Cerca

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko anawashukuru na kuwapongeza wale wote waliojisadaka kufanikisha hija yake ya 27 Kimataifa huko Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu! Baba Mtakatifu Francisko anawashukuru na kuwapongeza wale wote waliojisadaka kufanikisha hija yake ya 27 Kimataifa huko Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu! 

Umoja wa Falme za Kiarabu! Shukrani kutoka kwa Papa Francisko!

Hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko huko Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu ni tukio ambalo limeacha chapa kubwa katika maisha ya waamini ndani na nje ya Umoja wa Falme za Kiarabu! Kwa mara ya kwanza, katika Umoja wa Falme za Kiarabu, Khalifa wa Mtakatifu Petro ameadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu hadharani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Baba Mtakatifu Francisko kwenye Uwanja wa Michezo wa Zayed huko Abu Dhabi, 2019, imeshuhudiwa na mamilioni ya watu kwa njia ya vyombo vya mawasiliano ya jamii. Hili limekuwa ni tukio ambalo limeacha chapa kubwa katika maisha ya waamini ndani na nje ya Umoja wa Falme za Kiarabu! Kwa mara ya kwanza, katika Umoja wa Falme za Kiarabu, Khalifa wa Mtakatifu Petro ameadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu hadharani. Uhuru wa kuabudu ulianza kuzaa matunda kunako mwaka 1960 wakati Kanisa la kwanza lilipojengwa na hatimaye, kutabarukiwa na baadaye kufuatiwa na ujenzi wa shule za kikristo.

Baba Mtakatifu kabla ya kutoa baraka zake za kitume, ametumia fursa hii kuwashukuru waamini kutoka katika madhehebu mbali mbali ya Kikristo walioshiriki kwa wingi. Kwa namna ya pekee kabisa, amemshukuru Askofu Paul Hinder aliyechakarika usiku na mchana katika maandalizi na hatimaye, maadhimisho haya! Baba Mtakatifu amewashukuru na kuwapongeza Viongozi wakuu wa Makanisa, wakleri, watawa na waamini walei wanaoendelea kujisadaka katika huduma kwa maskini na ujenzi wa Kanisa la Yesu.

Baba Mtakatifu anahitimisha shukrani zake kwa kuwasalimia watoto wa Zayed katika nyumba ya Zayed; kwenye nchi ambayo imejaa utajiri wa maendeleo na amani; nchi yenye kung’ara kwa mwanga wa jua na utulivu; nchi ambayo watu wanaishi kwa maridhiano na hatimaye kuweza kukutana. Mwishoni, amewaombea ulinzi na tunza kutoka kwa Bikira Maria, ili waendelee kuwa ni vyombo na mashuhuda wa furaha ya Injili na upendo!

Papa: Shukrani

 

 

05 February 2019, 13:33