Vatican News
Papa Francisko: Heri za Mlimani ni dira na mwongozo wa maisha ya Kikristo! Papa Francisko: Heri za Mlimani ni dira na mwongozo wa maisha ya Kikristo!  (ANSA)

Umoja wa Falme za Kiarabu: Heri za Mlimani: Mwongozo wa maisha!

Baba Mtakatifu Francisko anasema, waamini wanapaswa kutambua kwamba, wana heri kwa sababu wao ni watoto wateule wa Mungu. Heri za Mlimani ni chemchemi ya furaha ya upendo aminifu wa Mungu inayobubujikia maisha ya waamini! Hii ni furaha endelevu ambayo hakuna mtu wala mazingira yanaweza kuwapokonya wateule wa Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Amani, ustawi, maendeleo pamoja na mafao ya wengi yanawezekana kwa kutambua kuwa, tofauti msingi ni amana na utajiri na kamwe si fursa ya kuwagawa na kuwasambaratisha watu. Baba Mtakatifu anasema imani kwa Mwenyezi Mungu ni sumaku inayowaunganisha waamini wa dini mbali mbali! Kwa njia ya tofauti msingi katika imani, waamini wanaweza kujenga na kudumisha udugu wa kibinadamu, kauli mbiu ambayo imeongoza Mkutano wa Kimataifa wa majadiliano ya kidini huko Abu Dhabi! “Nifanye chombo cha amani” ndiyo kauli mbiu iliyoongoza hija ya 27 ya Baba Mtakatifu Francisko kimataifa.

Maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu iliyoendeshwa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya kitume huko Abu Dhabi, kwenye Umoja wa Falme za Kiarabu,  Jumanne, tarehe 5 Februari 2019 kwenye Uwanja wa Michezo wa Zayed  ni kati ya zawadi kubwa ambazo Baba Mtakatifu ametoa kwa ajili ya Wakristo kwenye Umoja wa Falme za Kiarabu. Hili ni Kanisa linaloundwa na wahamiaji pamoja na wakimbizi kutoka sehemu mbali mbali za dunia, watu wenye chapa ya pekee katika maisha na utume wa Baba Mtakatifu Francisko. Bahari ya watu imejitokeza barabarani kumpokea na kumshangilia Baba Mtakatifu wakati akielekea kwenye maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu!

Wakati wa mahubiri yake, Baba Mtakatifu amejikita zaidi katika Heri za Mlimani, muhtasari wa mafundisho makuu yaliyotolewa na Kristo Yesu kwa wafuasi wake. Huu ni mwaliko wa kusikiliza kwa makini na kumwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha. Waamini wanapaswa kutambua kwamba, wana heri kwa sababu wao ni watoto wateule wa Mungu. Heri za Mlimani ni chemchemi ya furaha ya upendo aminifu wa Mungu inayobubujikia maisha ya waamini! Hii ni furaha endelevu ambayo hakuna mtu wala mazingira yanaweza kuwapokonya wateule wa Mungu.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, ujumbe ambao amekuja kuwapatia ni Heri za Mlimani zinazofumbatwa katika: Umaskini wa roho, huzuni, upole, njaa na kiu ya haki, rehema na moyo safi, upatanishi pamoja na uvumilivu hata pale wanaposhutumiwa na kuhudhiwa kwa uwongo. Hivi ndivyo alivyoishi hata Kristo Yesu, maskini wa mambo ya dunia, lakini tajiri wa huruma na upendo wa Mungu, aliyejisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuwatakasa watu. Kristo alikuja ili kuhudumia na wala si kuhudumiwa, akajinyenyekesha kiasi hata cha kuhukumiwa afe Msalabani.

Kwa njia hii, Kristo Yesu amewakirimia walimwengu upendo na huruma ya Mungu isiyokuwa na kifani, kiasi hata cha kushinda kifo, dhambi, mauti, woga na fahari za dunia. Hiki ni kielelezo cha upendo wa Mungu, mwaliko kwa waamini kumwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kuwakirimia neema ya kumfuasa Kristo na kuiga upendo wake unaosimikwa katika unyenyekevu, kiini cha upendo kwa Mungu na jirani. Baba Mtakatifu amechukua fursa hii kuwashukuru Wakristo kwenye Umoja wa Falme za Kiarabu kwa ushuhuda wanaoutoa kwa ajili ya kumwilisha tunu msingi za Kiinjili katika uhalisia wa maisha yao.

Waamini hawa katika tofauti zao msingi za mahali wanapotoka, lugha na madhehebu wanayotumia katika Ibada, lakini wote kwa njia ya Roho Mtakatifu wanajisikia kuwa wamoja katika imani inayoshuhudiwa katika maisha na kulijenga Kanisa la Kristo! Huu ni ushuhuda unaoendelea kumjenga na kumwimarisha Askofu Paul Hinder, Msimamizi wa Kitume huko Umoja wa Falme za Kiarabu, Oman na Yemen. Kwa hakika waamini wamekuwa wachungaji wema katika maisha na utume wake!

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, si wakati wote Wakristo wamekuwa ni vyombo na mashuhuda wa furaha inayobubujika kutoka katika Heri za Mlimani. Kuna kipindi wamekumbana na dhuluma, nyanyaso, mateso na hata kifo! Hii ndiyo hali halisi hata kwa waamini hawa ambao wengi wao wako mbali na makwao; wakati mwingine wanakosa upendo kutoka kwa familia na ndugu zao wa karibu na hata kukosa matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi. Jambo la msingi kukumbuka ni kwamba, Mwenyezi Mungu daima ni mwaminifu na kamwe hawezi kuwaacha waja wake.

Mtakatifu Anthony katika maisha na utume wake aliyacha yote na kwenda “kujichimbia” Jangwani ili kuendeleza mapambano ya maisha ya kiroho, lakini hata huko nako akapambana sana na vishawishi, “daima alikuwa anakumbuka historia ya maisha yake ya nyuma” kiasi cha kudhani kwamba, Mwenyezi Mungu amemwacha na kumtelekeza kama “gari bovu”! Lakini, Kristo Yesu alimhakikishia Mtakatifu Anthoni kwamba, daima amekuwa pamoja naye katika hija ya maisha. Katika kipindi cha mashaka na taabu nyingi, waamini wanaweza kudhani kwamba, Mwenyezi Mungu amewasahau, lakini daima yuko nao bega kwa bega! Jambo la msingi kwa waamini ni kuendelea kusonga mbele kwa sababu Mwenyezi Mungu kama ilivyokuwa kwenye Agano la Kale anataka kufanya njia jangwani.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Kristo Yesu ameliachia Kanisa urithi mkubwa wa ushuhuda wa maisha na utume wake na kwamba, Heri za Mlimani ni mwongozo wa maisha ya Kikristo, yanayopania kumuiga Kristo Yesu hatua kwa hatua katika historia ya maisha. Jambo la muhimu kwa waamini ni kuhakikisha kwamba, wanajitakasa, wanakuwa wanyenyekevu, mashuhuda na vyombo vya amani, licha ya changamoto mbali mbali wanazokumbana nazo katika maisha! Waamini wawe na huruma na daima wajitahidi kuungana na Mwenyezi Mungu, kwa kuhakikisha kwamba, wanashuhudia imani ya kama kielelezo makini cha utakatifu wa maisha.

Heri za Mlimani ziwasaidie waamini kupambana na changamoto mamboleo, ili hatimaye, waweze kuyatakatifuza malimwengu. Ili kutekeleza dhamana na utume huu, waamini wanapaswa kushikamana kwa dhati na Kristo Yesu, tayari kutenda mema kwa jirani na kwamba, jumuiya zao ziwe ni chemchemi ya amani. Waamini wanatakiwa kuwa wapole, ili waweze kuirithi nchi, wawe kweli ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa jirani zao, kwa njia ya imani kama alivyofanya Mtakatifu Francisko wa Assisi. Upole utawawezesha waamini kuwa ni vyombo vya uwepo endelevu wa Mungu kati ya watu wake, ili waweze kuzaa matunda yanayokusudiwa.

Baba Mtakatifu amewataka waamini kuwa wapatanishi, kwa kutafuta na kudumisha amani inayopaswa kukita mizizi yake ndani ya jumuiya zao. Wawe waaminifu kwa Neno la Mungu na mashuhuda wa upendo wa Mungu na udugu kati yao. Kwa njia hii wataweza kuzaa matunda ya amani, umoja, upendo na mshikamano wa kweli! Yesu anawaita kuwa wenyeheri, anawakirimia neema ya kusonga mbele, bila ya kukata tamaa, huku wakiendelea kukua na kukomaa katika upendo kati yao na kati ya wale wote wanaowazunguka!

Papa: Misa Abu Dhabi
05 February 2019, 11:30