Tafuta

Vatican News
Papa Francisko awataka waamini kudumu katika imani, matumaini na mapendo wakati wa giza na vishawishi katika maisha. Papa Francisko awataka waamini kudumu katika imani, matumaini na mapendo wakati wa giza na vishawishi katika maisha.  (ANSA)

Papa Francisko awataka waamini kudumu katika imani!

Kuna wakati wa mateso, shutuma na dhiki kubwa. Katika hali na mazingira kama haya, Wakristo wanapaswa kujifunza kudumu katika imani, wakitekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yao, ili siku moja waweze kupewa ahadi ya Mungu, kwa kutambua kwamba, wenye haki wataishi milele na Mwenyezi Mungu. Wakristo wajifunze kuwa imara katika majaribu na magumu ya maisha.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

 Maisha ya Mkristo yanafumbatwa katika nyakati za raha na kuchanua kwa ushuhuda wa imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Kuna wakati wa mateso, shutuma na dhiki kubwa. Katika hali na mazingira kama haya, Wakristo wanapaswa kujifunza kudumu katika imani, wakitekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yao, ili siku moja waweze kupewa ahadi ya Mungu, kwa kutambua kwamba, wenye haki wataishi milele na Mwenyezi Mungu. Wakristo wajifunze kuwa imara katika majaribu na magumu ya maisha.

Huu ni ushauri ambao umetolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa, tarehe 1 Februari 2019 kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican. Mahubiri ya Baba Mtakatifu yalijikita kutoka katika Waraka kwa Waebrania, 10: 32-39. Mwandishi wa Waraka huu anatoa wito kwa Wakristo kuwa ni mashujaa katika maisha na utume wao wa Kikristo. Mateso, dhuluma na nyanyaso, kamwe zisiwakatishe tamaa. Hali hii ni kama sehemu ya maisha ya mtu wa kawaida ambaye, kuna wakati anapitia giza na utupu wa maisha; hali ya kukata tamaa; mambo ambayo hata Kristo Yesu mwenyewe aliyapitia katika maisha na utume wake hapa duniani!

Baba Mtakatifu anakza kusema, maisha ya Kikristo ni safari inayosheheni nyakati za furaha na raha mustarehe; kuna nyakati za majonzi, giza na hali ya kukata tamaa; kiasi cha kuona kwamba, maisha hayana maana tena. Hali hii inawezekana kuwa ni mapambano ya maisha ya ndani au mapambano ya maisha ambayo mwamini anakabiliana nayo kutoka nje. Hapa, Mwandishi wa Waraka kwa Waebrania anawataka Wakristo kusimama kidete na kuendelea kudumu katika ushuhuda wa imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake.

Baba Mtakatifu anapenda kukazia mambo makuu mawili yaani: kumbu kumbu ha ona matumaini dhidi ya hali ya kukata tamaa na kutopea katika malimwengu. Waamini wakuze ndani mwao, kumbu kumbu ya mambo mema na matakatifu yatakayowasaidia kupita vipindi vya giza na ugumu wa maisha! Wakumbuke, ile siku walipokutana na Kristo Yesu kwa mara ya kwanza katika maisha yao, akawaonjesha: imani, matumaini na mapendo ya kweli. Waamini wanaweza pia kukumbukia magumu na mahangaiko ya maisha, lakini, hawapaswi kubaki wakiwa wamejikunyata huko, bali kusimama kidete na kusonga mbele ili kuambata ahadi za Mungu katika maisha yao.

Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha mahubiri yake kwa kusema kwamba, katika hija yake ya kitume nchini Lithuania, mwezi Septemba 2018, aliguswa kwa namna ya pekee kabisa na jinsi ambavyo watakatifu, mashuhuda na Wakristo wa kawaida walivyoweza kudumu katika imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Hata leo hii, kuna maelfu ya Wakristo wanaoendelea kunyanyaswa kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake, lakini bado wako imara, kwa sababu ya matumaini na wanaendelea kusonga mbele.

Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha mahubiri yake kwa kusema kwamba, huu ndio ushauri unaotolewa na Mwandishi wa Waraka kwa Waebrania nyakati za madhulumu dhidi ya Kanisa! Hata katika nyakati za giza, dumuni katika imani, matumaini na mapendo. Waamini wanaposhambuliwa na vishawishi vya Shetani, daima wamwangalie Kristo Yesu Msalabani na wakumbuke nyakati za upendo na kwamba, kwa imani na matumaini, wanaweza kusonga mbele pasi na kukata tamaa katika maisha!

Papa: mahubiri

 

01 February 2019, 15:15