Cerca

Vatican News
Papa Francisko katika hotuba yake kwa Wabunge wa Monaco amekazia umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa kujikita katika kanuni maadili na utu wema! Papa Francisko katika hotuba yake kwa Wabunge wa Monaco amekazia umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa kujikita katika kanuni maadili na utu wema!  (Vatican Media)

Papa Francisko: Kanuni maadili na utu wema vipewe kipaumbele!

Baba Mtakatifu Francisko anasema, kuliko wakati mwingine wowote katika historia ya maendeleo ya mwanadamu, kanuni maadili na utu wema vinapaswa kupewa msukumo wa pekee, kwani inaonekana kana kwamba, sayansi inahatarisha maendeleo yaliyokwisha kupatikana. Amani ni tunu inayopaswa kuvaliwa njuga na Jumuiya ya Kimataifa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika Maadhimisho ya Siku ya 52 ya Kuombea Amani Duniani kwa Mwaka 2019 uliongozwa na kauli mbiu “Siasa safi ni huduma ya amani”. Siasa safi ni msingi wa maendeleo endelevu na fungamani; demokrasia shirikishi na uongozi bora unaojikita katika hoja zenye mashiko na huduma kwa wananchi. Siasa safi inafumbatwa katika mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Utu na heshima ya binadamu viheshimiwe kadiri ya Katiba ya Ufalme wa Monaco!

Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, tarehe 2 Februari 2019, alipokutana na kuzungumza na Wabunge kutoka katika Bunge la Ufalme wa Monaco. Amewashukuru na kuwapongeza kwa kuendeleza mapokeo ya kutunza mazingira nyumba ya wote mintarfu kazi kubwa inayotekelezwa na Mfuko wa Albert wa II wa Ufalme wa Monaco. Leo hii, changamoto kubwa ni athari za mabadiliko ya tabianchi, hali ambayo inatishia usalama na amani ya watu wanaoishi katika mwambao wa bahari sehemu mbali mbali za dunia. Wabunge hawa, wamekuwa wakishirikiana na Makanisa pamoja na wadau mbali mbali ili kutoa msaada kwa familia maskini hususan katika sekta ya elimu, afya na uchumi.

Wabunge pia wamejiwekea vipaumbele vinavyodhihirisha uwezo wao wa kupambana na changamoto mamboleo, kielelezo cha matumaini kwa watu wengi kwa siku za usoni. Watu wazima hawana budi kuwajengea vijana matumaini, ili waweze kujisadaka kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Vijana wanapaswa kuondokana na ubinafsi, ili kujenga na kudumisha umoja na mshikamano hata katika kazi za kujitolea, zinazodumisha mafungamano ya kidiplomasia yanayopata chimbuko lake kutoka katika tunu msingi za Kiinjili, yaani upendo kwa Mungu na jirani! Tunu hizi ni msingi katika mchakato wa kupyaisha na kuimarisha huduma katika siasa, majadiliano na tamaduni mbali mbali, haki na ujenzi wa udugu.

Mwishoni Baba Mtakatifu anakaza kusema, changamoto mamboleo, zinawataka watu kufikiri na kutenda katika mwanga na mwelekeo mpya utakaosaidia kukuza na kudumisha amani na utulivu kati ya watu pamoja na kuzingatia hatima ya maisha ya binadamu. Kuliko wakati mwingine wowote katika historia ya maendeleo ya mwanadamu, kanuni maadili na utu wema vinapaswa kupewa msukumo wa pekee, kwani inaonekana kana kwamba, sayansi inahatarisha maendeleo yaliyokwisha kupatikana. Amani ni tunu inayopaswa kuvaliwa njuga na Jumuiya ya Kimataifa.

Wabunge wa Ufalme wa Monaco

 

 

02 February 2019, 14:41