Tafuta

Vatican News
Mkutano wa Kanisa Kuhusu Ulinzi wa Watoto Wadogo: Papa: Kanisa lisikilize kilio cha haki yao! Mkutano wa Kanisa Kuhusu Ulinzi wa Watoto Wadogo: Papa: Kanisa lisikilize kilio cha haki yao!  (Vatican Media)

Mkutano wa Kanisa kuhusu Ulinzi wa Watoto: Sikilizeni kilio chao

Baba Mtakatifu Francisko anasema, kashfa hii ni nyeti sana kwa sababu inagusa maisha na utume wa Kanisa. Huu ni wakati wa toba na wongofu wa ndani, sanjari na kuendelea kumwilisha “dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa” kwa kuzingatia misingi ya ukweli na uwazi, ili kupambanua sera na mikakati itakayoliwezesha Kanisa kufyekelea mbali kashfa za nyanyaso za kijinsia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakifu Francisko anasema ameitisha Mkutano wa Kanisa Kuhusu Ulinzi kwa Watoto Wadogo kuanzia tarehe 21-24 Februari 2019 kama kielelezo makini cha wajibu wa kichungaji ili kuweza kukabiliana na changamoto hii nyeti katika ulimwengu mamboleo. Hiki ni kipindi cha toba na wongofu wa ndani, kwa kusikiliza na kujibu kilio cha watoto wadogo wanaotaka kuona haki ikitendeka, lakini zaidi, Kanisa liibue mbinu mkakati madhubuti wa kuwalinda watoto wadogo, kwa kuwaundia mazingira salama katika malezi na makuzi yao.

Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake elekezi wakati wa ufunguzi wa mkutano huu, tarehe 21 Februari 2019 kwenye Ukumbi mpya wa Sinodi za Maaskofu; mkutano unaohudhuriwa na Marais wa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki kutoka sehemu mbali mbali za dunia, wakuu wa Makanisa na viongozi waandamizi kutoka Sekretarieti kuu, amewataka wajumbe, kujiweka chini ya ulinzi na tunza ya Roho Mtakatifu, ili kumsikiliza kwa makini, na hatimaye, kutambua kilio cha watoto wadogo wanaotaka kuona haki ikitendeka.

Kashfa hii ni nyeti sana kwa sababu inagusa maisha na utume wa Kanisa. Huu ni wakati wa toba na wongofu wa ndani, sanjari na kuendelea kumwilisha “dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa” kwa kuzingatia misingi ya ukweli na uwazi, ili kupambanua sera na mikakati itakayoliwezesha Kanisa kufyekelea mbali kashfa za nyanyaso za kijinsia. Watu wa Mungu kwa sasa wameyaelekeza macho na mawazo yao ili kuangalia kile kitakachoibuliwa na viongozi wa Kanisa katika mkutano huu kwa kuzingatia uzito wa kashfa yenyewe katika maisha na utume wa Kanisa!

Baba Mtakatifu katika hotuba yake elekezi, anawasihi Maaskofu kuhakikisha kwamba, wanachambua na kufuata dira na miongozo mbali mbali ambayo imetolewa na Mabaraza ya Maaskofu kama sera na mbinu mkakati wa kupambana na kashfa ya nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa. Wajumbe wa mkutano huu, waendelee kuonesha kipaji cha ubunifu katika kushirikisha mawazo yao.

Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuwashukuru wajumbe wa Kamati kuu ya Maandalizi, Tume ya Kipapa ya Kuwalinda Watoto Wadogo pamoja na Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa ambao wameshirikiana kuandaa mkutano huu wa aina yake, kuwahi kufanywa na Kanisa mintarafu kashfa ya nyanyaso za kijinsia. Hiki kiwe ni kipindi muafaka cha kujikita katika toba na wongofu wa ndani; wema na utakatifu wa maisha; kwa kuganga na kutibu madonda ya kashfa ya nyanyaso za kijinsia! Mkutano huu umefunguliwa kwa Sala, wajumbe wamepata fursa ya kusikiliza shuhuda mbali mbali kutoka kwa waathirika wa nyanyaso za kijinsia. Mwishoni, kumekuwepo na kimya kikuu katika ukumbi! Ni kashfa ambayo, wengi wanajiuliza, kwanini Mwenyezi Mungu hakuweza kuwasikiliza kilio na kuona machozi yao?

Papa: Kilio cha haki ya Watoto
21 February 2019, 11:40