Tafuta

Vatican News
Papa Francisko anawapongeza Wamisionari wa Afrika na Masista Wamisionari wa Mama Yetu Malkia wa Afrika kwa kutimiza Miaka 150 ya uwepo na utume wao! Papa Francisko anawapongea Wamisionari wa Afrika na Masista Wamisionari wa Mama Yetu Malkia wa Afrika kwa kutimiza miaka 150 ya uwepo na utume wao!  (Vatican Media)

Wamisionari wa Afrika, Jubilei ya Miaka 150 ya uwepo na utume!

Maisha yao ya wakfu na utume wao, unashuhudiwa katika maisha ya kidugu, utume wao katika medani mbali mbali, uaminifu kwa upendo na ukaribu wa Mungu katika maisha, ili kupandikiza matumaini katika nyoyo za watu waliotikiswa, kujeruhiwa, kukata tamaa na kwa sasa wanajisikia mara nyingi kana kwamba, wametelekezwa! Miaka 150 iliyopita si haba! Kazi inaonekana!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Wamisionari wa Afrika (White Fathers) na Masista Wamisionari wa Mama yetu Malkia wa Afrika (White Sisters), mwaka huu 2019 kwa pamoja wanaadhimisha Jubilei ya Miaka 150 tangu kuanzishwa kwao. Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa, tarehe 8 Februari 2019 amekutana na Wamisionari wa Mashirika haya mawili, ili kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani pamoja na kuwaonesha uwepo wake wa karibu kiroho katika maisha na utume wao! Amewapongeza kwa ari, ukarimu na uaminifu wao wa Injili kama ulivyooneshwa na kushuhudiwa na Kardinali Charles-Martial-Allemand Lavigerie muasisi wao.

Katika kipindi cha Miaka mitatu iliyopita, wameadhimisha kwa pamoja Jubilei hii kama “Familia ya Lavigerie” kwa kurejea tena katika mizizi ya historia na maisha yao, wakapata nguvu ya kupyaisha upendo wao kwa Injili ya Kristo, tayari kupandikiza matumaini. Huu ni muda wa kumshukuru Mungu kwa karama, uwepo, uaminifu na upendo unaoadhimishwa na Mashirika haya; changamoto ya kuendelea kuimarisha imani, umoja na mshikamano na Kristo Yesu. Maisha ya wakfu na utume wao, unashuhudiwa katika maisha ya kidugu, utume wao katika medani mbali mbali, uaminifu kwa upendo na ukaribu wa Mungu katika maisha, ili kupandikiza matumaini katika nyoyo za watu waliotikiswa, kujeruhiwa, kukata tamaa na kwa sasa wanajisikia mara nyingi kana kwamba, wametelekezwa!

Miaka 150 iliyopita wakati Mashirika haya yanaanzishwa, ni watawa wachache sana waliokuwa wanathubutu kutangaza na kushuhudia Injili kwa hali zote na watu wote, kiasi kwamba, mchakato wa kutoka kwenda kutangaza na kushuhudia Injili umekuwa ni utume na vinasaba vya utambulisho wao. Kipaumbele chao cha kwanza ulikuwa ni wasi wasi kwamba, kulikuwa na ndugu zao wengi waliokuwa wanaishi bila kuwa na nguvu, mwanga na faraja inayotokana na na urafiki na Kristo Yesu, bila kuwa na jumuiya ya imani inayowasaidia, bila malengo wala maana ya maisha. Ari hii inawabidisha kutoka kifua mbele kwenda kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu na wala si wongofu wa shuruti!

Lengo ni kushirikishana karama waliyopewa na Roho Mtakatifu kama zawadi na mkutano wa upendo ambao umewaletea mageuzi makubwa kiasi cha kuwekwa wakfu kwa ajili ya Kristo Yesu, Injili na Wokovu wa Ulimwengu! Ni kwa ajili yake, pamoja naye katika Yeye wanaweza kufanikiwa kuumwilisha utume wao kwa kutambua kwanza kabisa, mmisionari wa kweli ni mfuasi. Wamisionari hawa wanatakiwa kukuza na kudumisha mahusiano na Kristo Yesu kwa njia ya Sala, Maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa pamoja na huduma kwa jirani zao, ili kweli matendo yao yawe ni ushuhuda wa uwepo endelevu wa upendo wenye huruma, kwa watu ambao wametumwa kwao na Roho Mtakatifu ili kuwatangazia, ili kweli waweze kuwa ni “watu wasiokuwa na makazi maalum” kwa ajili ya Injili.

Wawe ni watu wenye ujasiri wa kwenda kwenye majangwa ya maisha ya watu wa nyakati hizi ili kutafuta nyenzo zitakazowasindikiza jirani zao hadi kufikia kisima cha maji ya uzima wa milele ambacho ni Kristo Yesu, ili maji hai yanayobubujika kutoka kwenye upendo wake, yaweze kuzima kiu ya maisha yao! Baba Mtakatifu anataka kuona maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 150 tangu kuanzishwa kwa Mashirika yao, yanaimarisha udugu, umoja na mshikamano wa kimisionari, ili waweze kuwa ni mashuhuda wa matumaini yasiyotahayarishwa kwa maana pendo la Mungu limekwisha kumiminwa tayari mioyoni mwao, licha ya magumu na changamoto za maisha.

Wanatakiwa kuthubutu kwenda kufanya utume ili kutangaza na kushuhudia upya wa uwepo wa Mungu unaowawajibisha kutoka kifua mbele kwenda hata mahali pasipofahamika, yaani pembezoni mwa vipaumbele vya watu, ili kwa njia ya Roho Mtakatifu waweze kuwa ni wajenzi wa madaraja na tamaduni zinazowaunganisha watu hata katika tofauti zao msingi. Baba Mtakatifu anawapongeza kwa kuendeleza majadiliano ya kidini kati ya Wakristo na Waislam, kwa njia ya ushuhuda wa maisha na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Kwa fuata nyayo za Kardinali Charles-Martial-Allemand Lavigerie, sasa wanaitwa na kutumwa kupandikiza mbegu ya matumaini; kwa kupambana na utumwa mamboleo; kwa kushikamana na maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii ili utu wao uweze kutambulika na kuheshimika; waweze kupokelewa, kulindwa, kusindikizwa, kuendelezwa na hatimaye, kushirikishwa!

Papa: Wamisionari

 

 

08 February 2019, 16:03