Vatican News
Nia za Baba Mtakatifu Francisko kwa Mwezi Februari 2019: Mshikamano katika mapambano dhidi ya biashara ya binadamu na utumwa mamboleo. Nia za Baba Mtakatifu Francisko kwa Mwezi Februari 2019: Mshikamano katika mapambano dhidi ya biashara ya binadamu na utumwa mamboleo. 

Nia za Baba Mtakatifu kwa mwezi Februari: Biashara ya binadamu

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwenye Mtandao wa Utume wa Sala Kimataifa, anasikitika kusema, utumwa mamboleo upo na wala si jambo lililopitwa na wakati” na wala hakuna mtu anayeweza kujitoa kabisa kwamba, hausiki na janga hili, kwani kwa namna moja au nyingine, anashiriki katika biashara ya utumwa mamboleo ambayo ni uhalifu dhidi ya ubinadamu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Waathirika wa biashara na utumwa mamboleo ni watu wanaoonekana kila kukicha, wakiwa wameandikwa kwenye vyombo vya mawasiliano ya jamii. Ni watu ambao wamepachikwa majina kama vile: wahamiaji wa kiuchumi, wakimbizi, wahamiaji haramu, watu wasiokuwa na makazi maalum; watoto wasiosindikizana na wazazi au walezi wao. Ni watu wanaosafiri katika misafara mikubwa ya watu pamoja na kukabiliana na changamoto mbali mbali! Kinachosikitisha ni kuona kwamba, wengi wanasahau kwamba, hawa ni binadamu, wenye utu, heshima na historia yao!

Kuna mamilioni ya watu wanaotumbukizwa katika utumwa mamboleo! Hawa ni watu wanaozikimbia familia na nchi zao kutokana na vita, baa la njaa na utapiamlo; madhulumu na nyanyaso za kisiasa na kidini, umaskini wa kutisha pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi. Kuna makundi makubwa ya uhalifu wa kitaifa na kimataifa yanayofaidika, kwa kuwatumbukiza watu katika utumwa mamboleo. Hawa ndio wale watoto wanaofanyishwa kazi za suluba; biashara ya ngono; biashara ya binadamu na viungo vyake na hata wakati mwingine wanajikuta wakilazimishwa kushiriki na kuridhia vitendo vya kihalifu.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwenye Mtandao wa Utume wa Sala Kimataifa, anasikitika kusema, utumwa mamboleo upo na wala si jambo lililopitwa na wakati” na wala hakuna mtu anayeweza kujitoa kabisa kwamba, hausiki na janga hili, kwani kwa namna moja au nyingine, anashiriki katika biashara ya utumwa mamboleo ambayo ni uhalifu dhidi ya ubinadamu. Kwa njia ya ushirikiano na “Talita Kum”, mtandao wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume Kimataifa unaotekeleza dhamana na wajibu wake katika nchi 77 duniani katika mapambano dhidi ya biashara ya binadamu na utumwa mamboleo inawezekana kabisa kukomesha utumwa mamboleo.

Juhudi hizi zinaungwa mkono na Idara ya Wahamiaji na Wakimbizi, Baraza ya Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu na Fungamani ya Binadamu; Huduma ya Wayesuit kwa ajili ya wahamiaji; Taasisi ya Kipapa ya Sayansi pamoja na Utume wa Bahari. Itakumbukwa kwamba, Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 8 Februari, anaadhimisha kumbu kumbu ya Mtakatifu Josefina Bakhita aliyezaliwa kunako mwaka 1868 huko Sudan Kongwe na kufariki dunia tarehe 8 Februari 1947. Mtakatifu Yohane Paulo II akamtangaza Josefina Bakhita kuwa Mwenyeheri tarehe 17 Mei 1992, na hatimaye, akamtangaza kuwa Mtakatifu tarehe 1 Oktoba, mwaka 2000.

Katika maadhimisho ya Kumbu kumbu ya Mtakatifu Josefina Bakhita, kunako mwaka 2015, Kanisa lilianzisha Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Biashara Haramu ya Binadamu na utumwa mamboleo unaoendelea kudhalilisha: utu, heshima na haki msingi za binadamu. Hii ni siku ya sala na tafakari ya kina kuhusu madhara ya biashara ya binadamu na viungo vyake, pamoja na mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo ambayo ni uhalifu mkubwa dhidi ya ubinadamu. Maadhimisho haya kwa mwaka 2019 yameongozwa na Kauli mbiu: “Tushikamane kwa pamoja kupambana na biashara ya binadamu”. Baba Mtakatifu katika nia zake za jumla kwa Mwezi Februari, 2019 anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kusali kwa ajili ya kuombea ukarimu kwa waathirika wa biashara ya binadamu, utumwa mamboleo, vita na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Kwa upande wake, Padre Frederic Fornos, Mkurugenzi wa Mtandao wa Utume wa Sala Kimataifa anasema, Baba Mtakatifu Francisko yuko mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya biashara ya binadamu na utumwa mamboleo. Baba Mtakatifu anasikitika kusema, watu wengi wanajikuta wakihatarisha maisha yao kwa kujitumbukiza hata katika mitego haramu inayohatarisha maisha, utu na heshima yao. Matokeo yake ni wimbi kubwa la wahamiaji na wakimbizi kutumbukizwa katika biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo. Makundi ya kigaidi na magenge ya uhalifu wa kimataifa yanatumia njia za wakimbizi na wahamiaji kujipatia fedha haramu. Watu wanapaswa kupambana na biashara haramu ya binadamu, kwa kutoa taarifa bila kusahau kukimbilia huruma ya Mungu kwa njia ya sala.

 

Padre Michael Czerny, Katibu mkuu msaidizi, Idara ya Wahamiaji na Wakimbizi, Baraza ya Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu na Fungamani ya Binadamu anasema kwamba, hivi karibuni, Baraza lake lilichapisha Mwongozo wa Shughuli za Kichungaji Kuhusiana na Biashara ya Binadamu. Mwongozo huu unafafanua kwa kina na mapana janga kubwa la biashara ya binadamu linaloendelea kukua na kupanuka kila mwaka sehemu mbali mbali za dunia. Serikali zinapaswa kuwa makini kulinda maisha na usalama wa raia wake. Wahusika watafutwe, wakamatwe na sheria ishike mkondo wake.

Nia za Papa Februari
12 February 2019, 13:20