Tafuta

Vatican News
Papa Francisko tarehe 25 Machi 2019 atatembelea Madhabahu ya Loreto na kutia sahihi Wosia wa Kitume baada ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Vijana 2018 Papa Francisko tarehe 25 Machi 2019 atatembelea Madhabahu ya Loreto na kutia sahihi Wosia wa Kitume baada ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Vijana 2018 

Papa Francisko kutembelea Loreto na kutia mkwaju Wosia wa kitume

Hii itakuwa ni siku maalum kwa Baba Mtakatifu Francisko kutia mkwaju kwenye Wosia wa Kitume, mara baada ya Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Vijana iliyokuwa inaongozwa na kauli mbiu “Vijana, imani na mang’amuzi ya miito”. Baba Mtakatifu anataka kumkabidhi Bikira Maria wa Loreto Wosia wake wa Kitume, baada ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu 2018.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kila mwaka ifikapo tarehe 25 Machi, Mama Kanisa anaadhimisha Siku kuu ya Bikira Maria kupashwa habari kuwa atakuwa ni Mama wa Mkombozi. Siku hii imekuwa ikitumiwa na Mabaraza mbali mbali ya Maaskofu Katoliki kwa ajili ya kuhimiza utamaduni wa kulinda uhai, kuonesha ukuu na utakatifu wa maisha yanayopaswa: kulindwa, kutunzwa na kuendelezwa. Baba Mtakatifu Francisko tarehe 25 Machi 2019 atafanya hija kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Loreto nchini Italia.

Hii itakuwa ni siku maalum kwa Baba Mtakatifu Francisko kutia mkwaju kwenye Wosia wa Kitume, mara baada ya Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Vijana iliyokuwa inaongozwa na kauli mbiu “Vijana, imani na mang’amuzi ya miito”. Haya yamebainishwa na Dr. Alessandro Gisoti, Msemaji mkuu wa muda wa Vatican. Baba Mtakatifu anataka kumkabidhi Bikira Maria wa Loreto Wosia wake wa Kitume, baada ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana iliyofanyika hapa mjini Vatican kuanzia tarehe 3 – 28 Oktoba 2018.

Baba Mtakatifu Francisko atakapowasili mjini Loreto, atapokelewa na viongozi wa Serikali na Kanisa na baadaye, ataelekea kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Loreto. Asubuhi, ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu na baada ya Misa, atatia sahihi kwenye Wosia wa Kitume, mara baada ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Vijana. Baba Mtakatifu atapata nafasi ya kusalimiana na wanajumuiya ya Wakapuchini na baadaye, atasalimiana na wagonjwa pamoja na familia ya Mungu mjini Loreto pamoja na viunga vyake. Baba Mtakatifu ataongoza Sala ya Malaika wa Bwana na baadaye kupata chakula cha mchana pamoja na Maaskofu. Majira ya alasiri, Baba Mtakatifu Francisko atakunja vilago na kurejea tena mjini Vatican kuendelea na maisha pamoja na utume wake!

26 February 2019, 08:49