Tafuta

Vatican News
Papa Francisko asema, kifodini ni ushuhuda, utume na zawadi kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake! Papa Francisko asema, kifodini ni ushuhuda, utume na zawadi kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake!  (Vatican Media)

Papa Francisko asema kifodini ni zawadi, utume na ushuhuda!

Mfalme Herode alidhani kwamba, Yohane Mbatizaji alikuwa ni Nabii, alimwogopa, kwani alijua kuwa ni mtu wa haki, mtakatifu, akamlinda na kumsikiliza kwa furaha. “Alimsweka ndani” kwa vile Yohane Mbatizaji alimshutumu kwa uzinzi, lakini hakutumia fursa hii kutubu na kumwongokea Mungu. Hii inatokana na ukweli kwamba, tayari alikuwa amelewa madaraka!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mwinjili Marko anasimulia kwa ufupi jinsi ambavyo Yohane Mbatizaji alivyoyamimina maisha yake kama ushuhuda kwa ukweli na upendo alioutangaza katika maisha na utume wake. Yohane Mbatizaji ni mtu maarufu katika Agano Jipya, lakini aliamua kujinyenyekesha ili kumwachia nafasi Kristo Yesu aweze kufahamika zaidi. Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake, kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha, Ijumaa, tarehe 8 Februari 2019 amewaalika waamini kutafakari kwa kina wahusika wakuu wanne wanaosimuliwa katika Injili ya Marko waliopelekea kukatisha maisha ya Yohane Mbatizaji: Mtu wa kwanza ni Mfalme Herode, fisadi na mtu asiye na msimamo katika maisha.

Pili, ni Herodia aliyekuwa anamchukia Yohane Mbatizaji kwa sababu alimwambia ukweli! Tatu ni Salome, binti Herodia aliyecheza mbele ya Mfalme, kiasi cha kumfanya achanganyikiwe na kutoa ahadi ambazo baadaye zimemtesa sana kwa mauaji ya mtu wa Mungu. Nne, ni Yohane Mbatizaji, Nabii aliyetangaza na kusimamia ukweli, aliyekatwa kichwa na wafuasi wake waliposikia wakaja na kuuchukua mwili wake kwenda kuuzika kwa heshima! Hivi ndivyo nyota angavu ya Yohane Mbatizaji, ilivyozimika baada ya kumshuhudia Kristo Yesu, Mwanakondoo wa Mungu anayeiondoa dhambi za ulimwengu.

Yohane Mbatizaji, kati ya watu maarufu wa Agano Jipya, anaishia kukatwa kichwa! Baba Mtakatifu anakaza kusema, kifodini ni huduma, utume na zawadi kubwa kutoka kwa Kristo Yesu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kifodini ni kielelezo cha ukatili wa binadamu dhidi ya watu waaminifu. Mfalme Herode alidhani kwamba, Yohane Mbatizaji alikuwa ni Nabii, alimwogopa, kwani alijua kuwa ni mtu wa haki, mtakatifu, akamlinda na kumsikiliza kwa furaha. “Alimsweka ndani” kwa vile Yohane Mbatizaji alimshutumu kwa uzinzi, lakini hakutumia fursa hii kutubu na kumwongokea Mungu. Hii ni kwa sababu alikuwa tayari amelewa madaraka kutokana na ufisadi, akasumbuliwa sana na dhamiri nyofu.

Baba Mtakatifu anasema, Herodia aliyekuwa anamchukia Yohane Mbatizaji na matokeo yake akahakikisha kwamba, anamfutilia mbali kutoka katika uso wa dunia, kazi kubwa ya Shetani. Ni mwanamke ambaye hakufahamu maana halisi ya upendo na badala yake, akamezwa na chuki pmoja na uhasama dhidi ya Yohane Mbatizaji. Salome, binti Herodia aliahidiwa kupewa nusu ya Ufalme wa Herode! Watu hawa wote wanaonekana kwamba, walikuwa ni wateja wa Shetani, aliyehakikisha kwamba, shuhuda wa ukweli na utakatifu unazimwa kama “kibatari” na kutoweka katika sura ya nchi.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Yohane Mbatizaji, akauwawa kikatili, peke yake mle gerezani kama ilivyo kwa wafidia dini na waungama imani wengi! Huu ni ushuhuda wa hali ya juu wa utakatifu unaofumbatwa katika maisha ya waamini. Ni maisha yanayomiminwa na sadaka inayotolewa, mwaliko na changamoto kwa waamini kufanya tafakari ya kina kuhusu wahusika wanaozungumziwa kwenye Injili ya Marko mintarafu kifo chake, kama changamoto ya kumshuhudia Kristo si tu kwa maneno, bali kwa njia ya maisha yao adili na matakatifu, kama alivyokuwa Yohane Mbatizaji!

Papa Mfalme Herode: Yohane Kukatwa Kichwa!

 

 

08 February 2019, 15:35