Siku kuu ya Kutolewa Bwana Hekaluni & Siku ya XXIII ya Watawa Duniani kwa Mwaka 2019 Siku kuu ya Kutolewa Bwana Hekaluni & Siku ya XXIII ya Watawa Duniani kwa Mwaka 2019 

Siku kuu ya Kutolewa Bwana Hekaluni: Siku ya Watawa Duniani

Maadhimisho ya Siku ya Watawa Duniani ni fursa ya kuangalia matumaini ya ongezeko la miito ya kitawa ndani ya Kanisa; changamoto mbali mbali zinazoendelea kujitokeza katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia pamoja na umuhimu wa ushuhuda wenye mvuto na mashiko kutoka kwa walezi waliokabidhiwa dhamana na jukumu la kuwasindikiza vijana!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Katika maadhimisho ya Siku kuu ya Kutolewa Bwana Hekaluni sanjari na maadhimisho ya Siku ya XXIII ya Watawa Duniani, Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, tarehe 2 Februari 2019, saa 11:30 jioni kwa Saa za Ulaya anatarajiwa kuongoza Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Ibada hii itatanguliwa na maandamano ya mishumaa, kielelezo cha hija ya Bikira Maria na Mtakatifu Yosefu kwenda kumpeleka Kristo Yesu Hekaluni, ili kukutana na watu wake waliokuwa wanamsubiri Masiha katika imani.

Watu hawa wanawakilishwa na Mzee Simeoni na Nabii Ana, waliomtambua Yesu kuwa ni mwangaza wa Mataifa na utukufu kwa watu wa Israeli. Kwa maandamano yatakayoongozwa na Baba Mtakatifu, waamini na kwa namna ya pekee kabisa watawa katika Siku kuu yao, watashiriki kwenda kukutana na Kristo Yesu katika Neno na wakati wa kuumega mkate, yaani wakati wa maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu. Maadhimisho ya Siku  ya Watawa Duniani ni fursa ya kuangalia matumaini ya ongezeko la miito ya kitawa ndani ya Kanisa; changamoto mbali mbali zinazoendelea kujitokeza katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia pamoja na umuhimu wa ushuhuda wenye mvuto na mashiko kutoka kwa walezi waliokabidhiwa dhamana na jukumu la kuwasindikiza vijana wanaotaka kujisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake!

Watawa wanakumbushwa kwamba, katika maisha na utume wao, watambue kwamba, daima mbele yao kuna ndugu zao katika Kristo Yesu wanaopaswa kuwapenda, kuwaheshimu na kuwathamini badala ya kuthamini vitu na hivyo kusahau utu, heshima na mahitaji msingi ya binadamu katika maisha ya kitawa! Watawa wanapaswa kujenga na kudumisha umoja na udugu, upendo na mshikamano wa dhati katika maisha na utume wao, licha ya changamoto mbali mbali wanaozokumbana nazo katika hija ya maisha na utume wao ndani ya Kanisa na jamii katika ujumla wake!

Baba Mtakatifu anawataka watawa kutambua kwamba, wito na hatimaye safari ya maisha na utume wao, inapata chimbuko kwa kukutana na Kristo Yesu katika maisha yao, changamoto ya kuhakikisha kwamba, daima wanalikumbuka tukio hili hatimaye, kuweza kuona uwepo wa watu wa Mungu pamoja na Kristo Yesu. Ni tukio linalolikutanisha Kanisa; vijana na wazee wakati ambapo Bikira Maria na Mtakatifu Yosefu wanatekeleza sheria, taratibu na kanuni za jamii yao. Mzee Simeoni na Nabii Ana wanawakilisha Unabii unaohifadhi mambo ya kale na vijana wanaonesha matumaini kwa siku za usoni!

Baba Mtakatifu anawaambia watawa kwamba, wanaweza kupyaisha mkutano na jirani zao kwa kuendelea kuandamana kwa pamoja, huku Mwenyezi Mungu akiwa ni kiini cha safari na hija yao. Wazee wanazo funguo za maarifa zinazotakiwa na vijana ili kukua na kuzaa matunda yanayokusudiwa. Unabii unafumbatwa kwa namna ya pekee katika kumbu kumbu ili kuweza kuwakutanisha watu. Inasikitisha kuona kwamba, kutokana na haraka ya binadamu katika ulimwengu mamboleo, baadhi ya watu wanataka kufunga malango ya maisha kutokana na hofu na wasi wasi, wakati ambapo maduka makubwa yanaendelea kuwa wazi pengine hata usiku kucha.

Watawa wanapaswa kutambua kwamba, mbele yao kuwa ndugu zao katika Kristo wanaopaswa kuwapenda, kuwaheshimu na kuwathamini, badala ya kuthamini simu ya kiganjani. Maisha ya kuwekwa wakfu hayana budi kutoa kipaumbele cha kwanza katika ushuhuda wenye mvuto, ili kuendelea kutangaza na kushuhudia matendo makuu ya Mungu, ili hatimaye, kuzaa matunda yanayokusudiwa, kwani maisha yao yamejikita katika mizizi ya kweli na wala si kutoa kipaumbele cha kwanza kwa miradi, teknolojia na miundo mbinu kwani kwa kufanya hivi, maisha ya kitawa yatakuwa butu pasi na mvuto wala mashiko! Jirani na mahitaji yake msingi ni muhimu kuliko mambo yote!

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, maisha ya kitawa yanapata chimbuko lake kwa kukutana na Kristo Yesu ambaye ni fukara, mseja na mtii! Hiki ni kielelezo cha huruma na upendo wa Mungu unaohitaji jibu makini bila kumung’unya mung’unya maneno, ili kumfuasa na kumuiga Yesu: fukara, mseja na mtii. Utawa unapania kuyaacha malimwengu na utajiri wake; furaha na anasa zake; ubinafsi na uchoyo wake, ili kumwambata Kristo Yesu, Jana, Leo na Daima. Maisha ya kitawa yanasimikwa katika nadhiri ya utii kama kielelezo cha hali ya juu kabisa cha uhuru wa mtu! Ni maisha yanayojazwa kwa amani na Injili ya furaha kwa kuwawezesha wazee kuhitimisha maisha yao kwa furaha inayojikita katika sakafu ya mioyo yao, kwani mikononi mwao, wamemkumbatia Kristo Yesu!

Baba Mtakatifu anawataka watawa kuhakikisha kwamba, wanamkumbatia Kristo Yesu na kumhifadhi katika ushuhuda wa maisha yao: wakati wa sala, wanapokuwa mezani; wanapokuwa wakizungumza kwa simu; wanapokuwa shuleni wakifundisha na kusoma; wanapowahudumia maskini na wahitaji, yaani, watawa wanapaswa kumkumbatia Kristo Yesu katika uhalisia wa maisha yao ya kila siku, kielelezo cha neema ya Mungu inayotenda kazi ndani mwao. Ili kuendelea kuwasha moto wa maisha ya kiroho, watawa hawana budi kuhakikisha kwamba, daima wanakutana na Kristo Yesu, kwa kuondokana na litania ya malalamiko yasiyokuwa na “kichwa wala miguu”, malalamiko ambayo yamekuwa kama wimbo usiokuwa na kiitikio!

Kutolewa Bwana Hekaluni
01 February 2019, 16:54