Tafuta

Vatican News
Siku ya Wagonjwa Duniani 2019: Utamaduni wa kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa wagonjwa na maskini duniani! Siku ya Wagonjwa Duniani 2019: Utamaduni wa kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa wagonjwa na maskini duniani! 

Siku ya 27 ya Wagonjwa Duniani: Utu na heshima ya binadamu!

Papa Francisko kwa Siku ya 27 ya Wagonjwa Duniani anakazia: Ujenzi wa utamaduni wa kujisadaka dhidi ya utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine. Hospitali, Zahanati na Vituo vya Afya vinavyoendeshwa na Kanisa Katoliki viwe ni mahali muafaka pa tiba, upendo na mshikamano. Miundo mbinu ya Kanisa iwe ni chemchemi ya: imani, urafiki na mshikamano wa kweli!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko hivi karibuni alimteua Kardinali Patrick D’Rozario, C.S.C, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dhaka, kuwa mwakilishi wake maalum katika maadhimisho ya Siku ya 27 ya Wagonjwa Duniani kwa Mwaka 2019, inayoadhimishwa rasmi kuanzia tarehe 9-11 Februari 2019 huko mjini Calcutta, nchini India, Mama Kanisa anapoadhimisha Siku kuu ya Bikira Maria wa Lourdes. Baba Mtakatifu anakaza kusema, mchakato wa tiba na huduma kwa wagonjwa uzingatie: utu, heshima na mahitaji msingi ya mgonjwa, kielelezo makini cha uinjilishaji wa kina, unaogusa mahitaji msingi ya binadamu!

Maadhimisho ya Mwaka huu, yanaongozwa na kauli mbiu “Mmepata bure, toeni bure”. Mt. 10:8. Huu ni mwaliko kwa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kuhakikisha kwamba, wanajisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma makini kwa wagonjwa sehemu mbali mbali za dunia, kama alivyofanya Msamaria mwema. Wagange kwa mafuta ya faraja na divai ya matumaini.

Baba Mtakatifu katika ujumbe wake kwa Kardinali Patrick D’Rozario anakazia umuhimu wa waamini kuambata utamaduni wa kujisadaka kwa ajili ya wengine, ili kuvuka changamoto ya utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine. Huduma kwa wagonjwa inapaswa kuzingatia weledi, kanuni maadili na utu wema; upendo na mshikamano, ili wagonjwa waweze kujisikia kweli wanapendwa na kuthaminiwa jinsi walivyo. Inasikitisha kuona kwamba, maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia katika tiba ya mwanadamu yanaendelea kusababisha hofu, kiasi kwamba, kumeanza kuzuka tabia ya kutaka kuwageuza watu kuwa kama kichokoo!

Baba Mtakatifu anawataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kushinda kishawishi cha ubinafsi na mipasuko ya kijamii, kwa kujikita katika upendo na mshikamano wa dhati kati ya watu wa dini na tamaduni mbali mbali duniani. Mwanadamu katika hatua mbali mbali za maisha yake, daima ni maskini na mhitaji, kielelezo makini kwamba, binadamu atabaki kuwa ni kiumbe. Katika hali na mazingira kama haya, watu wanapaswa kujenga fadhila ya unyenyekevu na ujasiri katika mshikamano, fadhila muhimu katika maisha ya binadamu. Kwa njia hii, watu wataweza kuwajabikiana na kusaidiana kwa hali na mali bila kugubikwa na “blanketi” la ubaguzi, kwani wote wanategemeana na kukamilishana kama ndugu wamoja.

Huu ndio mwanzo wa mchakato wa ujenzi wa udugu na mshikamano jamii, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Sadaka na majitoleo ya waamini ni chachu muhimu sana ya uinjilishaji anasema Baba Mtakatifu Francisko. Hapa ndiyo mahali ambapo tasaufi ya Msamaria mwema inapaswa kumwilishwa katika huduma kwa wagonjwa, kwa kuzingatia na kudumisha haki zao msingi, utu na heshima yao kama binadamu. Kuna haja kwa jamii kuendeleza sera na mikakati ya kuzuia na kutibu magonjwa kwa wakati muafaka; mambo ambayo yanapaswa kuwa ni sehemu ya vinasaba vya huduma kwa wagonjwa. Miundo mbinu ya huduma kwa wagonjwa inayomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki: vijijini na mijini, iendelee kuboreshwa kwa kusoma alama za nyakati.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, hapa ni mahali ambapo wadau mbali mbali wanapaswa kutangaza na kushuhudia sadaka na majitoleo yao; kwa kuguswa na mahangaiko ya watu na wala si msukumo wa kutafuta faida kubwa, kwa hasara ya Injili ya uhai. Mwishoni mwa ujumbe wake, kwa Kardinali Patrick D’Rozario, C.S.C, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dhaka, mwakilishi wake maalum katika maadhimisho ya Siku ya 27 ya Wagonjwa Duniani anakazia ujenzi wa utamaduni wa kujisadaka dhidi ya utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine. Hospitali, Zahanati na Vituo vya Afya vinavyoendeshwa na Kanisa Katoliki viwe ni mahali muafaka pa tiba, upendo na mshikamano. Miundo mbinu ya Kanisa iwe ni chemchemi ya: imani, urafiki na mshikamano wa kweli na kwamba, sadaka na majitoleo ni afya ya Wakristo!

Papa: Ujumbe kwa Kardinali Patrick
07 February 2019, 15:34