Tafuta

Vatican News
Papa Francisko anawataka watawa kujenga utamaduni wa kukutana na Kristo Yesu katika uhalisia wa maisha yao na kwa njia ya huduma kwa watu wa Mungu! Papa Francisko anawataka watawa kujenga utamaduni wa kukutana na Kristo Yesu katika uhalisia wa maisha yao na kwa njia ya huduma kwa watu wa Mungu!  (Vatican Media)

Siku kuu ya Kutolewa Bwana Hekaluni: Wito, Upendo, Huduma!

Papa amewataka watawa kukutana na Kristo Yesu kila siku ya maisha yao; kwa kutambua kwamba, wao ni mawaridi ya maisha na utume wa Kanisa; wanaitwa na kutumwa na Kanisa; wanatakiwa kuwa waaminifu katika uhalisia wa maisha, daima wakijitahidi kupyaisha maisha yao, licha ya changamoto mbali mbali wanazoweza kukutana nazo katika hija ya maisha yao hapa duniani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Katika maadhimisho ya Siku kuu ya Kutolewa Bwana Hekaluni sanjari na maadhimisho ya Siku ya XXIII ya Watawa Duniani, Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, tarehe 2 Februari 2019, ameongoza Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Ibada hii imetanguliwa na maandamano ya mishumaa, kielelezo cha hija ya Bikira Maria na Mtakatifu Yosefu kwenda kumpeleka Kristo Yesu Hekaluni, ili kukutana na watu wake waliokuwa wanamsubiri Masiha katika imani.

Baba Mtakatifu katika mahubiri yake, amewataka watawa kukutana na Kristo Yesu kila siku ya maisha yao; kwa kutambua kwamba, wao ni mawaridi ya maisha na utume wa Kanisa; wanaitwa na kutumwa na Kanisa; wanatakiwa kuwa waaminifu katika uhalisia wa maisha, daima wakijitahidi kupyaisha maisha yao, licha ya changamoto mbali mbali wanazoweza kukutana nazo katika hija ya maisha yao hapa duniani! Baba Mtakatifu anawataka watawa kuhakikisha kwamba, wanajibidisha kukutana na Kristo Yesu katika uhalisia wa hija ya maisha yao, kwa kumpatia kipaumbele cha kwanza. Kwa njia hii, ataweza kuwapatia neema ya kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu.

Watawa wahakikishe kwamba, wanatunza kumbu kumbu hai ya ule upendo wa kwanza walionjeshwa katika maisha yao kwa kukutana na Kristo. Kumbe, maisha yao, daima yawe ni hija ya kukutana na kuambatana na Kristo Yesu! Maandiko Matakatifu yanaonesha jinsi ambavyo Mwenyezi Mungu anakutana na waja wake yaani: vijana na wazee, kama ilivyo hata katika maisha ya kitawa ndani ya Kanisa. Siku kuu ya kutolewa Bwana Hekaluni ni siku ya watu kukutana, mwaliko kwa watawa ni kuomba neema ya kuweza kumtambua Kristo katika maisha ya watu wa Mungu, ili kuwawezesha kukutana na karama ya mashirika yao katika neema ya leo ya Mungu!

Baba Mtakatifu anawakumbusha watawa kwamba, wito wa kwanza ni kadiri ya Sheria ya Mungu kama ilivyotekelezwa na Bikira Maria na Mtakatifu Yosefu. Lakini wito wa pili ni kwa njia ya Roho Mtakatifu unaoshuhudiwa na Mzee Simeoni na Nabii Ana. Miito yote miwili ni kielelezo cha utekelezaji wa Sheria ya Mungu inayopaswa kutekelezwa kila siku ya maisha katika uaminifu na uadilifu, kama ilivyo pia kwa karama mbali mbali za mashirika ya kitawa na kazi za kitume. Kumbe, wito wa Sheria na Wito wa Roho Mtakatifu ni sawa na chanda na pete!

Maisha ya watawa yanafumbatwa katika utii kama ilivyokuwa mwanzoni mwa utume wa Yesu hadharani, alipogeuza maji kuwa divai kwenye harusi ya Kana ya Galilaya, kwa ombi kutoka kwa Bikira Maria. Hii inaonesha kwamba, Mwenyezi Mungu anakutana na waja wake katika uhalisia wa maisha yao ya: Sala, Sakramenti za Kanisa, Tafakari ya Neno la Mungu na Huduma ya upendo hasa kwa maskini na wale wote wanaposukumizwa pembezoni mwa jamii. Utii unapaswa kutekelezwa kwa njia ya upendo kama ilivyokuwa kwa Sr.  Maria Bernadetha wa Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili.

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, huyu ni mtawa ambaye alijisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa wakleri na majandokasisi; kwa hekima na upendo, utii na uaminifu na kamwe kwake upya wa maisha haukua kikwazo. Ndiyo maana Jimbo kuu la Roma limeanzisha mchakato ili aweze kutangazwa kuwa Mtumishi wa Mungu, Mwenyeheri na panapo majaliwa kuandikwa kwenye Orodha ya watakatifu wa Mungu. Mtawa huyu ni mfano bora wa kuigwa na watawa wenzake!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, maisha ya kitawa yanapata chimbuko lake katika maono kama ilivyokuwa kwa Mzee Simeoni aliyeona na kugusa unyenyekevu wa Mungu, kiasi cha kuthubutu kusema, “Nunc dimittis” yaani “Sasa Bwana, wamruhusu mtumishi wako...”! Hapa akaona chemchemi ya maisha mapya, kama ilivyo kwa watawa wanaopaswa kumwona Kristo Yesu, mbele ya macho yao, ili aweze kuwa kweli ni chemchemi ya furaha na matumaini yanayowawezesha watawa kuambata mambo msingi katika maisha yao!

Mwishoni Baba Mtakatifu anasema, kwa njia hii, watawa wanaweza kusimama kidete dhidi ya malimwengu, kwa kuondokana na litania za malalamiko, hali ya kutoridhika katika maisha na kutenda kwa mazoea. Watawa waendelee kupyaisha maisha yao, kwa kukutana na Mungu kati ya watu wake; daima wakiwa na utii unaofumbatwa katika upendo na uaminifu kwa karama za mashirika yao; wawe na maono ya kuweza kukumbatia furaha inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu!

Papa: Watawa
03 February 2019, 10:10