Tafuta

Vatican News
Papa Francisko asema, wokovu ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi mungu na ni kwa ajili ya watu wote! Papa Francisko asema, wokovu ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi mungu na ni kwa ajili ya watu wote!  (Vatican Media)

Papa Francisko: Wokovu wa Mungu ni zawadi kwa watu wote!

Baba Mtakatifu Francisko anasema, huduma ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu ni kwa ajili ya watu wote na wala si kwa wateule wachache! Hawa ni wale ambao wako tayari kutekeleza mapenzi ya Mungu na kuyashuhudia kwa uaminifu mbele ya watu wengine!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Liturujia la Neno la Mungu, Jumapili ya IV ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa inaonesha jinsi ambavyo Kristo Yesu alivyopambana na vikwazo katika utume wake wa kinabii, kiasi cha kukataliwa na watu wa nyumbani kwake, waliomwona kuwa ni Mwana wa Yusufu! Kwa watu hawa, Yesu alijifanya kuwa Masiha wa Bwana, aliyetumwa na Mwenyezi Mungu. Ni watu waliokuwa wanatafuta miujiza na alama na kamwe hawakuwa na imani kwa Mwenyezi Mungu ambaye anataka watu wote waokoke na kupata maisha ya uzima wa milele.

Kwa bahati mbaya, ni watu waliotaka uwepo na utume wa Masiha kwa ajili ya mafao yao binafsi! Ndiyo maana Yesu mwenyewe anawafafanulia madhara yaliyowapata Waisraeli kutokana na ugumu wa mioyo yao kwa kuwapatia mfano wa mjane wa Sarepta ambaye alifanyiwa miujiza na Nabii Eliya pamoja na Naamani mtu wa Shamu aliyetakaswa ukoma wake na Nabii Elisha! Hawa ni watu waliojiaminisha kwa Neno la Mungu na akawaonesha maajabu yake! Hii ni changamoto kwa waamini kufungua nyoyo zao kwa ukarimu kwa kutambua kwamba, wokovu ni kwa ajili ya watu wote!

Hii ni sehemu ya tafakari ya Neno la Mungu iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe 3 Februari 2019, kabla ya kuanza hija yake ya kitume kwenye Umoja wa Nchi za Falme za Kiarabu. Baba Mtakatifu anasema, Kristo Yesu, alipambana na vikwazo mwanzoni mwa utume wake wa hadhara kiasi kwamba, wananchi wa Nazareti wakataka kumfyekelea mbali, ili kumwondoa machoni pao! Kristo Yesu alitambua kabisa kwamba, katika maisha na utume wake, angelipambana na vikwazo, hali ya kukataliwa na hatimaye, kuhukumiwa na kufa Msalabani.

Hii ndiyo sadaka inayotolewa hata leo hii kwa Manabii wa kweli! Lakini pamoja na yote haya, Kristo Yesu hakukata tamaa, alisonga mbele katika maisha na utume wake wa kinabii, huku akiendelea kujiaminisha katika upendo wa Baba yake wa milele! Hata leo hii, wafuasi wa Kristo wanapaswa kujikita katika utume wa kinabii, kwa kuonesha ushujaa na udumifu katika kujibu na kuishi wito wao wa Kikristo. Waamini wanapaswa kuwa ni watu ambao wanasukumwa na nguvu ya Roho Mtakatifu ili kutangaza na kushuhudia matumaini na wokovu kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Jambo la msingi ni imani na wala si miujiza na upendeleo. Huduma ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu ni kwa ajili ya watu wote na wala si kwa wateule wachache! Hawa ni wale ambao wako tayari kutekeleza mapenzi ya Mungu na kuyashuhudia kwa uaminifu mbele ya watu wengine!

Papa: Angelus
03 February 2019, 14:02