Tafuta

Baraza Maaskofu Katoliki India: Mkutano mkuu wa mwaka 2019: Kutangaza na kushuhudia Furaha ya Injili Baraza Maaskofu Katoliki India: Mkutano mkuu wa mwaka 2019: Kutangaza na kushuhudia Furaha ya Injili 

Papa: Maaskofu tangazeni & kushuhudia Furaha ya Injili!

Waraka wa Kitume wa Papa Francisko “Furaha ya Injili”, unatoa kipaumbele cha kwanza kwa furaha ya Injili, kwa kuwaalika waamini kushirikisha furaha yao inayopata chimbuko kutoka katika huruma na upendo wa Mungu kwa wanadamu. Katika mwono huu, Kristo ni kiini cha Injili na kwamba, Kanisa linaalikwa kufanya mageuzi makubwa kama sehemu ya Uinjilishaji Mpya.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wa Kitume “Evangelii gaudium” yaani “Furaha ya Injili”, anatoa kipaumbele cha kwanza kwa furaha ya Injili, kwa kuwaalika waamini kushirikisha furaha yao inayopata chimbuko kutoka katika huruma na upendo wa Mungu kwa wanadamu. Katika mwono huu, Kristo ni kiini cha Injili na kwamba, Kanisa linaalikwa kufanya mageuzi makubwa kama sehemu ya Uinjilishaji Mpya. Waraka huu ni ramani inayotoa dira na mwongozo thabiti wa shughuli za kichungaji unaopaswa kutekelezwa na Mama Kanisa kwa sasa na kwa siku za usoni kwa kuwa na mwono wa kinabii na mwelekeo chanya, licha ya vikwazo na changamoto zinazoendelea kujitokeza katika maisha na utume wa Kanisa, ili Kristo Mfufuka aendelee kupeperusha bendera ya ushindi.

Waraka huu wa kitume unachota utajiri wake katika mapendekezo yaliyotolewa na Mababa wa Sinodi juu ya Uinjilishaji Mpya kama njia ya kutangaza na kushuhudia Imani ya Kikristo katika ulimwengu mamboleo. Baba Mtakatifu Francisko, akayasoma na kuyafanyia tafakari ya kina na hatimaye kuyaweka kuwa ni sehemu ya ujumbe wake kwa Familia ya Mungu wakati huu inapojielekeza katika hija ya uinjilishaji mpya, kwa kutambua kwamba, Yesu Kristo ndiye kiini cha uinjilishaji na ndiye Mwinjilishaji Mkuu. Wakristo wanahamasishwa kushiriki kikamilifu katika kazi ya ukombozi iliyoanzishwa na Yesu mwenyewe katika mazingira mapya ya uinjilishaji.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwenda kwa Baraza la Maaskofu Katoliki India, CCBI lililoanza Mkutano wake mkuu hapo tarehe 7 Januari na unatarajiwa kufungwa rasmi hapo tarehe 15 Januari 2019, anakazia umuhimu wa Kanisa kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili kwa familia ya Mungu nchini India. Anawaalika Maaskofu kukutana upya na Kristo Yesu katika hija ya maisha yao na kumpatia nafasi, ili aweze kupyaisha maisha na vipaumbele vyao, ili waendelee kuwa ni vyombo na mashuhuda wa furaha ya Injili.

Baba Mtakatifu anawaombea ili kwamba, majadiliano yao katika ukweli na uwazi, yaweze kuzaa matunda ya huduma kwa watu wa Mungu nchini India, wakati huu wanapoendelea kujizatiti kukua na kukomaa katika imani, matumaini na mapendo. Wawe wadumifu na washiriki wa Sakramenti za Kanisa, ili hatimaye, waweze kuishi wito na dhamana yao kama Wakristo mintarafu mwanga wa furaha ya Injili. Baba Mtakatifu anauweka mkutano mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki India nchini ya: maombezi, ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Nyota angavu ya uinjilishaji mpya.

Wakati huo huo, Askofu mkuu Giambattista Diquattro, Balozi wa Vatican nchini India katika hotuba yake elekezi, amelitaka Baraza la Maaskofu Katoliki India kujikita katika mchakato wa kusoma alama za nyakati, ili kusikiliza na kujibu kilio cha mahitaji msingi ya familia ya Mungu nchini India, kama chemchemi ya furaha ya Injili. Maaskofu wanatakiwa kuwa ni mashuhuda na vyombo vya furaha ya Injili kwa watu wa Mataifa, kama sehemu ya uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Huu ni ushuhuda wa maisha na upendo katika utume kwa Kristo na Kanisa lake. Baraza la Maaskofu Katoliki India linaloundwa na Majimbo 132 yanayohudumiwa na Maaskofu 189, ni kati ya Mabaraza makubwa ya Maaskofu Katoliki Barani Asia. Wakati huu, linapembua mbinu mkakati wa uinjilishaji mpya, matatizo, changamoto na fursa za uinjilishaji nchini India.

Papa: India
11 January 2019, 10:05