Tafuta

Vatican News
Hati ya udugu wa kibinadamu ni matunda ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican kuhusu Majadiliano ya kidini. Hati ya udugu wa kibinadamu ni matunda ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican kuhusu Majadiliano ya kidini.  (ANSA)

Hati ya Udugu wa Kibinadamu: Majadiliano ya Kidini: Mtaguso wa Vatican!

Papa Francisko anasema, Hati ya Udugu wa Kibinadamu ni utekelezaji wa Mafundisho ya Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, mchakato ambao unaendelea kukua na kukomaa, iko siku utazaa matunda yanayokusudiwa. Baadhi ya viongozi wa dini ya Kiislam wanasema, Hati ya Udugu wa Kibinadamu itaanza kufundishwa kwenye Chuo Kikuu cha Kiislam cha Al-Azhar, huko Kairo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko akiwa njiani kurejea kutoka Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu, Jumanne, tarehe 5 Februari 2019, amepata tena nafasi ya kuteta na waandishi wa habari waliokuwa kwenye msafara wake. Amegusia kuhusu: Hati ya Udugu wa Kibinadamu kama nguzo ya majadiliano ya kidini, ili kudumisha amani duniani na kama sehemu ya utekelezaji wa maamuzi ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Kuhusu mpasuko wa kisiasa nchini Venezuela, Baba Mtakatifu amekiri kupokea Barua kutoka Rais Nicolas Maduro, lakini bado hajaisoma. Amejadili kwa kina umuhimu wa kudumisha majadiliano ya kidini kati ya waamini wa dini mbali mbali duniani pamoja na kashfa ya nyanyaso za wakleri dhidi ya watawa wa kike!

Baba Mtakatifu anakiri kushangazwa sana na mji wa Abu Dhabi jinsi ulivyojengwa, mazingira safi na yenye kuvutia, fahari kubwa inayoweza kupatikana Jangwani. Hii ni nchi ambayo ineonesha ukaribu kwa kuwapokea wageni kutoka sehemu mbali mbali za dunia! Ni nchi ambayo inaangalia mbele zaidi, kwa kukazia elimu bora na makini kwa watoto; ustawi na maendeleo ya watu wake. Kwa sasa wamejiwekea mkakati wa kuchota maji kutoka baharini, ili yaweze kuondolewa chumvi na kuanza kutumika kama maji safi na salama kwa matumizi ya binadamu. Umoja wa Falme za Kiarabu unajiandaa pia kwa mabadiliko ya matumizi ya nishati, ili kupata nishati mbadala wa petroli.

Wananchi wa Umoja wa Falme za Kiarabu wanaendelea kujipambanua kuwa ni watu wanaotaka kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini, katika ukweli na uwazi; kwa kuheshimu na kudumisha haki, amani na maridhiano, ingawa bado kuna vita katika nchi jirani. Baba Mtakatifu anasema, ameguswa sana na tukio lililomwezesha kukutana na kuzungumza na Wazee wa Baraza Kuu la Waislam, watu wenye taaluma, uzoefu na mang’amuzi mbali mbali ya maisha. Ni watu kutoka katika tamaduni, lugha na jamaa, hali inayoonesha pia umoja, mshikamano na uwazi. Wazee mbali mbali walipata nafasi ya kushirikisha mang’amuzi yao na wote wamekazia hekima, uaminifu, urafiki na udugu kati ya watu, ili kujenga na kudumisha haki, amani na maridhiano.

Umoja wa Falme za Kiarabu unaendelea kujielekeza katika matumizi salama ya mitandao ya kijamii, kwa kuwalinda watoto wadogo dhidi ya nyanyaso zinazoweza kujitokeza pamoja na usambazaji wa picha za ngono, ambazo kwa sasa zimegeuzwa kuwa ni kiwanda cha “kufyatulia fedha” kwa wajanja wachache, wanaotumia nyanyaso za kijinsia kwa ajili ya mafao yao binafsi. Pengine, hata wao wanayo mapungufu yao, lakini Baba Mtakatifu anasema, anawashukuru kwa mapokezi makubwa na ukarimu waliomwonjesha.

Hati ya Udugu wa Kibinadamu kama nguzo ya majadiliano ya kidini, ili kudumisha amani duniani na kama sehemu ya utekelezaji wa maamuzi ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Hii ni hati ambayo imeandaliwa kwa sala na tafakari ya kina, ili kuweza kudhibiti: vita, uharibifu unaosababishwa na vitendo vya kigaidi, chuki na uhasama kati ya watu! Lengo ni kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano, chachu muhimu sana ya ustawi na maendeleo fungamani ya binadamu! Hakuna maendeleo ya kweli pasi na amani duniani. Hii ni hati inayopata chimbuko katika misingi ya imani kwa Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo! Imefanyiwa kazi kwa muda wa mwaka mzima na baada ya sala na tafakari ya kina, viongozi wakuu wameridhia na sasa ni dira na mwongozo wa majadiliano ya kidini.

Baba Mtakatifu anakiri kwamba, hii imekuwa ni hija fupi sana, lakini yenye kubeba utajiri mkubwa katika maisha na utume wa Kanisa mintarafu majadiliano ya kidini, uhuru wa kuabudu, haki na amani duniani. Umoja wa Falme za Kiarabu umefanya mambo makubwa kwa kutambua dhamana na mchango wa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Walitaka kuhakikisha kwamba, anajisikia kuwa yuko nyumbani kati pamoja na ndugu zake! Yote haya yamekuwa ni msingi wa kuendeleza mpango mkakati wa amani hasa nchini Yemen pamoja na Siria.

Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, anashutumiwa na baadhi ya watu: ndani na nje ya Kanisa kuhusu mwelekeo wake wa upendeleo kwa waamini wa dini ya Kiislam. Hati ya Udugu wa Kibinadamu inatajirishwa na Mafundisho makuu ya Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican kuhusu majadiliano ya kidini. Ni hati ambayo imepitiwa na viongozi wakuu wa Sekretarieti kuu ya Vatican, ikafanyiwa marekebisho na hatimaye, kuridhika kwamba, ni hati ambayo imeandikwa kwa mwanga wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican.

Hali kadhalika, kwa waamini wa dini ya Kiislam, kuna wale wenye misimamo mikali ya kidini na wale wanaoweza kuangalia mambo katika ukweli na uwazi; kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Hati hii ni utekelezaji wa Mafundisho ya Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, mchakato ambao unaendelea kukua na kukomaa, iko siku utazaa matunda yanayokusudiwa. Baadhi ya viongozi wa dini ya Kiislam wanasema, Hati ya Udugu wa Kibinadamu itaanza kufundishwa kwenye Chuo Kikuu cha Kiislam cha Al-Azhar, huko Kairo, Misri. Watu waelimishwe na wala wasilazimishwe, kwani elimu ni mwanga unaomwondolea mtu giza la ufahamu katika maisha!

Baba Mtakatifu Francisko amekubali mwaliko uliotolewa kwake na Mfalme Mohammed VI pamoja na Maaskofu Katoliki nchini Morocco, kutembelea nchi yao kuanzia tarehe 30-31 Machi 2019. Hija hii ya kitume inaongozwa na kauli mbiu “Mhudumu wa matumaini. Papa Francisko anasema, hija hizi za kitume ni mbinu mkakati wa kutaka kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini katika ukweli na uwazi; na kama fursa ya waamini wa dini hizi mbili kuweza kufahamiana, hasa wakati huu wa kumbu kumbu ya miaka mia nane, tangu Mtakatifu Francisko wa Assisi alipokutana na Sultani Al-Malik al Kamil.

Baba Mtakatifu anasema, alitamani sana kwenda, Marrakesh, Morocco kushiriki katika mkutano wa Kimataifa kuhusu Mkataba wa Usalama wa Wahamiaji 2018, ikashindikana kutokana na protokali na badala yake, Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican akamwakilisha. Ziara yake nchini Morocco inafuata nyayo za Mtakatifu Yohane Paulo II. Tayari Baba Mtakatifu Francisko anasema, amepokea mwaliko kutoka katika nchi kadhaa za Kiislam, zote hizi ni hapo mwakani, Mwenyezi Mungu akipenda!

Baba Mtakatifu Francisko anampongeza Mtakatifu Yohane Paulo II ambaye kunako mwaka 1978 alisaidia kuzima vita kati ya Argentina na Chile kwa kutumia diplomasia ya Vatican. Rais Nicolas Maduro amemwandikia Barua Baba Mtakatifu Francisko akimwomba, kusaidia kusuluisha mpasuko wa kisiasa nchini Venezuela. Baba Mtakatifu anakiri kwamba, alikuwa bado haijaisoma! Lakini, ili diplomasia iweze kufanya kazi yake, kuna haja ya pande zote mbili kuonesha utashi wa kushiriki! Vatican imejitahidi sana bila mafanikio! Baba Mtakatifu anasema, bado Vatican haijakata tamaa!

Dr. Ahmad Al-Tayyib, Imam Mkuu wa Msikiti wa Al- Azhar, ulioko Kairo, nchini Misri, katika hotuba yake amegusia kuhusu “Islamphobia” yaani “woga dhidi ya dini ya Kiislam”. Baba Mtakatifu anasema, Hati ya Udugu wa Kibinadamu inajikita zaidi katika umoja unaofumbatwa katika tofauti msingi pamoja na umuhimu wa kukuza na kudumisha urafiki. Hati inapinga kwa nguvu zote vitendo vyote vya kigaidi na kufuru ya kutumia jina la Mwenyezi Mungu kwa ajili ya ustawi na mafao ya watu binafsi.Uhuru wa kidini na uhuru wa kuabudu vimetiliwa mkazo.

Watu wanapaswa kuongozwa na dhamiri nyofu ili kutenda mema. Baba Mtakatifu anasema, kwa mara ya kwanza Wakristo huko Umoja wa Falme za Kiarabu wameweza kuadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu hadharani. Hii ni hatua kubwa kuelekea katika uhuru wa kuabudu na uhuru wa kidini. Baba Mtakatifu anasema, Jamii inapaswa kuwaheshimu na kuwathamini wanawake ambao wana mchango mkubwa katika maisha na utume wa Kanisa na jamii katika ujumla wake. Bado sehemu mbali mbali za dunia, zinatawaliwa na mfumo dume, unaowakandamiza na kuwanyanyasa wanawake. Hata ndani ya Kanisa, kuna baadhi ya viongozi ambao wamewanyanyasa watawa!

Lakini, tangu wakati wa Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI, Kanisa limeendelea kusimama kidete ili kuhakikisha kwamba, watawa wa kike wanalindwa na  kuheshimiwa. Kuna kesi ambazo zinaendelea kufanyiwa kazi na Sekretarieti kuu ya Vatican, zikikamilika uamuzi utatolewa haki kutendeka.Kwa maelezo haya Baba Mtakatifu, akahitimisha kipindi cha maswali na majibu kutoka kwa waandishi waliokuwa kwenye msafara wake wa hija yake ya 27 kimataifa kutoka Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu.

Papa na Waandishi wa habari

 

 

 

06 February 2019, 10:51