Baba Mtakatifu Francisko atakuta Kanisa hai linalojipambanua kwa huduma bila upendeleo! Baba Mtakatifu Francisko atakuta Kanisa hai linalojipambanua kwa huduma bila upendeleo! 

Siku ya XXXIV Vijana Duniani 2019: Ushuhuda wa Kanisa la huduma!

Kwa hakika, Baba Mtakatifu atakutana mubashara na Kanisa hai, linalotoka kimasomaso kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Injili ya huduma kwa wote bila ubaguzi! Baba Mtakatifu ataweza kushuhudia sura za vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia wakati wa maadhimisho ya Siku ya XXXIV ya Vijana Duniani kwa mwaka 2019 huko Panama! Yaani, we acha tu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Siku ya XXXIV ya Vijana Duniani huko Panama kuanzia tarehe 22 - 27 Januari 2019 yanaongozwa na kauli mbiu “Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; iwe kwangu kama ulivyosema”. Lk. 1:38. Katika hija hii, vijana wanasindikizwa kwa mfano na maombezi ya Bikira Maria, aliyeteuliwa na Mwenyezi Mungu kuwa Mama wa Mwanaye Mpendwa, Kristo Yesu. Bikira Maria anaendelea kufanya hija pamoja na waamini kwa kuwaongoza vijana wa kizazi kipya katika imani na udugu.

Ratiba elekezi ya Hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Panama inaonesha kwamba, Papa ataondoka Roma, Jumatano tarehe 23 Januari 2019 asubuhi na kuwasili majira ya jioni kwenye Uwanja wa Ndege wa Tocumen nchini Panama. Baba Mtakatifu atakaribishwa rasmi na viongozi wa Serikali na Kanisa na baadaye ataelekea kwenye Ubalozi wa Vatican nchini Panama kwa mapumziko.

Askofu mkuu Josè Domingo Ulloa Mendieta wa Jimbo kuu la Panama katika mahojiano maalum na Vatican News anasema, familia ya Mungu nchini Panama iko tayari kuwakaribisha vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia pamoja na kumpokea Baba Mtakatifu Francisko. Kwa hakika, Baba Mtakatifu atakutana mubashara na Kanisa hai, linalotoka kimasomaso kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Injili ya huduma kwa wote bila ubaguzi! Baba Mtakatifu ataweza kushuhudia sura za vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia.

Maandalizi ya ujio wa Baba Mtakatifu nchini Panama kwanza kabisa yamejikita katika sala, utume ambao umetekelezwa na familia ya Mungu nchini Panama tangu walipotangaziwa kuhusu maadhimisho haya nchini mwao! Kwa muda wa miaka miwili, wamesali na kumwomba Mtakatifu Yohane Paulo II awasaidie kutekeleza ndoto na matamanio halali ya vijana wakati wa maadhimisho ya Siku ya XXXIV Duniani kwa Mwaka 2019. Kanisa nchini Panama linaendelea kujieleza zaidi katika kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani, ni fursa kwa Mama Kanisa kukuza na kudumisha utume wake miongoni mwa vijana wa kizazi kipya: kwa kuwasikiliza, kuwasindikiza na kuwasaidia kufanya maamuzi magumu katika maisha yao kadiri ya mwanga wa Injili ya Kristo na Mafundisho Jamii ya Kanisa. Kwa mwaka huu, mkazo wa pekee ni kwa ajili ya vijana kutoka Amerika ya Kati, wanaokabiliana na changamoto mbali mbali katika maisha na utume wao.

Askofu mkuu Josè Domingo Ulloa Mendieta anaendelea kufafanua kwamba, vijana kutoka Amerika na Marekani wataweza kutumia fursa hii kuweza kushiriki kikamilifu. Kwa wale ambao kutokana na sababu mbali mbali hawataweza kuhudhuria, Kanisa limejiandaa barabara kuwashirikisha yale yanayojiri kwa njia ya mitandao ya kijamii. Lengo ni kutaka kuwasaidia vijana kuzima kiu ya maisha yao ya ndani kwa kukutana na Kristo Yesu katika safari ya maisha yao, tayari kuandika mpango mkakati mpya wa maisha, kwa kumshirikisha Kristo Yesu.

Maaskofu: Panama 2019
14 January 2019, 13:27