Tafuta

Papa Francisko awataka Mahakimu kusimamia haki, utu na heshima ya binadamu! Papa Francisko awataka Mahakimu kusimamia haki, utu na heshima ya binadamu! 

Mahakimu simamieni: haki, utu, na heshima ya binadamu!

Mahakimu wanayo nafasi ya pekee katika kuhakikisha kwamba, haki inatendeka ndani ya jamii. Baba Mtakatifu anatambua na kukiri changamoto mbali mbali wanazokabiliana nazo Mahakimu katika kutenda haki. Mosi ni upungufu mkubwa wa rasilimali fedha; masuala mtambuka kisheria; wingi wa sheria na tafsiri zake sahihi; hukumu ya kifo; haki za familia, wakimbizi na wahamiaji.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Chama cha Mahakimu Kitaifa Nchini Italia, mwaka huu 2019 kinaadhimisha Kumbu kumbu ya Miaka Mia Moja na Kumi, tangu kuanzishwa kwake, kunako mwaka 1909 changamoto na mwaliko wa kuangalia yaliyopita na kuyapembua kwa kina na mapana na hatimaye, kujiwekea malengo kwa siku za usoni. Kauli mbiu ya maadhimisho haya ni “Historia yetu kwa kuangalia ya mbeleni”. Mahakimu ni watu wanaotekeleza dhamana na wajibu wao kama walinzi wa demokrasia; wanaopaswa kukuza na kudumisha tunu msingi zinazofumbatwa katika Katiba ya nchi, sheria mama, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Utekelezaji wa tunu hizi msingi unafanyika kwa njia ya majadiliano katika ukweli na uwazi katika ngazi mbali mbali.

Takwimu zinaonesha kwamba, asilimia 90% ya Mahakimu wote ni watu wanaotekeleza dhamana na wajibu wao katika medani mbali mbali za maisha ya watu, kiasi kwamba, wanao ufahamu na uelewa mpana zaidi wa maisha ya wananchi na changamoto wanazokumbana nazo kila wakati! Ulimwengu mamboleo unazo changamoto zake zinazoendelea kusababisha kinzani katika maisha ya kijamii kiasi hata, cha watu kujitafuta wenyewe katika ubinafsi wao, hali inayopelekea kushamiri kwa vitendo vya uvunjifu wa sheria; tabia ya kutaka kulipiza kisasi kwa kujichukulia sheria mikononi; ongezeko la haki na wajibu kutokana na maendeleo ya teknolojia mpya. Kumbe, kuna haja ya kutii kwa hiyari bila shuruti sheria, kanuni na taratibu za nchi, ili kudumisha amani na utulivu.

Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, tarehe 9 Februari 2019 kwa Wajumbe wa Chama cha Mahakimu Kitaifa nchini Italia. Baba Mtakatifu anasema, Haki ni fadhila adilifu iliyo na utashi wa kudumu na thabiti wa kumpa Mwenyezi Mungu na jirani iliyo haki yao; kwa kuratibu mahusiano na mafungamano kuhusu watu, mali na jumuiya. Haki ni fadhila kuu inayokwenda sanjari na busara inayoiandaa akili ya kawaida kupambanua katika mazingira yote mema, yaliyo ya kweli na kuchagua njia za kuweza kuyafikia. Ni busara inayoongoza mara moja hukumu ya dhamiri. Kwa msaada wa fadhila hii Mahakimu hutumia misingi ya maadili katika masuala ya pekee bila kosa na kushinda mashaka juu ya mema ya kupata, na mabaya ya kuepuka.

Baba Mtakatifu anasema, bila haki, maisha ya kijamii yanakuwa ni “patashika nguo kuchanika”. Haki inapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza, kama njia ya kujenga na kudumisha amani. Mahakimu watambue kwamba, wanayo nafasi ya pekee katika kuhakikisha kwamba, haki inatendeka ndani ya jamii. Baba Mtakatifu anatambua na kukiri changamoto mbali mbali wanazokabiliana nazo Mahakimu katika kutenda haki. Mosi ni upungufu mkubwa wa rasilimali fedha; masuala mtambuka kisheria; wingi wa sheria na tafsiri zake sahihi; hukumu ya kifo; haki msingi za kifamilia pamoja na masuala ya haki msingi za wakimbizi na wahamiaji.

Changamoto zote hizi, zinawafanya Mahakimu kuwajibika barabara, huku wakiongozwa na dhamiri nyofu! Watu katika ulimwengu mamboleo wanapenda sana kupindisha ukweli na kusambaza habari za kughushi, kumbe, ni wajibu na dhamana ya Mahakimu kuhakikisha kwamba, wanasimamia na kulinda ukweli katika haki na matendo, bila kuchelewesha! Mahakimu wanapaswa kujiendeleza mara kwa mara katika medani mbali mbali za maisha ili kuweza kugundua mabadiliko yanayoendelea kujitokeza katika jamii na katika maisha ya watu, ili kwa hekima na busara waweze kutafsiri na hatimaye, kutoa hukumu ya haki kwa kuzingatia kanuni, sheria na taratibu zilizoko kwenye Katiba ya Nchi!

Baba Mtakatifu Francisko anawataka Mahakimu kufanya kazi kwa kushirikiana; kwa kutafuta na kudumisha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi na kamwe wasijitafutie mambo yao binafsi. Watekeleze wajibu wao kwa uhuru bila kuingiliwa na makando kando yanayoweza kuvuruga uamuzi wao! Mahakimu wafutilie mbali kishawishi cha kutaka kutoa upendeleo kutokana na mashinikizo pamoja na maagizo kutoka kwa “wakubwa”. Hukumu ikitolewa kwa haki inaacha chapa ya faraja, haki ikipindishwa, inawachia watu madonda makubwa nyoyoni mwao. Mahakimu wawe mstari wa mbele kulinda na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu.

Maandiko Matakatifu yanasema “maana hukumu haina huruma kwake yeye asiyeona huruma. Huruma hujitukuza juu ya hukumu”. Hukumu iwe na huruma kwa maskini na wanyonge; izingatie kanuni maadili na utu wema. Kimsingi, Mahakimu wanapaswa kuwa kweli ni mfano bora wa kuigwa hasa na vijana wa kizazi kipya. Baba Mtakatifu Francisko mwishoni anawapongeza Mahakimu wote waliopoteza maisha yao kwa kusimamia na kutenda haki!

Papa: Huruma na Haki

 

09 February 2019, 14:31