Tafuta

Vatican News
Papa Francisko anawaalika waamini kuwapenda adui zao ili waweze kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma na upendo wa Mungu duniani! Papa Francisko anawaalika waamini kuwapenda adui zao ili waweze kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma na upendo wa Mungu duniani!  (Vatican Media)

Wapendeni adui zenu, ili muwe vyombo vya huruma na upendo!

Amri ya Upendo, muhtasari wa mafundisho makuu ya Kristo Yesu, anakazia upendo kwa adui, kuwatendea mema wale wanaowachukia; kwa kuwabariki wale ambao wana walaani pamoja na kuwaombea wale wanaowaonea. Yesu anatambua fika kwamba, hii ni changamoto kubwa inayovuka uwezo wa wafuasi wake! Huu ndio mshikamano wa Fumbo la Umwilisho.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Yesu Kristo katika mafundisho yake kuhusu Amri ya Upendo, muhtasari wa mafundisho yake makuu, anakazia kwa namna ya pekee kabisa upendo kwa adui, kuwatendea mema wale wanaowachukia; kwa kuwabariki wale ambao wana walaani pamoja na kuwaombea wale wanaowaonea. Yesu anatambua fika kwamba, hii ni changamoto kubwa inayovuka uwezo wa wafuasi wake! Huu ndio mshikamano wa dhati unaofumbatwa katika Fumbo la Umwilisho, kielelezo cha mshikamano kati ya Kristo Yesu na mwanadamu mdhambi na dhaifu, ili waweze kupenda kama Mwenyezi Mungu anavyothubutu kupenda.

Huu ndio upendo unaotolewa na Kristo Yesu kwa wale wanaosikiliza kwa makini kwani ni kwa njia ya upendo na Roho wake Mtakatifu, wafuasi wa Kristo wanaweza kuthubutu kuwapenda hata adui zao! Ili kuweza kufikia katika hatua hii, kuna haja ya kuhakikisha kwamba, waamini wanajitahidi kuondoa ndani mwao chuki na uhasama, tayari kupandikiza mbegu ya upendo! Ikumbukwe kwamba, kilele cha upendo wa Kristo Yesu ni pale juu Mlimani Kalvari, alipoinamisha kichwa na kukata roho!

Upendo wa Kristo unawasukuma na kuwawajibisha waamini kwenda mbele zaidi kwa kutambua kwamba, wanaitwa kuwa ni vyombo vya huruma ya Baba yao wa mbinguni. Ili waamini kuweza kuwa kweli ni waana wa Mungu, kunahitajika jitihada za pekee kabisa, ili kuweza kulifikia lengo na hatimaye, kupata furaha ya kweli moyoni! Hii ni sehemu ya tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili, tarehe 24 Februari 2019 wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Hakuna sababu ya msingi kwa waamini kuwa wakatili kwa maneno na matendo, bali wanapaswa kugundua ndani mwao ile mbegu ya huruma na wema inayobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu na hivyo kuwafanya kuwa watu wa shukrani! Upendo ni kielelezo cha utu na heshima ya binadamu na kwamba, chuki na uhasama ni mambo yanayofifisha ule uzuri wa binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Waamini wanapaswa kuthubutu kujibu ubaya kwa kutenda wema, ili kujenga, kuimarisha na kumwilisha utamaduni wa huruma, chachu ya mapinduzi makubwa katika maisha ya mwanadamu.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, mashahidi na waungama imani wa nyakati zote wamekuwa ni mfano bora wa kuigwa na hatimaye, baada ya mapambano ya hapa duniani, Kristo Yesu, akawapatia tuzo mbinguni. Hawa ni watu waliotambua maana ya kusamehe pamoja na kutoa bila kudai malipo. Huu ni mwaliko kwa waamini kuwa wakarimu, vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu. Waamini wawe na ujasiri wa kusamehe na kusahau kwa kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu daima anawasamehe dhambi na mapungufu yao. Huruma, upendo na msamaha ni vifungo vya umoja na mshikamano wa kidugu unaoweza “kufyekelea” mbali ubaya wa moyo kwa kutenda mema.

Ni rahisi sana kwa mtu kukumbuka ubaya aliotendewa na kusahau mema ambayo mtu amewahi kupewa! Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, kwa hakika hii si njia njema. Inawapasa watu kukumbuka mema zaidi kama chachu ya huruma ya Mungu. Mwishoni, Baba Mtakatifu amemwomba Bikira Maria aweze kuwaombea waamini ili kwamba, Neno la Mungu linalowaka kama moto, liweze kuleta mageuzi ya watu kutenda wema, bila kungonja shukrani!

Papa: Upendo kwa adui
24 February 2019, 09:55