Cerca

Vatican News
Papa Francisko asema, uchafuzi wa mazingira ni dhambi! Papa Francisko asema, uchafuzi wa mazingira ni dhambi!  (Vatican Media)

Papa Francisko asema uchafuzi wa mazingira ni dhambi!

Taasisi ijenge mazingira na ukaribu zaidi katika uhalisia wa maisha ya watu binafsi na familia katika ujumla wake. Huu ni wajibu wa kusikiliza kwa makini mahangaiko na mateso ya watu wanaosumbuliwa na nguvu mbali mbali za Shetani kwa kukosa: usalama na uhakika wa maisha bora zaidi; umaskini wa hali na kipato pamoja na kusukumiziwa pembezoni mwa jamii!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Taasisi ya Maadili ya Alfonsianum iliyoko Jijini Roma, ilianzishwa kunako mwaka 1960 na Shirika la Mapadre wa Mkombozi, lililoanzishwa na Mtakatifu Alfonsi Maria wa Liguori. Taasisi hii ni kitivo cha Chuo Kikuu cha Kipapa cha Lateran na kwa mwaka 2019 inaadhimisha kumbu kumbu ya miaka 70 tangu kuanzishwa kwake! Ni katika muktadha huu, Jumuiya ya Taasisi ya Maadili ya Alfonsianum, Jumamosi, tarehe 9 Februari 2019 imekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko, ambaye amewataka kuangalia mbele kwa matumaini ili kupyaisha ari na mwamko wa kimisionari, tayari kupiga hatua mbele ili kuzima kiu ya matamanio halali ya watu wa Mungu katika ulimwengu mamboleo!

Baba Mtakatifu mintarafu mwanga wa Katiba ya Kitume “Veritatis gaudium” yaani “Furaha ya ukweli” ambao ni mwongozo makini unaovihusu vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu zinazomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki, anaitaka Taasisi ya Maadili ya Alfonsianum kuwa ni sehemu ya mchakato wa mageuzi makubwa yanayowagusa na kuwaambata watu wa Mungu, katika mwelekeo mzima wa utekelezaji wa utume wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika majadiliano ya kina. Lengo ni kutoa suluhu muafaka kwa changamoto zinazomwandama mwanadamu katika ulimwengu mamboleo kwa njia ya elimu bora na makini.

Baba Mtakatifu anaitaka Taasisi hii kujenga mazingira na ukaribu zaidi katika uhalisia wa maisha ya watu binafsi na familia katika ujumla wake. Huu ni wajibu wa kusikiliza kwa makini mahangaiko na mateso ya watu wanaosumbuliwa na nguvu mbali mbali za Shetani kwa kukosa: usalama na uhakika wa maisha bora zaidi; umaskini wa hali na kipato pamoja na kusukumiziwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii. Hapa hakuna sababu ya kuhukumu, bali kuganga na kuponya kama alivyofanya Kristo Yesu katika maisha na utume wake, aliyewaonea watu huruma na mapendo ya kweli!

Ufundishaji wa Taalimungu maadili hauna budi kusaidia mchakato wa kumwilisha tunu msingi za Kiinjili kama vile upendo, unaopania kumkomboa mwanadamu kutoka katika kongwa la sheria, utumwa wa dhambi na mauti. Huu ni uhuru unaowaambata maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Baba Mtakatifu anawataka wanataalimungu maadili kuvuka kishawishi cha ubinafsi, ili kuanza kujenga mtandao wa ushirikiano na mshikamano ulimwenguni.

Lengo ni kupambana kwa pamoja na changamoto “mpya” na “za hatari” zinazoendelea kuibuliwa kila kukicha. Mwanadamu katika ulimwengu mamboleo anajikuta akielemewa na ushindani usiokuwa na mvuto wala mashiko, kwa kutawaliwa na falsafa ya “Mwenye nguvu mpishe”, bila kuguswa hata kidogo na utu pamoja na heshima ya binadamu, ambaye, wakati mwingine, anageuzwa kuwa kama bidhaa ya kutumiwa na kutupwa! Baba Mtakatifu anasema haya ndiyo yanayoendelea kujitokeza katika sakata zima la uharibifu wa mazingira nyumba ya wote!

Kilio cha Dunia Mama ambaye amejeruhiwa na kunyonywa kupindukia kutokana na uchoyo na ubinafsi. Taalimungu maadili haina budi kupewa kipaumbele cha pekee katika kila nchi kwa kutambua na kuthamini juhudi za Jumuiya ya Kimataifa katika kulinda na kudumisha mazingira bora, nyumba ya wote, kwa kujikita katika sera na mikakati ya maendeleo fungamani ya binadamu! Baba Mtakatifu anakaza kusema, uharibifu wa mazingira nyumba ya wote ni dhambia ambayo waamini wengi hawajathubutu kuitambua wala kuiungama. Hii ni changamato kwa wana maadili kuwaelewesha waamini na watu wenye mapenzi mema kwamba, uharibifu wa mazingira ni dhambi ambayo wanapaswa kuitambua, kuijutia na kuiungama!

Baba Mtakatifu anahitimisha hotuba yake kwa kusema, juhudi za pamoja hazina budi pia kuelekezwa kwenye kanuni maadili ya kibaiolojia. Tafiti za kimaadili hazina budi kushuhudia tunu ya maisha ya binadamu inayopaswa kulindwa, kutunzwa na kuendelezwa, kwa kudumisha imani, umoja, upendo na mshikamano. Taalimungu maadili lazima izame kabisa katika matatizo na changamoto mamboleo, kwa kutangaza na kumshuhudia Kristo Yesu, aliye: Njia, Ukweli na Uzima!

Papa: Alfonsianum
09 February 2019, 14:54