Vatican News
Papa Francisko asema, uekumene wa damu ni ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Papa Francisko asema, uekumene wa damu ni ushuhuda wenye mvuto na mashiko!  (ANSA)

Papa Francisko: Uekumene wa damu ni ushuhuda wenye mvuto!

Vita ni matokeo ya uchu wa mali na madaraka na matokeo yake ni majanga na amani kutoweka. Amani ni matokeo ya utawala wa sheria na haki. Umefika wakati kwa Wakristo huko Mashariki ya Kati kutambuliwa kuwa ni sehemu muhimu sana ya jamii; watu wenye haki sawa na wajibu wanaopaswa kuutekeleza. Maisha ya watakatifu wengi ndani ya Makanisa yamekuwa ni mbegu ya amani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Tume Mchanganyiko ya Kimataifa ya Majadiliano ya Kiekumene kati ya Kanisa Katoliki na Kanisa la Kiorthodox inaendelea kutekeleza dhamana na utume wake kwa kutembea katika umoja na udugu. Wajumbe wa tume hii, Ijumaa, tarehe 1 Februari 2019 wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko ambaye amewashukuru na kuwapongeza kwa kazi kubwa wanayoendelea kuitekeleza na kwamba, kwa sasa wamefikia mkutano wa kumi na sita.

Hili ni jambo ambalo Makanisa yanapaswa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu, kwani mara nyingi inonekana kwamba, hizo formula za kitaalimungu hazina mashindano, bali zinakamilishana, kama walivyofafanua Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Itakumbukwa kwamba, hivi karibuni, Kanisa limeadhimisha kumbu kumbu ya Miaka 60 ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Tafakari kuhusu Sakramenti za Kanisa na hasa uwezekano wa kuadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu kwa pamoja ni sehemu muhimu na kielelezo kuelekea umoja kamili.

Mwaka huu, Tume imejikita katika kutafakari juu ya Sakramenti ya Ndoa ambayo inaonesha kwamba, mwanaume na mwanamke, wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Utimilifu wa mwanaume unajionesha pale anapoishi na mwanamke katika kifungu cha upendo, kwani Mungu ni upendo. Majadiliano haya yanapania kuifaidisha familia ya Mungu na Kanisa ambalo ni Mchumba wa Kristo ambaye wanataka kumpeleka kwa Kristo Yesu bila ila, wala kunyanzi; bila madonda wala migawanyiko, lakini katika uzuri wa umoja mkamilifu.

Baba Mtakatifu katika hotuba yake, ameikumbuka Siku ya Sala ya Kiekumene kwa ajili ya kuombea umoja na amani huko Mashariki ya Kati iliyofanyika mwezi Julai, 2018 huko Bari, Kusini mwa Italia. Matukio kama haya yanaweza kujirudia ili kuimarisha umoja na mshikamano miongoni mwa Wakristo. Baba Mtakatifu anasema, bado anaendelea kusali kwa ajili ya Mashariki ya Kati, ili baada ya kupitia giza la vita, siku moja waweze kuona mapambazuko ya amani, ili kweli Mashariki ya Kati liweze kuwa ni eneo la amani. Haiwezekani kwamba, Mashariki ya Kati liendelee kuwa ni uwanja wa vita na ghasia.

Inabidi watu kukumbuka kwamba, vitani matokeo ya uchu wa mali na madaraka na matokeo yake ni majanga na amani kutoweka. Amani ni matokeo ya utawala wa sheria na haki. Umefika wakati kwa Wakristo huko Mashariki ya Kati kutambuliwa kuwa ni sehemu muhimu sana ya jamii; watu wenye haki sawa na wajibu wanaopaswa kuutekeleza. Maisha ya watakatifu wengi ndani ya Makanisa yamekuwa ni mbegu ya amani. Huko mbinguni waliko anasema Baba Mtakatifu wanaendelea kusindikiza na kuombea mchakato wa umoja wa Wakristo kama sehemu ya utekelezaji wa utashi wa Kristo Yesu mwenyewe ili wote wawe wamoja.

Wakristo wanapaswa kushuhudia umoja unaofumbatwa katika uhalisia wa maisha sanjari na damu ya watakatifu iliyomwagika katika nyakati hizi. Hawa ni waamini wa Makanisa mbali mbali, lakini wanaunganishwa kwa njia ya mateso na imani yao kwa Kristo Yesu na huko mbinguni wanaendelea kushirikishana utukufu huo. Baba Mtakatifu amehitimisha mkutano huu, kwa kusali pamoja na wajumbe hawa Sala ya Baba Yetu.

Tume Majadiliano ya Kiekumene

 

01 February 2019, 17:31