Tafuta

Vatican News
Papa Francisko asikitishwa na vifo vya wakimbizi na wahamiaji kutoka Haiti! Papa Francisko asikitishwa na vifo vya wakimbizi na wahamiaji kutoka Haiti!  (AFP or licensors)

Papa Francisko asikitishwa na maafa huko Haiti!

Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kusali kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea wote waliofariki dunia au kuguswa kwa namna ya pekee kutokana na kuzama kwa boti hii ambayo ilikuwa imebeba wahamiaji wengi. Anawaombea waliopata majeraha kupona haraka ili waendelee na shughuli zao. Katika tukio hili, watu 17 waliweza kuokolewa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mwishoni mwa Katekesi mintarafu hija yake ya kitume huko Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu, Jumatano tarehe 6 Februari 2019, ameonesha masikitiko yake makubwa kutokana na wakimbizi na wahamiaji 28 kutoka Haiti waliokuwa wanaelekea kwenye Kisiwa cha Bahamas kuzama na kufa maji, Jumamosi, tarehe 2 Februari 2019. Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, hawa ni watu waliokuwa wanatafuta: usalama, hifadhi na maisha bora zaidi, lakini mauti imewafika kabla ya kutekeleza ndoto ya maisha yao.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kusali kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea wote waliofariki dunia au kuguswa kwa namna ya pekee kutokana na kuzama kwa boti hii ambayo ilikuwa imebeba wahamiaji wengi. Anawaombea waliopata majeraha kupona haraka na hatimaye, kuendelea na shughuli zao. Katika tukio hili, watu 17 waliweza kuokolewa. Kutokana na hali ngumu ya maisha, umaskini na majanga mbali mbali, watu wengi kutoka Haiti wamekuwa wakitafuta hifadhi, usalama na maisha bora zaidi kwenye visiwa vya jirani. Katika kipindi cha mwaka 2019, zaidi ya wakimbizi na wahamiaji 300 wamekamatwa kwa kuingia nchi jirani bila kuwa na nyaraka rasmi.

Papa: Vifo Haiti
06 February 2019, 14:58