Tafuta

Vatican News
Papa Francisko asema, hija yake ya kitume Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu ilikuwa fupi sana, lakini muhimu kwa maisha na utume wa Kanisa katika majadiliano ya kidini! Papa Francisko asema, hija yake ya kitume Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu ilikuwa fupi sana, lakini muhimu kwa maisha na utume wa Kanisa katika majadiliano ya kidini!  (ANSA)

Umoja wa Falme za Kiarabu: Papa: Safari fupi, muhimu sana!

Baba Mtakatifu Francisko, kwa namna ya pekee kabisa amemshukuru na kumpongeza Mfalme mrithi Sheikh Mohammed bin Zayed Al Nahyan pamoja na wananchi wake, kwa ukarimu na mapokezi makubwa waliyomkirimia wakati alipokuwa nchini mwao. Amewahakikishia kwamba, ataendelea kuwakumbuka katika sala na sadaka yake!

Na Padre Richard A. Mjigwa, - Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, muujiza wa aina yake, Jumanne, tarehe 5 Februari 2019 kwenye Uwanja wa Michezo wa Zayed, Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu amesema, waamini wanapaswa kutambua kwamba, wana heri kwa sababu wao ni watoto wateule wa Mungu. Heri za Mlimani ni chemchemi ya furaha ya upendo aminifu wa Mungu inayobubujikia maisha ya waamini! Hii ni furaha endelevu ambayo hakuna mtu wala mazingira yanaweza kuwapokonya wateule wa Mungu.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Hati ya Udugu wa Kibinadamu, iliyotiwa mkwaju kati yake na Dr. Ahmad Al-Tayyib, Imam Mkuu wa Msikiti wa Al- Azhar, ulioko Kairo, nchini Misri, Jumatatu, tarehe 4 Februari 2019 ni mwaliko kwa waamini wa dini mbali mbali duniani, kuungana na kushikamana, ili kufanya kazi katika umoja na udugu, ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Haya ni matukio makuu mawili ambayo yameacha chapa ya kudumu katika akili na nyoyo za watu ndani na nje ya Umoja wa Falme za Kiarabu.

Baba Mtakatifu, Jumanne, tarehe 5 Februari 2019 aliagana na wenyeji wake waliokuwa wanaongozwa na Mfalme mrithi  Sheikh Mohammed bin Zayed Al Nahyan. Baba Mtakatifu alikuwa amefuatana na viongozi wakuu kutoka Vatican waliokuwa kwenye msafara wake, wakiongozwa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican pamoja na viongozi mahalia, walioshiriki kikamilifu katika maandalizi ya hija hii ya 27 ya Baba Mtakatifu Francisko kimataifa! Baba Mtakatifu akiwa njiani kurejea mjini Vatican akitokea Abu Dhambi, Umoja wa Falme za Kiarabu amewatumia wakuu wa nchi salam na matashi mema alipokuwa akipita juu ya anga la nchi zao. Marais hawa ni wale wa: Umoja wa Falme za Kiarabu, Bahrain, Saudi Arabia, Misri, Ugiriki, Malta, pamoja na Italia.

Baba Mtakatifu kwa namna ya pekee kabisa amemshukuru na kumpongeza Mfalme mrithi  Sheikh Mohammed bin Zayed Al Nahyan pamoja na wananchi wake, kwa ukarimu na mapokezi makubwa waliyomkirimia wakati alipokuwa nchini mwao. Amewahakikishia kwamba, ataendelea kuwakumbuka katika sala na sadaka yake! Kwa viongozi wengine wa Kimataifa amewatakia: furaha, amani, baraka na nguvu ya kusonga mbele katika mchakato wa maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu.

Baba Mtakatifu katika salam na matashi mema kwa Rais Sergio Mattarella wa Italia amemwambia kwamba, anarejea kutoka Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu kama hujaji wa amani na udugu kati ya watu wa Mataifa. Anasema, huko Abu Dhabi amepata nafasi ya kukutana na kuzungumza na viongozi mbali mbali wa kidini, wakishuhudia dhamana na wajibu fungamani wa kusimama kidete katika hija ya amani na mshikamano. Mwishoni, Baba Mtakatifu anamtakia heri na baraka Rais Sergio Mattarella pamoja na familia yote ya Mungu nchini Italia. Baba Mtakatifu baada ya kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Roma- Ciampino, majira ya 11: 00 za jioni, alikwenda moja kwa moja kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria mkuu, Jimbo kuu la Roma, ili kusali na kushukuru kwa ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Afya ya Warumi.

Papa: Safari Kurejea
06 February 2019, 10:35