Tafuta

Sherehe ya Tokeo la Bwana, Kanisa pia linatangaza Mbiu ya Fumbo la Pasaka kwa mwaka 2019 Sherehe ya Tokeo la Bwana, Kanisa pia linatangaza Mbiu ya Fumbo la Pasaka kwa mwaka 2019 

Mbiu ya Fumbo la Pasaka kwa Mwaka 2019

Katika hija ya maisha ya kila siku, waamini wanajitahidi kumwilisha Fumbo la Ukombozi, kiini cha maadhimisho haya ni Liturujia ya Mwaka wa Kanisa, lakini kwa namna ya pekee, Siku kuu tatu zinazoonesha: Mateso, kifo na ufufuko wa Kristo kutoka kwa wafu, yaani Sherehe ya Pasaka ambayo kwa Mwaka huu itaadhimishwa hapo tarehe 21 Aprili 2019.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Sherehe ya Tokeo la Bwana, yaani Epifania ni kati ya Sherehe kubwa zinazoadhimishwa na Mama Kanisa katika Liturujia ya Mwaka wa Kanisa. Mtoto Yesu aliyezaliwa na Bikira Maria anajifunua kwa mataifa kama Mwana wa Mungu, Masiha na Mwanga wa Mataifa. Mama Kanisa katika Maadhimisho ya Siku kuu ya Tokeo la Bwana, anatangaza pia Fumbo la Pasaka, linaloonesha kwa namna ya pekee, utukufu wa Kristo kati ya watu wake hadi pale atakapokuja tena kuwahukumu wazima na wafu.

Katika hija ya maisha ya kila siku, waamini wanajitahidi kumwilisha Fumbo la Ukombozi, kiini cha maadhimisho haya ni Liturujia ya Mwaka wa Kanisa, lakini kwa namna ya pekee, Siku kuu tatu zinazoonesha: Mateso, kifo na ufufuko wa Kristo kutoka kwa wafu, yaani Sherehe ya Pasaka ambayo kwa Mwaka huu itaadhimishwa hapo tarehe 21 Aprili 2019.  Kila Jumapili, Mama Kanisa anaadhimisha Pasaka ya Bwana na kuwawezesha waamini kuendelea kuadhimisha tukio hili kuu katika maisha na imani yao; kwani Kristo ameshinda dhambi na mauti.

Sherehe ya Pasaka ni chemchemi ya Siku kuu nyingine zote zinazoadhimishwa na Mama Kanisa. Kipindi cha Kwaresima kwa mwaka huu, kitaanza rasmi tarehe 6 Machi 2019 kwa kupakwa majivu, mwaliko wa toba na wongofu wa ndani. Mama Kanisa ataadhimisha Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni hapo tarehe 2 Juni 2019 na Sherehe Pentekoste yaani Siku kuu ya kuzaliwa kwa Kanisa na Siku ya waamini walei itaadhimishwa hapo tarehe 9 Juni 2019. Jumapili ya kwanza ya kipindi cha Majilio ambayo kimsingi ni mwanzo wa Mwaka Mpya wa Kanisa, na maandalizi ya ujio wa Kristo itaadhimishwa hapo tarehe 1 Desemba 2019.

Mama Kanisa anayeendelea kufanya hija yake hapa duniani anatangaza pia Pasaka ya Bwana, anapoadhimisha Siku kuu za Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa; Siku kuu za Mitume na Watakatifu mbali mbali; anapowakumbuka watoto wake waliotangulia katika usingizi wa amani, wakiwa na tumaini katika ufufuko wa wafu. Sifa na utukufu kwa Kristo aliyekuwepo, aliyepo na atakayekuja. Yeye ni Bwana wa Historia na nyakati zote ni zake. Amina.

Wakati wa Sala ya waamini, Kanisa limesali ili kuwaombea viongozi wa Kanisa ili waweze kutangaza ukweli wa Injili kwa watu wa Mataifa; limewaombea watunga sheria, ili waweze kuwa watii katika kuhudumia utu wa kila mtu. Kanisa limewaombea wakristo wanaoteseka sehemu mbali mbali za dunia, ili waendelee kuimarika na kamwe wasikate tamaa na kurejea nyuma; wanasayansi nao pia wamekumbukwa katika sala za waamini, ili waweze kuondokana na maamuzi mbele pamoja na sera zinazokinzana na uzuri na utakatifu wa Mungu aliyejifunua kwa njia ya Kristo Yesu. Mwishoni, Kanisa limesali na kuwaombea wadhambi, kwa kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu hafurahii kifo cha mdhambi, aguse nyoyo zao kwa neema yake, awaongoe katika maisha yao na kuwafariji kwa furaha ya msamaha! Ombi hili kwa lugha ya Kiswahili limesomwa na Padre Innocent Miku, C.PP.S.

Fumbo la Pasaka 2019
07 January 2019, 08:01