Cerca

Vatican News
Papa Francisko asema, Jamii haina budi kuhakikisha kwamba, utu, heshima na haki msingi za wanawake magerezani zinalindwa na wote! Papa Francisko anasema, Jamii haina budi kuhakikisha kwamba, utu, heshima na haki msingi za wanawake magerezani zinalindwa na wote!  (Vatican Media)

Papa Francisko: Utu na heshima ya wanawake wafungwa viheshimiwe!

Jamii inapashwa kuboresha hali ya magereza ili kuwawezesha wafungwa wanapomaliza kutumia adhabu zao, waweze kurejea tena katika maisha ya kawaida na kwamba, kifungo si laana ya maisha! Wafungwa magerezani wajengewe mazingira mazuri yatakayowawezesha kujifunza stadi za maisha; kuboresha mahusiano na mafungamano yao ya kijamii, ili wasitengwe na jamii!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, hivi karibuni alisikika akisema,  magereza yanapaswa kuboreshwa zaidi, ili kulinda na kudumisha utu na heshima ya binadamu! Inasikitisha kusikia na kuona kwamba, magereza yanageuka kuwa ni mahali pa vurugu, uvunjifu wa sheria, kanuni na taratibu za nchi. Magereza yamekuwa ni mahali ambapo utu na heshima ya binadamu vinasiginwa kwa kiasi kikubwa!

Utume kwa wafungwa magerezani ni kati ya mambo ambayo Baba Mtakatifu anayapatia kipaumbele, ili kuwasaidia wafungwa na mahabusu kulinda na kudumisha utu na heshima yao, chemchemi ya matumaini ya maisha mapya! Baba Mtakatifu katika barua ambazo amekua akiandiakiana na baadhi ya wafungwa wa kike kutoka Gereza la Wanawake la Ezeiza huko nchini Argentina anakazia umuhimu wa wanawake kulinda utu na heshima yao, licha ya changamoto na magumu mbali mbali wanayopitia katika kutekeleza adhabu yao gerezani.

Jamii inapashwa kuboresha hali ya magereza ili kuwawezesha wafungwa wanapomaliza kutumikia adhabu zao, waweze kurejea tena katika maisha ya kawaida na kwamba, kifungo si laana ya maisha! Wafungwa magerezani wajengewe mazingira mazuri yatakayowawezesha kujifunza stadi za maisha; kuboresha mahusiano na mafungamano yao ya kijamii, ili kuondokana na kishawishi cha kuwatenga watu waliomaliza kutumikia adhabu zao. Hali kama itawaongezea machungu. Baba Mtakatifu anawaalika watu kuonja udhaifu wa binadamu badala ya kuwagawa watu katika makundi ya wema na wabaya. Waone ubaya wa dhambi, tayari kukimbilia na kuambata huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao.

Baba Mtakatifu anasikitika kusema, wafungwa wengi wanawake wanateseka na watoto wao magerezani! Hii inakuwa ni changamoto kubwa kuweza kukabiliana na ugumu wa maisha! Katika hali na mazingira haya, wafungwa wanapaswa kujengewa matumaini, kwa kutambua kwamba, wao ni binadamu wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, wanahistoria ya maisha na kwamba, wanayo ari ya kutaka kuambata matumaini. Maisha ya wafungwa, utu na heshima yao, familia na watu wanaowategemea ni mambo msingi yanayopaswa kuzingatiwa, watu wanapoangalia changamoto za wafungwa wa kike magerezani!

Wanawake

 

12 February 2019, 11:33