Cerca

Vatican News
Papa Francisko: Kanisa limedhamiria kupambana na kashfa ya nyanyaso za kijinsia katika maisha na utume wake! Papa Francisko: Kanisa limedhamiria kupambana na kashfa ya nyanyaso za kijinsia katika maisha na utume wake!  (AFP or licensors)

Mkutano wa Kanisa Kuhusu Ulinzi wa Watoto: Kanisa limedhamiria!

Nyanyaso za kijinsia ni janga ambalo linawaandama watu wote, ndiyo maana Baba Mtakatifu akataka Kanisa kushirikiana ili kujibu kashfa hii kwa kutumia “dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa”. Mkutano huu imekuwa ni fursa ya kuwasikiliza waathirika wa nyanyaso za kijinsia; kusali na kuomba msamaha kwa Mwenyezi Mungu na wale watu ambao hawakutendewa haki.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili, tarehe 24 Februari 2019 amehitimisha Mkutano wa Kanisa Kuhusu Kuwalinda Watoto Wadogo uliofunguliwa hapo tarehe 21 Februari 2019 kwa kuwashirikisha: Marais wa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki, Viongozi wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume, Viongozi wakuu wa Makanisa pamoja na viongozi waandamizi kutoka Sekretarieti kuu ya Vatican. Lengo lililkuwa ni kujadili kwa kina na mapana kashfa ya nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo ambayo imechafua maisha na utume wa Kanisa.

Huu ni uhalifu dhidi ya utu na heshima ya binadamu. Waathirika wa nyanyaso za kijinsia ni watu walioteseka sana na kwa bahati mbaya, Kanisa halikuweza kusikiliza killio chao wala kuona madonda ya mahangaiko yao; baadhi ya viongozi wa Kanisa wakajenga utamaduni wa kutaka kulindana! Haya yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili, tarehe 24 Februari 2019 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican mara tu baada ya Sala ya Malaika wa Bwana.

Nyanyaso za kijinsia ni janga ambalo linawaandama watu wote, ndiyo maana Baba Mtakatifu akataka Kanisa kushirikiana ili kujibu kashfa hii kwa kutumia “dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa”. Mkutano huu imekuwa ni fursa ya kuwasikiliza waathirika wa nyanyaso za kijinsia; kusali na kuomba msamaha kwa Mwenyezi Mungu na wale watu ambao hawakutendewa haki. Kanisa linatambua fika dhamana na wajibu wake wa kutenda haki katika ukweli pamoja na kuendelea kujizatiti zaidi katika mchakato utakaoliwezesha Kanisa kung’oa aina mbali mbali za matumizi mabaya ya mamlaka; pamoja na kutambua madhara ya nyanyaso za kijinsia.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Kanisa linataka kuhakikisha kwamba, shughuli na maeneo yake yote yanakuwa ni salama kwa malezi na makuzi ya watoto wadogo. Hii ni changamoto ya kuhakikisha kwamba, hatua muhimu zinachukuliwa ili kusitokee tena uhalifu wa namna hii. Kanisa linataka kurejesha hali yake ya kuaminiwa na kutegemewa katika huduma na elimu kwa watoto wadogo kadiri ya mafundisho ya Kristo Yesu. Kanisa linataka kushirikiana na watu wote wenye mapenzi mema sehemu mbali mbali za dunia na hata katika kiwango cha kimataifa ili kuweza kupambana hadi nukta ya mwisho, dhidi ya mifumo yote ya nyanyaso za kijinsia, janga kubwa ambalo limeleta athari kubwa kwa mamilioni ya watoto sehemu mbali mbali za dunia!

Papa: Nyanyaso za Kijinsia
24 February 2019, 10:14