Tafuta

Vatican News
Papa Francisko: Boresheni hali ya maisha magerezani ili kuleta matumaini mapya kwa watu! Papa Francisko: Boresheni hali ya maisha magerezani ili kuleta matumaini mapya kwa watu!  (Vatican Media)

Papa: Boresheni magereza ili kuleta matumaini mapya!

Baba Mtakatifu anasema, magereza yanapaswa kuboreshwa zaidi, ili kulinda na kudumisha utu na heshima ya binadamu! Inasikitisha kusikia na kuona kwamba, magereza yanageuka kuwa ni mahali pa vurugu, uvunjifu wa sheria, kanuni na taratibu; mahali ambapo utu na heshima ya binadamu vinasiginwa kwa kiasi kikubwa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kiini cha Alhamisi Kuu katika maisha na utume wa Kanisa ni kumbu kumbu ya kuwekwa kwa Fumbo la Ekaristi Takatifu, Daraja Takatifu pamoja na Huduma ya upendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii! Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi Kuu, tarehe 29 Machi 2018 aliadhimisha Mafumbo ya Kanisa katika Gereza Kuu la “Regina Coeli” lililopo mjini Roma! Viongozi, Askari Magereza, Waganga, Walezi maisha ya kiroho pamoja na watu wa kujitolea, Alhamisi, tarehe 7 Februari 2019 wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican.

Baba Mtakatifu katika hotuba yake, amewashukuru na kuwapongeza kwa kazi kubwa wanayotekeleza kwa ajili ya wafungwa na mahabusu wanaotumikia adhabu zao kwenye Gereza kuu la “Regina Coeli”. Hii ni huduma inayohitaji nguvu ya ndani, udumifu sanjari na kutambua utume maalum ambao wameitwa kuutekeleza kwa dhati! Gereza ni mahali pa watu kutumikia adhabu zao na wakati mwingine ni mahali pa  mateso yanayohitaji kuangaliwa kwa jicho la huruma na mapendo, kwa kukazia utu wa binadamu. Magereza ni mahali ambapo wadau mbali mbali wanaitwa na kutumwa kuganga madonda ya watu waliofanya makosa na sasa wako kifungoni na hawana tena uhuru binafsi.

Baba Mtakatifu anasikitika kusema, kutokana na uhaba wa askari magereza pamoja na magereza kufurika kwa kuwa na idadi kubwa ya watu kuliko uwezo wake, kuna hatari kwa magereza kugeuka kuwa ni mahali ambapo watu wana changanyikiwa na hivyo kupoteza dira na mwelekeo sahihi wa maisha! Hii inatokana na ukweli kwamba, wafanyakazi magerezani wanakabiliwa na msongo mkubwa wa mawazo ambao unathari kubwa katika maisha yao, kiasi hata cha kuwafanya kushindwa kutekeleza vyema dhamana na wajibu huu tete katika maisha ya wafungwa na mahabusu. Hawa ni watu wanaopaswa kuhakikisha usalama wa wafungwa na gereza lenyewe, lakini wakati mwingine, wanajikuta wakiwaachia madonda ya kudumu wafungwa magerezani.

Baba Mtakatifu anasema, magereza yanapaswa kuboreshwa zaidi, ili kulinda na kudumisha utu na heshima ya binadamu! Inasikitisha kusikia na kuona kwamba, magereza yanageuka kuwa ni mahali pa vurugu, uvunjifu wa sheria, kanuni na taratibu; mahali ambapo utu na heshima ya binadamu vinasiginwa kwa kiasi kikubwa! Ikumbukwe kwamba, wafungwa na mahabusu wengi ni watu wa kawaida kabisa; wengi wao hawana hata uhakika wa usalama wa maisha yao, hawana rejea wala familia; hawana uwezo wala nguvu ya kiuchumi kuweza kusimamia na kupigania haki zao msingi. Hawa ni watu ambao wametelekezwa na kwa jamii wanaonekana si mali kitu na hata wakati mwingine ni mzigo mzito usiobebeka hata kidogo “hata kama atabebeshwa Mnyamwezi” kama wanavyosema Waswahili!

Baba Mtakatifu anafurahi kusema kwamba, uzoefu na mang’amuzi yanaonesha kwamba, gereza linaweza kuwa ni mahali pa msaada mkubwa kwa wadau mbali mbali; mahali ambapo panaweza kugeuka kuwa ni chemchemi ya mwanzo mpya wa maisha; mahali ambapo wale waliodhani kwamba wamekufa na kusahaulika mbele ya uso wa dunia, wanaweza kufufuka tena na kutoka kifua mbele kutangaza matendo makuu ya Mungu. Gereza ni mahali ambapo wafungwa wanaweza kufanya mageuzi makubwa katika maisha yao. Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, yote haya yanawezekana kwa njia ya elimu na stadi za maisha; kwa uwepo wa karibu wa walezi wa maisha ya kiroho wanaotekeleza dhamana na wajibu wao kama alivyofanya Msamaria mwema.

Upendo na ukaribu kwa wafungwa unapaswa kupata chimbuko lake kutoka kwa Kristo Yesu. Hali hii itawapatia wafungwa imani na matumaini kwamba, wanapendwa na kuthaminiwa! Kazi hii inapaswa kutekelezwa kwa umoja, upendo na utulivu wa ndani unaooneshwa na kushuhudiwa na wadau mbali mbali, ili kuwasaidia wawe walioteleza na kuanguka katika hatia kwa makosa mbali mbali, waweze kusimama tena na kusonga mbele kwa imani na matumaini makubwa. Baba Mtakatifu amehitimisha hotuba yake, kwa kuwahakikishia wadau wote kwamba, anawasindikiza kwa sala na sadaka yake, ili kweli magereza yawe ni mahali pa kutumikia adhabu na mateso ya mwanadamu; lakini pia magereza yawe ni maabara ya utu, heshima na matumaini mapya!

Papa: Magereza
07 February 2019, 14:38