Cerca

Vatican News
Papa Francisko: Jifunzeni kuwahudumia maskini kama alivyofanya Mtakatifu Josefina Bakhita, Msimamizi wa waathirika wa biashara ya binadamu! Papa Francisko: Jifunzeni kuwahudumia maskini kama alivyofanya Mtakatifu Josefina Bakhita, Msimamizi wa waathirika wa biashara ya binadamu!  (Vatican Media)

Papa Francisko: Jifunzeni kuwahudumia maskini kama Mt. Bakhita!

Baba Mtakatifu amewataka wanachama wa Mfuko wa Galileo kuchangia zaidi katika mchakato wa kuragibisha kuhusu madhara ya umaskini na unyonyaji unaofanywa kwa njia ya biashara ya binadamu pamoja na mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo. Tarehe 8 Februari, Kanisa linafanya kumbu kumbu ya Mtakatifu Josefina Bakhita, Msimamizi wa waathirika wa utumwa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mfuko wa Galileo ulianzishwa kunako mwaka 1934 huko Pisa, Kaskazini mwa Italia, ukiwa na lengo la kusambaza tafiti mbali mbali za imani, kanuni maadili na utu wema mintarafu Mafundisho jamii ya Kanisa. Mfuko huu unapania kumjengea uwezo Khalifa wa Mtakatifu Petro katika kuwasaidia watu mbali mbali na kwamba, unashirikiana kwa karibu sana na Taasisi za Kipapa za Sayansi na Sayansi Jamii ili kutekeleza malengo haya!

Wadhamini pamoja na wafadhili wa Mfuko huu, Ijumaa, tarehe 8 Februari 2019 wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko ambaye amewashukuru na kuwapongeza kwa kuchangia kugharimia miradi mbali mbali inayotekelezwa na Mama Kanisa. Kwa njia hii, waamini walei wameweza kutekeleza wito na utume wao, kwa kusaidia kueneza Habari Njema ya Wokovu sehemu mbali mbali za dunia, ushuhuda unaopaswa kuendelezwa na kudumishwa!

Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu amewataka wanachama wa Mfuko wa Galileo kuchangia zaidi katika mchakato wa kuragibisha kuhusu madhara ya umaskini na unyonyaji unaofanywa kwa njia ya biashara ya binadamu pamoja na mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo. Tarehe 8 Februari, Kanisa linafanya kumbu kumbu ya Mtakatifu Josefina Bakhita, Msimamizi wa waathirika wa biashara ya binadamu. Katika maisha yake, alionja uchungu wa biashara ya utumwa, nyanyaso na madhara yake.

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwa kusema kwamba, Lakini kwa neema ya Mungu Bakhita akaweza pia kutambua ukweli, uhuru na furaha. Utakatifu wake wa maisha ni mwaliko na changamoto ya kupambana kwa ari na moyo mkuu dhidi ya mifumo yote ya utumwa mamboleo, ambayo inasababisha madonda makubwa kwa Fumbo la Mwili wa Kanisa na kwamba, huu ni uhalifu dhidi ya ubinadamu! Waamini wajifunze kutoka kwa Mtakatifu Bakhita, jinsi ya kuwahudumia maskini, kwa upendo, wema na huruma! Mwishoni, Baba Mtakatifu amewatakia heri na baraka wajumbe wa Mfuko wa Galileo kuendelea kutekeleza miradi yao kwa kujikita katika sala, ili waweze kuimarishwa zaidi kwa maombezi ya Mtakatifu Josefina Bakhita pamoja na nguvu za Roho Mtakatifu.

Mfuko wa Galileo

 

08 February 2019, 15:48