaria mwema. Huduma ya kujitolea kuwasaidia wagonjwa na maskini ni sehemu ya mchakato wa kutetea na kudumisha haki msingi kwa wagonja na hasa zaidi wagonjwa wanaoteseka kwa magonjwa ya muda mrefu!

Baba Mtakatifu anawataka wadau katika sekta ya afya kuongeza jitihada za kuzua magonjwa pamoja na kuwasaidia wagonjwa hawa katika maisha yao ya kiroho. Watu wa kujitolea wawe ni mfano bora wa urafiki kati ya Kanisa na wagonjwa; kwa kujenga sanaa ya kusikiliza na kujali: hisia, matatizo na machungu ya wagonjwa! Wawe mstari wa mbele kushiriki katika mchakato wa matibabu, ili kuwarudishia tena wagonjwa matumaini, hali inayoweza kusaidia maboresho makubwa ya matibabu. Watu wa kujitolea wawe ni vyombo na mashuhuda wa maadili na matendo yanayojikita katika misingi ya ukarimu, ili kweli huduma ya afya iwe ni ya kibinadamu zaidi.

Baba Mtakatifu anapenda kuhimiza roho ya ukarimu na sadaka ili kushinda kishawishi cha uchu wa kutaka kupata faida kubwa kwa hasara ya utu na heshima ya binadamu. Taasisi za afya zinazomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki ziwe ni mfano bora wa huduma kwa wagonjwa, kwa kuongozwa na tunu msingi za Kiinjili. Ziwe ni chemchemi ya ukarimu, huruma na upendo badala ya kugeuzwa kuwa ni “kichaka” cha kuwanyonya wagonjwa. Kipaumbele cha kwanza ni utu, heshima na huduma kwa wagonjwa na wala si faida.

Baba Mtakatifu anahitimisha ujumbe wake kwa Siku ya 27 ya Wagonjwa Duniani kwa kuwataka wadau katika sekta ya afya kutambua kwamba, hii ni huduma shirikishi inayohitaji kushirikiana, kuaminiana, kushikamana na hatimaye kujenga urafiki. Hii ni amana na utajiri mkubwa hasa pale sadaka inapotolewa kwa ajili ya wengine! Furaha ya kujitoa kwa ajili ya wengine ni kipimo thabiti cha afya ya Mkristo! Baba Mtakatifu anawakabidhi watu wote chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria Mfariji wa wagonjwa, ili awasaidie watu kushirikishana karama kwa moyo radhi, kwa kusikilizana na kupokeana jinsi walivyo; kwa kuishi na kushirikiana kama ndugu katika Kristo Yesu. Kwa njia hii, wataweza pia kutambua mahitaji ya jirani zao na hivyo kutoa kwa ukarimu na hivyo kuendelea kujifunza kujisadaka kwa ajili ya wengine!

Papa Siku Wagonjwa 2019
09 February 2019, 15:11