Tafuta

Papa Francisko kwa Shirika la Fatebenefratelli: Mkazo: Mang'amuzi, ukaribu na ukarimu; pamoja na utume shirikishi Papa Francisko kwa Shirika la Fatebenefratelli: Mkazo: Mang'amuzi, ukaribu na ukarimu; pamoja na utume shirikishi 

Mang'amuzi, ukarimu na utume shirikishi ni muhimu kwa watawa!

Papa Francisko asema: mambo makuu matatu yapewe kipaumbele cha kwanza: Mang’amuzi; ukaribu na ukarimu pamoja na utume shirikishi! Huu ni ushauri ambao umetolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa, tarehe 1Februari 2019 alipokutana na kuzungumza na wajumbe wa mkutano mkuu wa Shirika la Wahudumu wa Hospitali la Mtakatifu Yohane wa Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Katika maadhimisho ya Mkutano Mkuu wa 69 wa Shirika la Wahudumu wa Hospitali la Mtakatifu Yohane wa Mungu, maarufu kama “Fatebenefratelli mambo makuu matatu yanapewa kipaumbele cha kwanza: Mang’amuzi; ukaribu na ukarimu pamoja na utume shirikishi! Huu ni ushauri ambao umetolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa, tarehe 1Februari 2019 alipokutana na kuzungumza na wajumbe wa mkutano mkuu wa Shirika la Wahudumu wa Hospitali la Mtakatifu Yohane wa Mungu.

Mang’amuzi ni msingi wa utume wa Kanisa na maisha ya kuwekwa wakfu, kwa kutafakari yaliyopita kwa moyo wa shukrani, kuyaishi ya sasa kwa moyo wa hamasa na kuyakumbatia ya mbeleni kwa moyo wa matumaini. Haya ni kati ya mambo makuu yaliyopewa kipaumbele cha kwanza wakati wa maadhimisho wa Mwaka wa Watawa Duniani. Hii ni sehemu ya mchakato wa kutakasa: historia, karama na kujikita katika mambo msingi ya maisha na utume wa Shirika. Lengo ni kuondokana na kishawishi cha kutekeleza utume kwa mazoea pasi na upendo wa dhati kwa mateso na mahangaiko ya Kristo Yesu miongoni mwa waja wake.

Kwa njia ya mang’amuzi, watawa hawa ambao wamejikita katika huduma kwa wagonjwa hospitalini wataweza kupambana na changamoto mamboleo kwa ari na moyo mkuu kwa sababu mang’amuzi yao yamekita mizizi katika historia! Maadhimisho ya Mkutano mkuu iwe ni fursa ya kukuza na kudumisha majadiliano, mang’amuzi kwa kumsikiliza Roho Mtakatifu, wanashirika na wadau wengine katika huduma kwa wagonjwa. Baba Mtakatifu anasema, hii ni changamoto ya kujadili, kupanga, kuamua na kutekeleza maisha na utume wa Shirika, daima wakiendelea kuwasikiliza hata wagonjwa na wale wote wanaohitaji msaada wao kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Yohane wa Mungu, aliyekuwa na uchaji wa Mungu, huruma na upendo kwa wagonjwa!

Ukaribu na ukarimu ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wao katika huduma kwa wagonjwa. Ni mambo yanayotoa maana ya utume wao; chachu ya tasaufi na sehemu ya maboresho ya maisha ya kidugu katika jumuiya, kielelezo makini cha upendo kwa Kristo Yesu. Kwa njia ya ushuhuda wa huduma ya upendo, wanashirika hawa kama familia wanaweza kujisadaka wakati wowote kwa ajili ya huduma kwa ulimwengu ambao umejeruhiwa na kuathirika kwa magonjwa.

Ulimwengu mamboleo una alama nyingi za kifo ambazo zinapaswa kuangaliwa kwa jicho la huruma na upendo anasema Baba Mtakatifu. Wao kama wahudumu wajitahidi kuiga mfano wa Msamaria mwema kwa kuwaganga wagonjwa kwa mafuta ya faraja na divai ya matumaini; mambo msingi katika kutambua karama ya Shirika lao na sehemu ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu kwa njia ya huduma kwa maskini na wagonjwa. Msamaria mwema alipomwona, akamhurumia, akakaribia, akamfunga jeraha zake, akazitia mafuta na divai: Huu ni mwelekeo wa kiutu na maisha ya kiroho yanayogusa maskini na wagonjwa na pamoja na kuwasaidia wahudumu wao kama watawa kupyaisha maisha yao katika huruma na upendo wa Mungu.

Baba Mtakatifu anawataka wanashirika hawa kuwa na sehemu ambamo, maskini na wale wote wanaoskumizwa pembezoni mwa jamii wanaweza kupata huduma. Waendelee kutengeneza mitandao ya wasamaria wema kwa wagonjwa maskini, kwa kuhakikisha kwamba, wanaendelea kuwa ni Jumuiya ambayo iko wazi, tayari kujikita katika utandawazi wa mshikamano wa upendo na huruma. Utume shirikishi ni changamoto pevu kutokana na uhaba wa miito ya kitawa na ongezeko kubwa la watawa wenye umri mkubwa. Katika hali na mazingira kama haya, kuna haja ya kukuza ari na moyo wa kimisionari kwa kuwashirikisha waamini katika kutoa huduma ya faraja na upendo, hata kama wakati mwingine, utume wao unaweza kuwa hatarini.

Mwishoni wa hotuba yake, Baba Mtakatifu amekazia umuhimu wa malezi na majiundo makini kwa wale wanaotaka kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa Kristo na Kanisa lake; wajitahidi kushirikisha karama yao kwa waamini walei, ili kwa pamoja waweze kuwaonjesha wagonjwa: huruma na upendo wa Kristo Yesu. Wajitahidi kutoka katika ubinafsi wao na kujiunga katika msafara wa mshikamano wa huduma na upendo!

Fatebenefratelli
01 February 2019, 17:47