Tafuta

Mtakatifu Josephine Bakhita aliyekuwa mwathirika wa utumwa Mtakatifu Josephine Bakhita aliyekuwa mwathirika wa utumwa 

Baba Mtakatifu amekumbuka siku ya kupinga biashara ya binadamu na utumwa!

Baba Mtakatifu ametoa wito kwa serikali kudhibiti biashara ya binadamu na utumwa na kuwalinda wathirika na wakati huo amesali na waamini sala ya Mtakatifu Bakhita,kwamba asaidie wale wote walioangukia katika mtego wa utumwa.Ni mara baada ya sala ya Malaika wa Bwana tarehe 10 Februari 2019

Na Sr. Angela Rwezaula -Vatican

Siku mbili katika kumbukumbu ya Mtakatifu Josefina Bakhita ni mwaka  wa tano wa Siku ya kupinga  Biashara ya binadamu na utumwa. Kauli mbiu ya mwaka huu ni kwa pamoja kupambana  dhidi ya kupinga biashara ya utumwa. Kwa pamoja tupinge biashara na tusisahau hilo! Ni mwanzo wa maneno ya Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili  tarehe 10 Februari 2019  mara baada ya sala ya Malaika wa Bwana, akikumbusha Siku hii muhimu ya kupinga biashara ya Utumwa ambayo inaadhimishwa kila ifikapo tarehe 8 Februari ya kila mwaka, sambamba na kumbukumbu ya liturujia  ya Mtakatifu Josefina Bakhita ambaye ni mwathirika wa utumwa.

Akiendelea Baba Mtakatifu kuhimiza maana ya siku hii, anawaalika kuunganisha nguvu zote ili kushinda changamoto hii. Anawashukuru wadau wote ambao wanajikita kupambana na janga hili kwa namna ya pekee wamewataja watawa. Ametoa wito maalum kwa serikali zote duniani ili ziweze kukabiliana na maamuzi ya sababu zinazo sababisha janga hili na pia wapate kuwalinda waathirika wa utumwa. Aidha anasema kuwa lakini kwa wote inawezekana na lazima kushirikiana katika kutoa taarifa za kesi za unyanyaswaji na utumwa wa wanaume, wanawake na watoto. Baba Mtakatifu ameongeza kusema kwamba, sala ni nguvu inayosaidia jitahada za pamoja na kwa maana hiyo amewaalika kusali kwa pamoja, sala ya Mtakatifu Josefina Bakhita ambayo ilikuwa imesambazwa kawenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro na kwa wote wamesali…

Sala ya Mtakatifu Bakhita: Mtakatifu Bakhita ukiwa mtoto wa miaka 6 uliuzwa kama mtumwa na ukaweza kukabiliana na matatizo na mateso yasiyoelezeka. Mara baada ya kukombolewa kimwili, ulipata ukombozi wa kweli kwa kukutana na Kristo na Kanisa lake. Mtakatifu Bakhita, uwasaidie wote walioangukia  katika mtego wa utumwa. Kwa jina lao uwaombee kwa Mungu wa huruma, ili minyororo ambayo imewafunga iweze kukatika. Mungu aweze kuwakomboa wote ambao wako hatarini, wamejeruhiwa au wananyanyaswa na utumwa mamboleo na biashara ya binadamu. Leta faraja kwa wale ambao wameweza kukombolewa kutoka utumwani na uwafundishe wamtazame Yesu kama mfano wa imani na matumaini, kwa kufanya hivyo wanaweza kuponya majeraha yao. Tunakuomba usali na kutuombea sisi sote, ili tusiangukie katika utofauti, kwa sababu tunaweza kufungua macho ili kutazama suluba na majeraha ya kaka na dada wanaokosa hadhi na uhuru wao na usikilize kilio chao. Amina. Mtakatifu Josefina Bakhita utuombee.

Mara baada ya sala hiyo amewasalimia mahujaji wote waliofika toka pande zote za dunia na kuwatakia Jumapili njema lakini wasisahau kusali kwa ajili yake.

 

11 February 2019, 10:46