Hija ya kitume ya Papa Francisko kwenye Umoja wa Falme za Kiatabu unapania kujenga na kuimarisha madaraja ya udugu wa kibinadamu! Hija ya kitume ya Papa Francisko kwenye Umoja wa Falme za Kiatabu unapania kujenga na kuimarisha madaraja ya udugu wa kibinadamu! 

Papa Francisko Umoja wa Falme za Kiarabu: kuimarisha udugu!

Mwenyezi Mungu ni asili ya: uhai, wema na utakatifu na kamwe hawezi kuwa ni chanzo cha vita, chuki na uhasama! Jina la Mungu ni takatifu na ni chemchemi ya furaha na amani ya kweli. Leo hii dunia inawahitaji wajenzi wa amani na wala si “wachochezi wa vita na ghasia” dunia inawahitaji watu jasiri wanaoweza kuthubutu kuzima moto wa chuki na uhasama na wala si watu wa vita!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, kuanzia tarehe 3 hadi 5 Februari 2019, anafanya hija ya kitume ya ishirini na saba kimataifa huko Abu Dhabi, kwenye Umoja wa Falme za Kiarabu, ili kuhudhuria Mkutano wa Kimataifa wa majadiliano ya kidini unaoongozwa na kauli mbiu "Udugu wa kibinadamu”. Baba Mtakatifu katika hija hii anapenda kuwa ni chombo cha amani, mjenzi wa madaraja ya watu kukutana ili kudumisha udugu wa kibinadamu; haki msingi, utu na heshima ya binadamu, daima uhuru wa kidini na uhuru wa kuabudu vikipewa uzito unaostahili.

Kwa mara ya kwanza katika historia ya Kanisa, Baba Mtakatifu Francisko anatembelea Umoja wa Falme za Kiarabu, ulioanzisha uhusiano wa kidiplomasia na Vatican kunako mwaka 2007. Lakini, Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake tangu 2013 amepata fursa ya kukutana na waamini pamoja na viongozi wa dini ya Kiislam pamoja na kubahatika kutembelea nchi kadhaa zenye waamini wengi wa dini ya Kiislam. Lengo ni kushuhudia umoja na upendo wa watu wa Mungu unaofumbatwa katika tofauti zao msingi na kwamba, dini ni chombo cha haki, amani, upendo na mshikamano wa dhati na kamwe hakiwezi kutumiwa kwa ajili ya kuleta: vita, kinzani na mipasuko ya kijamii!

Waamini wa dini mbali mbali wanapaswa kuheshimiana, kuthaminiana na kuaminiana, ili kukuza na kudumisha haki, amani na maridhiano kama ndugu wamoja! Kunako mwaka 2014 Baba Mtakatifu alifanya hija ya kitume nchini Yordani, akawataka Wakristo na Waislam kujenga na kudumisha uhusiano na mafungamano bora; kwa kuzingatia misingi ya uhuru wa kidini; utu na heshima ya binadamu. Akiwa nchini Albania, aliwahamasisha waamini wa dini mbali mbali nchini humo kushikamana, kushirikiana na kuheshimiana.

Akiwa nchini Uturuki, Baba Mtakatifu aliwaambia waandishi wa habari kwamba, alikwenda nchini humo kama hujaji wa amani, akapata nafasi ya kusali na waamini wa dini ya Kiislam. Mufti akamfafanulia kwa unyenyekevu na heshima kubwa nafasi ya Bikira Maria na Yohane Mbatizaji kadiri ya Koran Tukufu! Kwa pamoja waliweza kusali kwa ajili ya kuombea amani nchini Uturuki na sehemu mbali mbali za dunia.

Mwaka 2015, Baba Mtakatifu Francisko akabahatika kutembelea Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati na huko akafungua maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya Huruma ya Mungu. Hii ni nchi ambayo ilikuwa inachechea sana kutokana na vita ya wenyewe kwa wenyewe iliyogeuzwa na kufunikwa na “blanketi la udini” unaofumbatwa na misimamo mikali ya kiimani. Baba Mtakatifu aliwakumbusha wananchi wa Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati kwamba, wao ni ndugu wamoja, licha ya tofauti zao msingi za kiimani na kidini.

Vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini humo, kilikuwa ni kielelezo cha uchu wa mali, madaraka, fedha na umaarufu usiokuwa na tija wala mashiko kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wananchi wengi. Waamini wanapaswa kuwa ni wajumbe na vyombo vya haki, amani na maridhiano. Kwa miaka nenda rudi, Wakristo na Waislam wamekuwa wakiishi kwa amani na utulivu! Misimamo mikali ya kidini, kiimani pamoja na vitendo vya kigaidi ni mambo ambayo yamevuruga kwa kiasi kikubwa umoja, mshikamano na mafungamano ya kijamii.

Waamini wanahamasishwa na Baba Mtakatifu kuwa macho na makini ili wajanja wachache katika jamii, wasiwatumbukize katika majanga na maafa makubwa kutokana na sababu zao binafsi. Baba Mtakatifu katika hija yake nchini Misri kwa mwaliko wa Dr. Ahmad Al-Tayyib, Imam Mkuu wa Msikiti wa Al- Azhar, ulioko Kairo, nchini Misri alikumbushia umuhimu wa waamini kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Waamini wawe kweli ni vyombo na wajenzi wa amani na utulivu, nguzo msingi katika mchakato wa maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu.

Baba Mtakatifu anasema, Mwenyezi Mungu ni asili ya: uhai, wema na utakatifu na kamwe hawezi kuwa ni chanzo cha vita, chuki na uhasama! Jina la Mungu ni takatifu na ni chemchemi ya furaha na amani ya kweli. Leo hii dunia inawahitaji wajenzi wa amani na wala si “wachochezi wa vita na ghasia” dunia inawahitaji watu jasiri wanaoweza kuthubutu kuzima moto wa chuki na uhasama na wala si watu wanaochekelea vita na maafa ya watu! Dunia inawahitaji manabii na wahubiri wa haki, amani na upatanisho!

Baba Mtakatifu alipokutana na Rais Abdel Fattal al Sisi wa Misri, alikazia umuhimu wa kuwaelimisha na kuwafunda vijana wa kizazi kipya sanaa na utamaduni wa haki, amani na maridhiano; umoja na udugu, ili kufyekelea mbali utamaduni wa kifo. Baba Mtakatifu akiwa nchini Myanmar na Bangaladesh, aliwahimiza waamini wa dini mbali mbali katika nchi hizi kujenga na kudumisha umoja, upendo na mshikamano; nyenzo msingi katika ustawi na maendeleo ya wengi. Waamini wawe na ujasiri wa kukataa utamaduni wa kifo, kwa kujenga madaraja yanayowakutanisha watu katika ukweli na uwazi; upendo na mshikamano.

Viongozi wa kidini wanapaswa kuwa na sauti moja dhidi ya misimamo mikali ya kidini inayohatarisha misingi ya haki, amani na maridhiano, kiasi cha kuwatumbukiza watu katika majanga na maafa makubwa: kiroho na kimwili. Mkutano wa Kimataifa wa majadiliano ya kidini huko Abu Dhambi, Umoja wa Falme za Kiarabu ambao umeandaliwa na Wazee wa Dini ya Kiislam unahudhuriwa na viongozi takribani 600 kutoka katika dini mbali mbali duniani, ili kujenga na kudumisha udugu wa kibinadamu!

Papa na Majadiliano ya Kidini
02 February 2019, 15:17