Cerca

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko amewasili Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu ili kushiriki katika mkutano wa majadiliano ya kidini kimataifa. Baba Mtakatifu Francisko amewasili Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu ili kushiriki katika mkutano wa majadiliano ya kidini kimataifa. 

Umoja wa Falme za Kiarabu: Papa Francisko mjumbe wa amani!

Baba Mtakatifu alipowasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa amelakiwa na viongozi wa Kanisa pamoja na viongozi wa Serikali waliokuwa chini ya uongozi wa Mfalme Mrithi Sheikh Mohammed bin Zayed Al Nahyan. Watoto wawili wamemzawadia Baba Mtakatifu shada la maua na baadaye akakagua gwaride la heshima. Baba Mtakatifu amesalimiana na baadhi ya wajumbe.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Hija ya 27 ya  Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko kwenye Umoja wa Falme za Kiarabu kuanzia tarehe 3-5 Februari 2019 inaongozwa na kauli mbiu “Nifanye chombo cha amani”. Hii ni ziara inayopania kuandika ukurasa mpya wa historia na matumaini ya watu wa Mungu mintarafru majadiliano ya kidini ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu!

Baba Mtakatifu akiwa njiani kuelekea Abu Dhambi, Umoja wa Falme za Kiarabu amewatumia wakuu wa nchi salam na matashi mema alipokuwa akipita juu ya anga la nchi zao. Marais hawa ni wale wa Italia, Malta, Ugiriki, Misri, Saudi Arabia pamoja na Bahrain. Baba Mtakatifu katika salam na matashi mema kwa Rais Sergio Mattarella wa Italia amemwambia kwamba, anakwenda kwenye Nchi ya Umoja wa Falme za Kiarabu kama hujaji wa amani na udugu kati ya watu wa Mataifa. Baba Mtakatifu amewatakia wananchi wa Italia, ustawi na maendeleo. Kwa viongozi wengine wa Kimataifa amewatakia: furaha, amani, baraka na nguvu ya kusonga mbele katika mchakato wa maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu. Akiwa njiani, Baba Mtakatifu kama sehemu ya mapokeo yake, “amechonga tena” na waandishi wa habari walioko kwenye msafara wake!

Waandishi hawa wamemkaribisha kwa salam na matashi mema ya amani na afya njema. Wamemtakia kila la kheri katika hija hii ya kitume, ili kweli aweze kuwa ni chombo cha amani, ili kusaidia mchakato wa kuimarisha majadiliano ya kidini yanayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu, ili kweli amani iweze kushamiri katika akili na nyoyo za watu wa Mataifa, daima wakiendelea kudumisha udugu wa kibinadamu. Baba Mtakatifu amewaambia waandishi wa habari kwamba, mvua kubwa ilikuwa inanyeesha huko Abu Dhabi, dalili za neema na baraka. Baba Mtakatifu amewagawia waandishi wa Habari, Picha iliyochorwa kwenye Monasteri ya Bose inayojikita katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene. Baba Mtakatifu anasema, ni picha inayoonesha majadiliano kati ya vijana wa kizazi kipya pamoja na “vijana wa zamani”. Hii ni changamoto kubwa katika ulimwengu mamboleo.

Katika matukio kama haya, alama ya neema, huruma na upendo wa Mungu vinajionesha kati ya watu. Kuna daktari mmoja kutoka Umoja wa Falme za Kiarabu, aliyesomea nchini Italia na kufaulu vizuri, kama alama ya shukrani kwa Mwenyezi Mungu, katika siku hizi za karibuni, ameamua kuwafanyia upasuaji mkubwa watoto kutoka Yemen ambao wameathirika kutokana na vita! Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko kabla ya kuondoka kuanza safari yake ya kitume, amewakumbuka watoto wa Yemen wanaoteseka kwa baa la njaa, kiu na magonjwa.

Hatimaye, Baba Mtakatifu alipowasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa amelakiwa na viongozi wa Kanisa pamoja na viongozi wa Serikali waliokuwa chini ya uongozi wa Mfalme Mrithi  Sheikh Mohammed bin Zayed Al Nahyan. Watoto wawili wamemzawadia Baba Mtakatifu shada la maua na baadaye akakagua gwaride la heshima. Baba Mtakatifu amesalimiana na wajumbe waliokuwepo hapo na kati yao alikuwepo Dr. Ahmad Al-Tayyib, Imam Mkuu wa Msikiti wa Al- Azhar, ulioko Kairo, nchini Misri. Kwa pamoja wakaelekea kwenye Jumba la Al Mushrif.

Papa: Kuwasili

 

04 February 2019, 11:14