Tafuta

Vatican News
Papa Francisko asema, hija yake ya kitume huko Umoja wa Falme za Kiarabu amekazia: amani, majadiliano na udugu! Papa Francisko asema hija yake ya kitume huko Umoja wa Falme za Kiarabu amekazia: amani, majadiliano na udugu! 

Papa: Umoja wa Falme za Kiarabu: Amani, Majadiliano na Udugu!

Baba Mtakatifu anasema, wakati wote wa hija yake huko Umoja wa Falme za Kiarabu amemfikiria sana Mtakatifu Francisko wa Assisi; moyoni mwake uliwaka moto wa Injili na Upendo kwa Kristo Yesu! Katika matukio mbali mbali, Sala ya Baba Yetu kwa ajili ya watoto wake wote, lakini zaidi kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii iliendelea kusikika moyoni mwake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kama sehemu ya kumbu kumbu ya maadhimisho ya Miaka 800 tangu Mtakatifu Francisko wa Assisi alipomtembelea Sultan Al Malik Al-Kamil, Baba Mtakatifu Francisko, kuanzia tarehe 3-5 Februari 2019 amefanya hija ya kitume huko Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu, kwa kuongozwa na kauli mbiu “Nifanye chombo cha amani”. Hija hii ni mwendelezo wa jitihada za majadiliano ya kidini kati ya Kanisa Katoliki la waamini wa dini ya Kiislam.

Itakumbukwa kwamba, kunako mwaka 2017, Baba Mtakatifu Francisko alitembelea Chuo Kikuu cha Al-Azhar, Kairo, Misri na kuhudhuria mkutano wa majadiliano ya kidini kimataifa. Baba Mtakatifu wakati wa Katekesi yake, Jumatano, tarehe 6 Februari 2019 amefanya rejea kwenye Hija yake ya 27 Kimataifa huko Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu, ambako ameandika historia ya ukurasa mpya wa majadiliano ya kidini kati ya Wakristo na Waislam kwa kujikita katika kutafuta na kudumisha amani duniani inayofumbatwa katika udugu wa kibinadamu.

Baba Mtakatifu anasema, wakati wote wa hija yake huko Umoja wa Falme za Kiarabu amemfikiria sana Mtakatifu Francisko wa Assisi; moyoni mwake uliwaka moto wa Injili na Upendo kwa Kristo Yesu! Katika matukio mbali mbali, Sala ya Baba Yetu kwa ajili ya watoto wake wote, lakini zaidi kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii iliendelea kusikika moyoni mwake.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, amewakumbuka na kuwaombea waathirika wa  dhuluma na nyanyaso mbali mbali; watu wanaoonewa na kuteseka kutokana na ukosefu wa haki msingi za kijamii; watu wanaopoteza maisha yao kutokana na vita, maafa na majanga mbali mbali ya maisha. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, majadiliano ya kidini kati ya Wakristo na Waislam hayana budi kupata chimbuko lake katika sala, nguzo msingi ya kudumisha amani katika ulimwengu mamboleo.

Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuwashukuru viongozi wakuu wa Umoja wa Falme za Kiarabu waliompokea na kumkaribisha kwa heshima kubwa. Akashuhudia ustawi na maendeleo ya wananchi wa Umoja wa Falme za Kiarabu, ambayo kwa miaka ya hivi karibuni, imecharuka sana kwa maendeleo, kiasi cha kuwa ni daraja kati ya nchi za Mashariki na Magharibi; chemchemi ya watu kutoka katika makabila na dini mbali mbali, mazingira ambayo ni muafaka sana katika kukuza na kudumisha utamaduni wa watu kukutana.

Baba Mtakatifu anawashukuru viongozi wa Kanisa na jumuiya zote za wakristo; wakleri, watawa na waamini walei katika ujumla wao, wanaoendelea kujisadaka kwa ajili yakutangaza na kushuhudia furaha ya Injili huko Uarabuni. Anasema, amebahatika kukutana na Padre wa kwanza kabisa kwenda Umoja wa Falme za Kiarabu, kwa sasa ana miaka 90, amezeeka na ni kipofu, lakini bado ni msheshi sana na mtu wa shukrani kwa kubahatika kutangaza na kushuhudia Injili pamoja na kuanzisha jumuiya za waamini. Hata leo hii bado anachapa kazi, matendo makuu ya Mungu. Baba Mtakatifu amewashukuru mapadre wote wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa Kristo Yesu na Kanisa lake na amewatia shime kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu!

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Hati ya Udugu wa Kibinadamu, iliyotiwa mkwaju kati yake na Dr. Ahmad Al-Tayyib, Imam Mkuu wa Msikiti wa Al- Azhar, ulioko Kairo, nchini Misri, Jumatatu, tarehe 4 Februari 2019 ni hatua kubwa! Viongozi wa kidini wanakiri kwa pamoja wito wa watu wote kwamba, wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu; wote ni watoto wa Baba mmoja! Kwa nguvu zote wanalaani vitendo vyote vinavyosababisha vita na ghasia hasa zile zinazofumbatwa katika misingi ya udini.

Kwa pamoja wanataka kusimama kidete kutangaza na kushuhudia tunu msingi za maisha ya kiroho na amani duniani. Baba Mtakatifu anasema, Hati hii itasomwa na kufundishwa kwenye shule, taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu sehemu mbali mbali za dunia. Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuisoma, kuitafakari na kuifahamu, ili kupata changamoto ya kuweza kusonga mbele katika mchakato wa majadiliano mintarafu udugu wa kibinadamu.

Hati hii ni muhimu sana katika mchakato wa kujenga na kudumisha amani, upendo na mshikamano, kinyume kabisa cha watu wengi ambao wangependa kuona Wakristo na Waislam wakisigana, wakitofautiana na pale inapobidi, “wakitwangana ngumi”! Hii ni hatua kubwa katika mchakato wa ujenzi wa waamini wa dini mbali mbali kukutana, kujadiliana, kupendana na kuheshimiana kama ndugu licha ya tofauti zao msingi. Waislam na Wakristo katika umoja wao, wanaheshimu na kuthamini: maisha, tunu msingi za familia, maisha ya kiroho, heshima na adabu kwa wazee na watu wazima; elimu kwa vijana pamoja na mambo kama haya!

Baba Mtakatifu ameendelea kufafanua kwamba, huko katika Umoja wa Falme za Kiarabu kuna Wakristo takribani milioni moja kutoka sehemu mbali mbali za dunia, lakini wengi wao ni wale wanaotoka Barani Asia. Baba Mtakatifu anasema, amebahatika kukutana na kuzungumza na wawakilishi wao kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Yosefu, Abu Dhabi. Hili ni Kanisa la kawaida. Baada ya hapo alikwenda kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa watu wote, tukio ambalo limehudhuriwa na kushuhudiwa na umati mkubwa wa waamini na watu wenye mapenzi mema kutoka ndani na nje ya Umoja wa Falme za Kiarabu.

Baba Mtakatifu anasisitizia kwamba, ameadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu katika Uwanja wa Michezo wa Zayed, Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu, huku akitangaza Injili ya Heri za Mlimani, muhtasari wa Mafundisho makuu ya Kristo Yesu kwa wafuasi wake. Baba Mtakatifu ameshirikiana na viongozi mbali mbali wa Makanisa kusali kwa ajili ya kuombea haki na amani duniani, lakini zaidi huko Mashariki ya Kati pamoja na Yemen ambayo kwa sasa imegeuka kuwa ni uwanja wa vita, mateso na mahangaiko ya watu wasiokuwa na hatia!

Baba Mtakatifu amehitimisha katekesi yake kwa kusema, haya ni kati ya maajabu ambayo Mwenyezi Mungu anaendelea kulitendea Kanisa lake. Waamini wanao wajibu wa kumshukuru kwa uwepo wake na kuendelea kuomba ili mbegu za Habari Njema ya Wokovu zilizopandwa sehemu mbali mbali za dunia ziweze kuzaa matunda yanayokusudiwa kadiri ya mapenzi yake!

Papa: Katekesi
06 February 2019, 14:36